Blog ya kijanja kwa ajili ya watu wajanja

Blog ya kijanja kwa ajili ya watu wajanja

Saturday, November 2, 2013

JANGILI LAUA ASKARI MANYONI

WATU wawili, akiwemo askari polisi, wameuawa katika Kitongoji cha Kirumbi, Kijiji cha Kintanula, Kata ya Mwamagembe, mkoani Singida wakati wakirushiana risasi na kundi la majangili wanaodaiwa kujihusisha na vitendo vya biashara haramu ya nyara za serikali.
 
Tukio hilo lilitokea wakati askari huyo akirejea nyumbani wilayani Manyoni, usiku wa kuamkia Oktoba 31, akitokea katika Operesheni Tokomeza Ujangili inayoendelea wilayani Manyoni, mwaka huu.
 
Askari aliyeuawa ni mwenye namba G.9934 D/C Mgaka (26) huku mtuhumiwa wa ujangili akitambulika kwa jina la Selemani Kimpinde maarufu kwa jina la “Masta”, mkazi wa Kijiji cha Kipili, Kata ya Sikonge mkoani Tabora.
 
Inadaiwa kuwa baada ya askari wa kikosi maalumu cha Operesheni Tokomeza Ujangili kumkamata mtuhumiwa na pikipiki aliyokuwa akitumia katika matukio ya ujangili, aliwaomba kwenda kuwaonyesha mahali zilipo silaha wanazotumia kufanyia vitendo hivyo.
 
Mkuu wa wilaya hiyo, Fatma Taofiq, alithibitisha tukio hilo akisema baada ya askari huyo kumkamata mtuhumiwa walipanda gari na kuanza safari ya kwenda kuonyeshwa zilipo silaha aina ya SMG, lakini walipofika mita kama 100 kabla ya kufika kwenye eneo husika, askari hao waliamua kushuka kwenye gari na kuanza kutembea kwa miguu.
 
Alisema kuwa baada ya kufika kwenye eneo ambalo walitegemea kuonyeshwa silaha, alitokea jangili mmoja aliyekwenda kumpora askari silaha aliyokuwanayo.
 
Kwa mujibu wa mkuu huyo, wakati wa purukushani na jangili hilo lililomnyang’anya silaha askari, walijitokeza majangili wengine wawili na kumpiga risasi askari huyo.
 
Alisema baada ya askari huyo kuanguka chini akiugulia maumivu, ndipo jangili huyo alianza kutimua mbio mara tu baada ya tukio hilo.
 
Kwamba wakati likitimua mbio, askari wengine waliokuwa wamejificha, mmoja wao alimpiga risasi na kufa papo hapo.
 
Mkuu huyo wa wilaya aliwapongeza askari wanaofanya kazi hiyo kwa kile alichodai kuwa operesheni hiyo imefanikiwa kwa kiasi kikubwa sana na bado wanaendelea kuwasaka majangili waliokimbia mara baada ya kutenda tukio hilo.
 
Via: Tanzani Daima

No comments:

Post a Comment