Ni wa majaribio katika wilaya 40
Maswali mengine yakosa majibu
12 yamtoa jasho Profesa UDSM
Madudu zaidi yamebainika katika Wizara ya Elimu
na Mafunzo ya Ufundi, baada ya mtihani wa kujipima wa darasa la saba uliofanyika
Julai, mwaka huu katika wilaya 40 za Tanzania Bara kuwa na mapungufu makubwa na
ya wazi.
Aidha, maswali 12 kati ya 50 katika mtihani wa
Hisabati hayana majibu, 14 ni magumu ambayo mtoto wa darasa la saba hawezi
kuyajibu na mengine matano yamekosewa na hata yafanywe kwa kiasi gani hayawezi
kuwa na majibu.
Mbunge wa Kuteuliwa
(NCCR-Mageuzi), James Mbatia, alibainisha madudu hayo jana wakati akizungumza na
waandishi wa habari ofisini kwake na kuwataka Watanzania kushiriki kupinga
anguko la elimu linalotia aibu Taifa.
Mbatia alibainisha
kuwa katika mtihani huo uliofanywa Julai 8 na 9, mwaka huu, kwa masomo ya
Hisabati, Kiswahili na Kiingereza, jina la Wizara limeandikwa ni Wizara ya Elimu
na Mafunzo ya Ufundi Stadi huku usahihi hakuna neno
Stadi.
Alisema matokeo hayo
yamekuja katika kipindi ambacho serikali iko katika dhana ya matokeo makubwa
sasa (big result now), katika sekta ya elimu na mtihani huo umetungwa kwa dhana
hiyo.
Alisema baada ya
kupata mtihani huo, alikusanya baadhi ya walimu wa shule za msingi na sekondari
katika moja ya shule jijini Dar es Salaam na kuufanya na zaidi ya nusu
walishindwa kupata daraja la tatu yaani C.
“Sikuishia hapo,
nilimtafuata msomi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) yaani Profesa na kumpa
mtihani wa hesabu aliufanya kwa muda wa saa 2:03, lakini na hakupata daraja la
kwanza, alishindwa kujibu baadhi ya maswali na mengine kukosa majibu kabisa,”
alisema.
Kwa mujibu wa Mbatia,
Profesa huyo alisema swali namba 33 ni gumu ambalo linafanywa na mwanafunzi wa
fani ya uhandisi na linahitaji muda mrefu kupata jibu.
“Sikutaka kuridhika
na majibu yao, nilijifungia ofisini majira ya asubuhi kwa saa 2:30 na kuufanya
mtihani wote nikalinganisha na majibu ya wengine, lakini sikupata alama
A…ninachojiuliza hii ndiyo Big Result Now?” alibainisha na
kuhoji.
Katika somo la
Kiingereza, kulikuwa na mapungufu makubwa ya kisarufi na majina ikiwamo historia
ya Tanzania kwa viongozi wa Taifa kama Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Amani
Karume.
Mbatia alisema jina
la Mwalimu Nyerere limekosewa na kuandikwa Julias na Rais wa awamu ya Pili
likiandikwa Ally Mwinyi badala ya Ali Hassan Mwinyi, huku wakishindwa kueleza
kifo cha Karume na kueleza kama kifo cha kufanana na Mwalimu Nyerere.
Itakumbukwa kwamba, Mwalimu Nyerere alifariki dunia baada ya kuugua wakati
Karume aliuawa.
Aidha, alisema katika
mtihani wa Kiswahili, kuna mapungufu mengi hususani ya usahihi wa lugha na
kuwafanya Watanzania kujiuliza kama mitihani hiyo ilitungwa na wanataaluma
walibobea au ni ubabaishaji.
Alisema suala hilo
linakwenda sambamba na makosa yaliyopo kwenye vitabu vinavyotumiwa na wanafunzi
wa shule za msingi hadi sekondari ambavyo vimepitishwa na kupewa cheti cha
ithibati.
“Tumefika mahali
pagumu kielimu yaani ni janga la kitaifa,” alisema
Mbatia.
Alisema kitabu cha
uraia cha darasa la nne, kuna mahali kimeandikwa ‘Serikali za mitaa zinaongozwa
na viongozi wa vitongoji’ huku cha hesabu kikieleza namba nzima ni moja hadi 99
badala ya moja hadi tisa.
“Haya yote wanalishwa
watoto wa maskini wa nchi hii, hakuna mtoto wa kigogo anayesoma kwenye shule
hizi na hawajafanya mitihani hii,” alisema.
MAPENDEKEZO YA
MBATIA
Kuundwa kwa tume ya
kudumu ya elimu nchini, itakayoshughulika pamoja na mambo mengine, kuhakikisha
ubora wa elimu nchini na kudhibiti mambo yote yanayosababisha kutetereka kwa
ubora huo (Education quality assurance and control).
Aliongeza kuwa tume
hiyo iwe na mamlaka ya kuhakiki utendaji wa taasisi mbalimbali za elimu ambazo
hadi sasa zimeonekana kutotimiza vyema majukumu yake.
“Tume itakapoundwa
inaweza vile vile kusaidia kubainisha wazi ni nini falsafa na malengo hasa ya
utoaji wa elimu nchini kulingana na wakati tulionao,”
alisema.
Januari 31, mwaka
huu, Mbunge huyo aliwasilisha hoja binafsi bungeni kuhusu udhaifu uliopo katika
sekta ya elimu nchini.
Alianisha sura hizo
ni kuporomoka kwa uwajibikaji, kutokuthamini rasilimali za Taifa, kukithiri kwa
ukiukwaji wa haki za binadamu, kumomonyoka kwa uadilifu miongoni mwa watumishi
wa umma na kupungua kwa uzalendo.
Hata hivyo, hoja hiyo
haikutiliwa maanani ingawa siku chache baada ya hoja hiyo, Wizara ilifuta Kamati
ya Uthibitishaji ya Vifaa vya Elimu (Emac).
Aidha, Februari 18,
mwaka huu, Wizara hiyo ilitangaza matokeo ya kidato cha nne yaliyonyesha zaidi
ya watahiniwa 240,000 walipata daraja sifuri ikiwa ni asilimia 66 na baadaye
matokeo hayo yalipangwa upya na watahiniwa 210,000 wakapata daraja la
sifuri.
Kwa mujibu wa matokeo
ya ualimu ngazi ya Astashahada na Shahada yaliyotangazwa na Baraza la Mitihani
Tanzania (Necta), Julai, mwaka huu, watahiniwa 2,606 wa Stashahada wanarudia
mtihani na 533 wamefeli.
Msemaji wa Wizara ya
Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Ntambi Bunyazu, alipotafutwa na NIPASHE,
alithibitisha mitihani hiyo kufanyika katika halmashauri 40 nchini na kusema
kwamba asingeeleza undani wa makosa yaliyobainika hadi atakapopata ufafanuzi wa
kitaalam.
No comments:
Post a Comment