WIKI moja tangu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru
Kawambwa, atangaze matokeo ya darasa la saba na kudai ufaulu umeongezeka,
baadhi ya walimu na wazazi wamefichua ‘madudu’ yaliyofanyika kupanga
washindi wakidai hatua hiyo itaongeza idadi ya wajinga nchini.
Waziri Kawambwa alisema kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi hao kwa
mwaka 2012 kimeongezeka kwa asilimia 8.8 ikilinganishwa na matokeo ya mwaka
2011.
Alisema kuwa alama ya juu ya ufaulu kwa wanafunzi wote ni 234 kati
ya alama 250 ambapo wasichana wamefaulu kwa wingi zaidi kuliko wavulana
kutoka kwenye idadi hiyo ya 865,827 waliofanya mtihani huo.
Hata hivyo, vyanzo vyetu vya taarifa kutoka kwa baadhi ya walimu na
wazazi wa wanafunzi hao, vilionyesha kuwa hawakubaliani na maelezo ya
Kawambwa ya kuongezeka kwa kiwango cha ufaulu wakati alama zilizotumika
kuwachagua washindi zilikuwa chini ya kiwango.
Katika takwimu zilizopatikana kwenye wilaya za Arusha (shule za
msingi Kioga na sekondari Ilkiding’a), Sengerema (shule za msingi
Buzilasoga, Tamabu Butonga na Buyangu), Bukombe (shule ya msingi Katente),
Shinyanga Vijijini, na Singida Mjini (shule za Mungumaji, Mfumbu, Kisasida
na Ipungi), kiwango cha ufauli kinatisha.
Akizungumzia matokeo hayo, Mwenyekiti wa Chama cha Walimu Mkoa wa
Geita (CWT), Dotto Biteko, alihoji ufaulu umeongezeka vipi wakati alama
zinazotumika kama vigezo zilishushwa ili kukidhi idadi badala ya kiwango?
Biteko alisema kuwa wanafunzi waliochaguliwa hawakufikisha alama 100
kati ya 250 kwa masomo yote matano yaliyofanywa na wengi wao wamechukuliwa
wakiwa na alama 70 au chini zaidi ya zile zinazohitajika.
Aliongeza kuwa kama waliokuwa wanachagua wanafunzi hao wangezingatia
alama 100 zinazohitajika, pamoja na kwamba bado ipo chini ya kiwango cha
utahini, shule nyingi za kata zingekuwa na wanafunzi wachache au kukosa
kabisa.
“Uteuzi wa wanafunzi ulifanyika kisiasa ili kuziba mapengo shule za
kata na kutowavunja moyo wazazi wa watoto,” alisisitiza.
Naye mwalimu Mkuu wa Shule ya msingi Kioga, Vincent Osinga Mollel,
alisema kuwa tatizo hilo ni la kweli kwani wanafunzi wamechukuliwa wakiwa
na alama 70 badala ya 100.
“Tunashindwa kuelewa vigezo vilivyotumika, hata hivyo kuna wanafunzi
wamepata alama 90 wameachwa huku walio na alama hata chini ya 70
wakichukuliwa suala ambalo limetuletea mgogoro na wazazi ambao tayari wana
mpango wa kuandamana kupinga matokeo hayo,” alisema.
Pia walimu wengine wa shule za sekondari katika wilaya za Sengerema,
Singida na Geita walisema wanasikitika kuwa wanafunzi waliochaguliwa bado
wapo ambao hawajui kusoma na kuandika.
Mwalimu wa Taaluma katika shule ya sekondari ya Buyangu wilayani Sengerema,
Enock Boniface, alisema ni hali ngumu kwao kwani baadhi ya wanafunzi
waliofika kuchukua fomu za kujiunga na shule hiyo hawajui kusoma na
kuandika hatua inayowapa shida.
“Tumepokea wanafunzi wenye sifa, yaani waliopata alama 100 kati ya
250 wapo 27, ila wale ambao wamefeli tumeletewa wanafunzi 49, lengo ni
kukidhi idadi ya wanafunzi darasani,” alisema.
Naye mwalimu mwingine ambaye hakupenda kutajwa jina, alisema kuwa
kuwa wakati wa uteuzi wa wanafunzi hao walifanya uchaguzi wa wanafunzi
katika ngazi za wilaya, lakini baadaye zoezi lilirudiwa kimkoa na
lilifanyika Ukerewe.
Mwalimu huyo ambaye alishiriki uteuzi, alisema kuwa walipomaliza
kuchagua wanafunzi wenye alama 100 walionekana wako pungufu na hivyo kuketi
tena kwa siku tatu, wakirudia upya uteuzi huo hadi kufikia hatua ya
kuchukua wale wenye alama 70.
“Tutakuwa tumewapatia walimu wa sekondari kazi sana, maana
tumechagua watu ambao wamefeli tukawapitisha kwenda sekondari,” alisema.
Baadhi ya walimu wengine walisema kuwa kuna waraka ambao wamepewa na
wizara katika kuwatungia mtihani wa kusoma, kuandika na kuhesabu, hata
hivyo walilalamika kwamba wale waliosema hawajui kusoma na kuandika mwaka
jana hawakuondolewa shuleni na sasa wataingia kidato cha pili.
Gazeti hili lilimtafuta Waziri Kawambwa kuzungumzia suala hilo
lakini akasema yuko katika kikao na hivyo kuomba apigiwe baada ya nusu saa,
ila alipopigiwa hakupokea na hata alipotumiwa ujumbe mfupi hakujibu.
Pia Naibu Waziri, Philipo Mulugo, naye alipokea simu na kuomba
aandikiwe ujumbe mfupi lakini hakuweza kuujibu.
Source: Tanzania Daima
|