UMOJA wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM), umeutia doa mkutano wa Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, na waandishi wa habari uliofanyika juzi katika hoteli ya Serena baada ya maandalizi na uratibu wake kusimamiwa na vijana wa umoja huo.
Vijana hao wa UVCCM ambao ndio waliosimamia mkutano huo, walipata kuwa wanachama na viongozi wa CHADEMA lakini baadaye walienguliwa kwa makosa ya usaliti na baadaye kujiunga na UVCCM.
Vijana hao ni pamoja Juliana Shonza aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Umoja wa Vijana CHADEMA (BAVICHA), Tanzania Bara, Mtela Mwampamba, na Habib Mchange waliokuwa wanachama wa kawaida.
Mwampamba na Machage ndio waliokuwepo ukumbini juzi na ndio waliosimamia mkutano huo wa Zitto na Dk. Kitilla ambao waliutumia kufafanua na kujisafisha tuhuma zilizoelekezwa kwao na Kamati Kuu ya CHADEMA, iliyoamua kuwavua nyadhifa zao za uongozi na kubaki wanachama.
Vijana hao waliofukuzwa uanachama wa CHADEMA kisha wakajiunga na CCM kwa kupokelewa na Mwenyekiti wa chama hicho taifa, Rais Jakaya Kikwete, mjini Dodoma mapema mwaka huu.
Kisha wakaanza kuzunguka maeneo mbalimbali nchini wakiwa pamoja na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Tanzania Bara, Mwigulu Nchemba, ambapo wamekuwa wakisimama majukwaani na kwenye mitandao ya kijamii wakikiponda chama chao cha zamani pamoja na viongozi wake.
Katika siku za hivi karibuni, Mwampamba amekuwa akijiita kuwa ni msemaji wa UVCCM. Mchange yeye ingawa hajawahi kuonekana wala kutamka hadharani kuwa amehamia CCM, anajulikana kwa kuisema vibaya CHADEMA na viongozi wake, hasa mitandaoni.
Katika mkutano wa juzi wa Zitto na Dk. Kitila, Habib Mchange ndiye alikuwa anafanya uratibu wa masuala mbalimbali ukumbini ikiwemo wakati wa maswali na majibu kutoka kwa waandishi wa habari na wadau wengine waliohudhuria.
Mwampamba ambaye ni mwanachama wa CCM, yeye alikuwepo ukumbini ambapo alionekana akizunguka na kutimiza majukumu fulani fulani, kisha baadaye inadaiwa alipeleka mkanda wa video wa mkutano wote ili urushwe katika kituo cha televisheni cha Star tv.
Uwepo wa vijana hao, unamtia doa Zitto ambaye katika moja ya tuhuma zinazoelekezwa kwake ni pamoja na madai ya kutumiwa na CCM kuisaliti CHADEMA.
Katika moja ya tuhuma zake ambazo hata hivyo juzi alizipangua, Zitto anadaiwa kuandika barua kwa baadhi ya wagombea ubunge wa CHADEMA katika majimbo kadhaa, wajitoe ili kuiwezesha CCM ishinde bila kupingwa katika majimbo hayo.
Katika mkutano na wahariri na waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari, Zitto ambaye alikuwa Naibu Katibu Mkuu CHADEMA, ameapa kuwa hayuko tayari kuondoka ndani ya chama hicho na atakuwa mtu mwisho kuondoka kwa hiari.
Wakati Zitto akiapa kwamba hayuko tayari kuondoka CHADEMA, Dk. Mkumbo, ambaye amekuwa mshauri mkuu wa chama hicho maarufu nchini, amesema kuwa kile kinachoitwa uhaini ndani ya CHADEMA ni wasiwasi wa siasa za ushindani kwa watu wasiotaka mabadiliko.
Akieleza sababu za kutokujitoa CHADEMA, Zitto alisema zaidi ya nusu ya maisha yake yamekuwa CHADEMA kwani alijiunga nacho tangu alipokuwa na miaka 16 hadi sasa ana miaka 37 na amekabiliana na vitisho mbalimbali dhidi ya wasiotaka mageuzi kwa wakati ule.
Mbunge huyo ambaye amepata umaarufu mkubwa tangu alipoingia bungeni, alieleza kuumizwa na shutuma nyingi ambazo zimekuwa zikielekezwa kwake kwa muda mrefu.
Alisema amekuwa akiitwa msaliti, mnafiki, mla rushwa akihongwa kwa ajili ya kukisaliti chama.
Zitto ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Hesabu za Serikali (PAC), alisema akiwa mwanasiasa kijana na binadamu anaamini ana makosa kwa kuwa hakuna binadamu aliye mkamilifu na kwamba upungufu wake unapaswa kupimwa na mema aliyoyafanya.
Kwa upande wake Dk. Kitilla Mkumbo alikiri kuuandaa waraka huo kwa kushirikiana na Mwenyekiti wa Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba, ambaye naye kwa sasa amesimamishwa.
Alisema waraka huo uliandaliwa kwa siri bila kumshirikisha Zitto na kwamba hajui lolote kwani walipanga kumpelekea baada ya kukamilika na baada ya chama kutangaza tarehe ya uchaguzi.
Via: Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment