MBUNGE wa Maswa Magharibi, John Shibuda (CHADEMA), ametimuliwa katika kikao
cha ndani ya chama hicho Kanda ya Ziwa Mashariki kwa madai ya usaliti.
Uamuzi wa kutimuliwa kwa mwanasiasa huyo ulifikiwa juzi jioni mkoani
Shinyanga wakati Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, alipokutana na viongozi
wa kanda hiyo katika kikao cha ndani kwa ajili ya mikakati ya ujenzi wa
chama.
Akizungumzia tukio hilo, Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Ziwa Mashariki,
Silvester Kasulumbai, alisema kuwa katika mkutano huo uliowahusisha viongozi wa
mikoa ya Shinyanga, Simiyu na Mara, kabla ya Shibuda kutimuliwa, Mbowe alimpa
nafasi ya kutetea tuhuma zilizotolewa dhidi yake ikiwamo sababu ya kuhudhuria
majukwaa ya mikutano ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
“Mmoja wa wajumbe alisimama na kutoa hoja ya kuwa kikao hicho hakiwezi
kuendelea kujadili masuala ya msingi ya chama ilhali kukiwa na watu wanaotoa
taarifa kwa CCM na ghafla akamtaja mtu huyo kuwa ni Shibuda,” alisema.
Kasulumbai aliongeza kuwa mtoa hoja alisisitiza kuwa Shibuda alipanda katika
jukwaa moja na viongozi wa CCM na kudai kuwa vyama vya upinzani havina kitu,
kwamba CCM ndicho chama tawala, hali aliyoeleza kuwa hata mikakati itakayopangwa
katika mkutano huo anaweza kuivujisha na hivyo kumtaka Mbowe amtoe nje ya kikao
hicho.
Kwa mujibu wa Kasulumbai ambaye pia ni Mbunge wa Maswa Mashariki, baada ya
hoja hiyo Mbowe aliwataka wajumbe wasiwe na jazba na wampe nafasi Shibuda ili
aweze kujitetea dhidi ya tuhuma zilizoelekezwa kwake.
Alisema baada ya Shibuda kupewa nafasi alieleza kuwa yeye kupanda katika
jukwaa la CCM si jambo la ajabu katika masuala ya kisiasa na kutolea mfano hatua
ya wenyeviti wa vyama vitatu vya CHADEMA, NCCR-Mageuzi na CUF kukutana na Rais
Jakaya Kikwete Ikulu huku wakijua kuwa ni mwenyekiti wa CCM.
Kasulumbai alisema katika utetezi wake, Shibuda alisema kwamba mtu mzima
anapokuwa na shida yoyote hukimbilia kwa baba yake na kumaainisha baba huyo ni
chama kinachotawala yaani CCM.
Aliongeza kuwa kauli ya Shibuda iliwakasirisha wajumbe na kuwaudhi zaidi,
hivyo kuanza kumshambulia kwa maneno hali iliyomfanya Mbowe kuingilia kati na
kuwataka wajumbe kupiga kura kwa ajili ya kufikia hitimisho juu ya uwepo wake
katika kikao hicho.
“Zilipigwa kura akapata kura 38 zilizotaka aendelee kubaki ndani, tano
ziliharibika na 90 zilitaka aondolewe katika kikao na wajumbe wakamuomba Mbowe
afanye utaratibu wa kumuondoa kwa amani,” alisema Kasulumbai.
Alipotafutwa kwa simu jana kuzungumzia tuki hilo, Shibuda alisema wanachama
na wafuasi wa CHADEMA walimuelewa vibaya alipopanda jukwaani katika mkutano wa
CCM mjini Geita.
Alisema wakati alipopanda jukwaani na kuonana na viongozi wa CCM, alikuwa
akiwakilisha kilio cha wakulima wa pamba wa Kanda ya Ziwa.
“Mimi ni mlezi wa wakulima wa pamba Kanda ya Ziwa na pale nilimfuata Katibu
wa CCM nikamueleza kuwa akamwambie mwenyekiti wake, Rais wa nchi kwamba tunapata
taabu na masilahi kidogo kwa kuwa tunanyonywa na wajanja katika kilimo cha
pamba,” alisema.
Kwa mujibu wa Shibuda, kitendo hicho angekifanya kwa kiongozi wa chama
chochote kilicho madarakani kwa kile alichoeleza kuwa ilani ya wakati
itakayokuwa inatekelezwa ni ya chama husika.
Aliongeza kuwa kwa nafasi yake ya mbunge anayetokana na CHADEMA hoja yoyote
atakayoipeleka serikalini na kufanikiwa zitakuwa ni juhudi za chama badala ya
watu kumfikiria kuwa msaliti.
“Kuna waganga njaa ndio wanaendekeza mifarakano ndani ya chama na hii ipo
katika vyama vyote, wanafanya hivi si kwa sababu ya masilahi ya chama na nchi
bali kuhakikisha matumbo yao yanashiba wakati wote kwa kuendekeza misigano isiyo
na ulazima,” alisema.
Aliongeza kuwa kama hatua ya kutaka kuwatetea wakulima wa pamba Kanda ya Ziwa
ni usaliti atakuwa tayari kuhukumiwa na kufukuzwa kwa hatua hiyo.
Via: Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment