Mwanachama mzuri wa chama chochote cha siasa ni yule anayeendelea kuwa mwanachama hata pale kiongozi anayempenda, kumuamini sana anapofanya kosa na kuvuliwa cheo au kufukuzwa.
Ni vizuri kuwa muumini wa dini kuliko kuwa muumini wa kiongozi wa dini. Ni vizuri pia kuwa muumini wa
taasisi (chama) kuliko kuwa wa kiongozi wa taasisi.
Baadhi ya viongozi na wanachama wa CHADEMA wameonyesha kuwa waumini wa viongozi badala ya chama, hawa hawana mapenzi mema na chama ambacho hivi sasa kimekuwa kimbilio la watu waliochoshwa na minyororo ya CCM.
Baada ya aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu, Zitto Kabwe, mjumbe wa Kamati Kuu, Dk. Kitila Mkumbo na Mwenyekiti wa Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba kuvuliwa uongozi kwa madai ya kukisaliti chama, wafuasi wao sasa wameanza kuondoka.
Kuondoka ndani ya chama kwa sababu ya kiongozi fulani kavuliwa cheo au kafukuzwa ndani ya chama kunaonyesha baadhi ya watu wanavyojiunga ndani ya vyama bila kusoma kwa undani sera, katiba, kanuni na matakwa ya chama.
Chama chochote makini hakiwezi kuwaacha viongozi au wanachama wake wanaobainika kwenda kinyume na katiba, sera na kanuni za chama. Mgawanyiko ndani ya chama ni hatari.
Inawezekana watu wanaishi kwa hofu ya kuwaondoa viongozi wa ngazi za juu, kama hivi ndivyo, basi siasa hasa za upinzani kamwe haziwezi kukua.
Zitto na wenzake walivuliwa nyadhifa zao baada ya kuonekana hawana mwenendo mzuri wa kujenga chama, hawa walionekana na nyendo za kukigawa chama, kwa kitendo chao cha kuwa na “mikakati ya mabadiliko ndani ya CHADEMA”, mikakati ya kutaka kupata uongozi wa juu wa chama hicho kwa kile walichokiita “udhaifu wa mwenyekiti”.
Najua uamuzi wowote unapotolewa haukosi uungwaji mkono au upingwaji, jambo la muhimu kuzingatiwa ni kufanya tafakuri ya kina ya kile kilichofanyika. Je, kina maslahi kwa chama?
Masilahi ya chama ni muhimu zaidi kuliko umaarufu wa kiongozi fulani. Wenye kuhama chama kwa sababu ya kiongozi kuvuliwa cheo au kufukuzwa hapaswi kunyenyekewa wala kubembelezwa.
Kwa maoni yangu wale wanaomuunga mkono Zitto kuwa ameonewa, hawana mapenzi na CHADEMA, bali wana mapenzi na kada huyo kitu ambacho si sahihi, si kitaasisi tu bali pia hata kidini.
Huwezi kuwa na mapenzi ya kupindukia kwa anayeongoza taasisi na kuacha kuwa na mapenzi na taasisi anayoiongoza.
Mapenzi kwa kiongozi si tu kwa CHADEMA, hata kwa vyama vingine vya siasa kama vile CCM, NCCR-Mageuzi, TLP, CUF.
Ni udunishaji wa siasa, ikitokea Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Mwigulu Nchemba na wafuasi wake wanaweka mikakati ya kumtoa mwenyekiti wao Jakaya Kikwete, lakini hawavuliwi uongozi kwa sababu ya umaarufu wao.
Kuwavumilia watu wanaokwenda kinyume na sera, katiba na utaratibu wa chama ni kukibomoa. Uimara wa chama hujidhihirisha kwa kuchukua hatua ngumu zenye lengo la kukiimarisha bila kujali umaarufu wa mtu au lawama kutoka kwa watu wenye mahaba na aliyechukuliwa hatua.
Naamini kuwa si wanachama wote wa CHADEMA ni wajumbe wa Kamati Kuu, lakini pia si wajumbe wote waliokubali Zitto na wenzake wavuliwe vyeo. Wajumbe wengi walijiridhisha kwamba kilichokuwa kikifanywa na makada wenzao kina dhamira ya kukigawa na kukidhoofisha chama.
Wajumbe wa Kamati Kuu wanajua umoja na mshikamano ndani ya chama ni muhimu zaidi kuliko jambo lolote, ndiyo maana wakaamua kuwavua madaraka Zitto na wenzake.
Zitto mara kwa mara amekuwa akisisitiza watu kufuata misingi ya chama, na si watu ndani ya chama, hili
nadhani hivi sasa ndilo jukumu kubwa analopaswa kulifanya hivi sasa
Na. Antony Gella, Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment