SHIRIKA la mtandao wa vijana linalojishughulisha na uzuiaji wa vitendo vya
kikatili dhidi ya wanawake (Y2Y Movement), limeitaja mikoa ya Mara na Singida
kuwa bado inakabiliwa na janga kubwa la vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake,
ikiwa ni pamoja na biashara haramu ya kusafirisha binadamu.
Mbali na mikoa hiyo, mikoa mingine iliyotajwa kuendeleza vitendo hivyo vya
kinyama, ni pamoja na Mwanza na Shinyanga, ambapo imeelezwa kwamba zaidi ya nusu
ya wanawake na wasichana wamekuwa wakitendewa ukatili huo, huku asilimia 40 ya
kundi la vijana wa kuanzia miaka 10 hadi 24 bado wanaamini kuwa mwanamke anayo
haki ya kuteswa.
Akitoa mada katika semina ya kupambana na ukatili iliyofanyika jijini hapa,
Mkurugenzi wa shirika hilo, Hellen Mahindi, alisema vijana wa mikoa ya Mara,
Singida, Shinyanga na Mwanza wamekuwa wakijihusisha na ukiukwaji wa haki za
binadamu kwa kumnyanyasa mwanamke.
Mahindi alisema baadhi ya jamii ya Mkoa wa Singida wamekuwa wakijihusisha na
biashara haramu ya kusafirisha watoto wa umri mdogo kwenda mkoani Tabora kwa
ajili ya kuwatumikisha katika baadhi ya shughuli, ikiwa ni pamoja na kutega na
kufuga nyuki, kulima na kufanyishwa kazi ngumu za majumbani.
Aliitaka serikali kupitia vyombo vyake vya dola kufanya uchunguzi wa kina
katika suala hilo, kisha hatua kali zichukuliwe mara moja kwa watu wote
watakaobainika kuhusika na biashara hiyo haramu ya binadamu.
Alisema kuwa, lazima wanaharakati, mashirika na serikali washirikiane kwa
pamoja kudhibiti hali hiyo na kujenga taifa lenye mtazamo chanya wa
kimaendeleo.
“Asilimia 40 ya kundi la vijana bado wanaamini haki ya kunyanyaswa mwanamke.
Hivi ni vitendo vibaya na tunatakiwa sote kwa pamoja tuunganishe nguvu
kutokomeza kabisa ukatili wa namna hii, maana binadamu wote ni sawa,”
alisema.
Mahindi alisema kuwa wamelenga kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2015 asilimia
kubwa ya vijana nchini watakuwa wameelimika na kuachana kabisa na unyanyasaji
huu wa kijinsia.
Chanzo: Tanzania Daima Jumapili 04 Nov. 2012
No comments:
Post a Comment