WIKI moja tangu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Prof.
Sifuni Mchome, atangaze mfumo mpya wa upangaji alama za matokeo ya wanafunzi wa
sekondari kwa kufuta daraja sifuri na kuanzisha daraja la tano, naibu waziri
ameibuka na kupingana naye.
Naibu waziri huyo, Philipo Mulugo, aliibua mkanganyiko huo bungeni jana,
akisema si kweli kwamba serikali imefuta daraja la sifuri katika mitihani ya
kidato cha nne kama ilivyoeleweka.
Kutokana na kukinzana huko, Spika wa Bunge, Anne Makinda aliiagiza serikali
kuleta bungeni mabadiliko ya madaraja hayo ya ufaulu kwa wanafunzi wa kidato
cha nne na sita yaliyotangazwa hivi karibuni.
“Naibu Waziri nenda mtuletee kauli ya Serikali kuhusiana na utaratibu huo ili
kuweza kupata majibu ambayo yanaridhisha,” alisema.
Awali akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalumu, Catherine Magige
(CCM), Mulugo alisema taarifa zilizoenea kwamba daraja la sifuri limefutwa si za
kweli.
Katika swali lake, Magige alitaka kujua kama uamuzi wa serikali wa kushusha
madaraja katika mitihani ya kidato cha nne lengo lake ni kuwaokoa wanafunzi
wanaofeli.
“Serikali haijafuta divisheni sifuri na wala hakuna daraja la tano, yaliyopo
ni la kwanza, pili, tatu, nne na sifuri kama kawaida,” alisema.
Alisema unamuzi wa kushusha madaraja uliofanywa haukuwa na lengo la kuwaokoa
wanafunzi wanaofeli bali ni kuondoa mrundikano wa alama katika daraja moja.
Alisema serikali imeweka madaraja mapya kwa kutofautisha alama kumi kumi
kutoka daraja moja kwenda jingine na kwamba hata hivyo alama za ufaulu bado ni
40 ambazo ni daraja la C.
Awali akijibu swali la msingi la Magige, Mulugo alisema serikali haina mpango
wa kuanzisha programu maalumu hasa za ufundi kwa wanafunzi waliofeli katika
mtihani wa kidato cha nne mwaka jana.
“Kwa mwaka 2013, jumla ya wanafunzi 60,507 wa kujitegemea, wamejisajili
kufanya mtihani huo, watahiniwa 3,578 wakiwamo wasichana 2,020 na wavulana 1,558
waliofeli katika mtihani wa kidato cha nne mwaka jana wamejisajili kurudia
mtihani huo,” alisema.
Alisema kwa sasa katika vyuo vya Ufundi Stadi kuna programu za fani
mbalimbali za muda mfupi na muda mrefu ambazo wanafunzi waliomaliza elimu ya
msingi na sekondari wanaweza kujiunga kwa vile mafunzo yatolewayo katika vyuo
hivyo huzingatia stadi moja tu.
“Serikali imekuwa ikiongeza na kuboresha vyuo vya ufundi na kuweka mazingira
rahisi kwa wanafunzi ili waweze kupata stadi mbalimbali,” alisema.
Mulugo aliongeza kuwa kati ya mwaka 2010 hadi 2012, serikali kupitia VETA
imesajili jumla ya vyuo vya Ufundi Stadi 75 sawa na asilimia 75 na asilimia 10.8
ya vyuo 618 vilivyokuwapo.
Naibu waziri huyo alifafanua kuwa katika kipindi hicho, jumla ya vyuo vinane
sawa na asilimia 3.2 ya vyuo 248 vilivyokuwepo vilisajiliwa na NACTE.
Via : Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment