Blog ya kijanja kwa ajili ya watu wajanja

Blog ya kijanja kwa ajili ya watu wajanja

Wednesday, August 7, 2013

MKENYA ALIYETUHUMIWA KUMTEKA DR. ULIMBOKA AFUTIWA KESI

Jamaa aliyekuwa akidaiwa kumteka na kumtesa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari nchini, Dk. Steven Ulimboka afutiwa mashtaka, hili ndo sakata ambalo Sugu alimwambia Kamanda Kova arudi studio kuisuka ngoma yake upya maana kitaa haikueleweka, ungana na mwanandishi Happiness Katabazi katika gazeti la Tanzania Daima kuhusiana na sakata hilo anaripoti hivi:
 
MKURUGENZI wa Mashitaka nchini (DPP), Dk. Eliezer Feleshi, amefuta kesi ya kuteka na kujaribu kumuua Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari nchini, Dk. Steven Ulimboka, iliyokuwa ikimkabili raia wa Kenya, Joshua Mulundi, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.
 
 
Hatua hiyo imeelezwa kuwa ni baada ya DPP kuona hana haja ya kuendelea kumshitaki kwa makosa hayo ambayo yalikuwa hayana dhamana.
 
Hati hiyo ya DPP iliwasilishwa chini ya kifungu cha 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2002 kwa niaba yake na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Tumaini Kweka, jana mbele ya Hakimu Mkazi Waliarwande Lema.
 
Kweka aliiambia mahakama kuwa kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya kutajwa lakini upande wa Jamhuri hauna nia tena ya kuendelea kumshitaki Mulundi kwa kesi hiyo.
 
Hakimu Lema alikubaliana na hoja hiyo na akamfutia kesi hiyo Mulundi ambaye yupo gerezani tangu Julai 13, mwaka jana.
 
 
Hata hivyo muda mfupi baada ya Hakimu Lema kumfutia kesi hiyo Mulundi, askari kanzu walimkamata tena na kumfikisha kwa Hakimu Mkazi, Alocye Katemana na kisha Wakili Kweka akaiambia mahakama kuwa upande wa Jamhuri umemfungulia kesi mpya ambayo itakuwa na shitaka moja tu.
 
 
Mbele ya Hakimu Katema, wakili huyo alidai kuwa Julai 3, mwaka jana, Mulundi katika Kituo cha Polisi Oystebay alitoa taarifa za uongo kwa ofisa wa polisi kuwa yeye na wenzake walikodiwa kwenda kumteka na kumjeruhi Dk. Ulimboka, jambo ambalo si kweli.
 
 
Alidai kosa hilo ni kinyume cha kifungu cha 122 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002 na kuongeza kuwa upelelezi wa kesi hiyo mpya umekamilika.
 
 
Wakili Kweka alidai licha ya kosa hilo kuwa na dhamana kwa mujibu wa sheria, lakini upande wa Jamhuri unaomba Mulundi asipewe dhamana kwa ajili ya usalama wake.
 
Hakimu Katemana aliiahirisha kesi hiyo kwa muda na kisha kuutaka upande wa Jamhuri uende ukalete kwa maandishi hati ya kumfungia dhamana mshitakiwa huyo.
 
Hata hivyo mshitakiwa huyo alikanusha shitaka hilo na akaomba apewe dhamana kwani alikuwa na wadhamini. Pia alidai amesota muda mrefu gerezani bila kosa.
 
“Ninajua wanataka kunifungia dhamana makusudi ili waweze kunyamazisha Bunge na umma usiendelee kupiga kelele kuhusu tukio la kupigwa na kuteswa kwa Dk. Ulimboka na kwa taarifa yenu mkinipeleka tena gerezani naenda kuanza mgomo …nimechoka kuonewa,” alidai Mulundi.
 
 
Hata hivyo kesi hiyo iliporudi tena mchana, Wakili Kweka hakuweza kuja na hati ya kuzuia dhamana, hali iliyosababisha Hakimu Katemana kutoa masharti ya dhamana kwa mshitakiwa huyo.
Hata hivyo mshitakiwa huyo jana alishindwa kutimiza masharti hayo na Hakimu Katemana aliahirisha kesi hiyo hadi Agosti 20, mwaka huu.
 
 
Katika kesi hiyo awali, Wakili wa Serikali, Ladslaus Komanya, mbele ya Hakimu Agnes Mchome, alidai kuwa Mulundi Juni 26, mwaka jana, akiwa eneo la Leaders Club alimteka Dk. Ulimboka.
Katika shtaka la pili, Komanya alidai kuwa Juni 26, mwaka huu, akiwa katika eneo la Msitu wa Mabwepande, Tegeta, Dar es Salaam, kinyume cha sheria, mshtakiwa huyo alijaribu kumsababishia kifo Dk. Ulimboka.
 
Chanzo: Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment