Blog ya kijanja kwa ajili ya watu wajanja

Blog ya kijanja kwa ajili ya watu wajanja

Monday, December 23, 2013

UASI WAANDALIWA KUIVURUGA CHADEMA, YENYEWE YABAINI MKAKATI HUO, SASA KUCHUKUA MAAMUZI MAGUMU ZAIDI

Dk Willibrod SlaaKATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa amesema kuwa chama hicho kimenasa mkakati mzito uliolenga kuwarubuni viongozi wa wilaya wa chama hicho wafanye uasi bila kujua.
 
Alisema kuwa mkakati huo umetolewa na watu aliowaita matapeli wa kisiasa, ambao wanasambaza barua katika maeneo kadhaa wakisema kuwa imetoka Makao Makuu ya CHADEMA ikiambatanishwa na fomu ambayo wanaambiwa wasaini kuonyesha wanataka kufanyika kwa kikao cha dharura cha Baraza Kuu la chama hicho.
 
Akizungumza katika mkutano wa hadhara mjini Nzega juzi, pia katika Kijiji cha Nanga na mjini Igunga jana, Dk. Slaa alisema kuwa hila za watu hao wanaolenga kuwarubuni viongozi wa chini wa chama hicho ili waonekane wanapinga uamuzi wa Kamati Kuu iliyochukua hatua za kinidhamu dhidi ya mbunge Zitto Kabwe na wenzake, zimebainika baada ya kushtukia ulaghai huo.
 
“Nataka kutoa ufafanuzi wa suala hili la kitaifa kupitia mikutano hii ili niwajulishe viongozi na wanachama wote kwa pamoja badala ya kumjibu mtu mmoja mmoja, kwamba tumenasa mkakati huo unaoandaliwa na watu wanaotaka CHADEMA isiwepo.
 
“Wamepeleka barua kwa baadhi ya viongozi wetu mathalani mikoa ya Lindi na Mtwara, ambayo imeambatanishwa na fomu ambazo hazijaandikwa kitu chochote pale juu, lakini wanaambiwa wasaini. Tumegundua nia yao ni kufanya kitu kinaitwa ‘petition’ dhidi ya maamuzi ya chama. Tunasema huo ni uasi.
 
“Na kuonyesha kuwa suala hilo halina nia njema na kwamba wanajua halikubaliki na wao wenyewe hawakubaliki kwa sababu ya hila zao dhidi ya chama, wamesingizia kuwa barua hiyo pamoja na fomu zimetoka Makao Makuu ya CHADEMA.
 
“Wamesambaza watu, wamepeleka na hela, wamelipa watu hela nyingi kwa kazi hiyo. Najiuliza hizo hela zimetoka wapi, ni za kazi gani, kwa ajili ya manufaa ya nani? Napenda kutoa kauli, Makao Makuu wala Ofisi ya Katibu Mkuu wa CHADEMA haijatuma barua wala fomu ya namna hiyo wala haijatuma watu wa namna hiyo,” alisema Dk. Slaa.
 
Aliwashukuru viongozi wa wilaya ambao wameshafuatwa na wanaosambaza hila hiyo kwa kumtaarifu na kumpatia taarifa nzima ya namna mpango ulivyosukwa kutaka kuwanunua kwa fedha nyingi.
 
Wakati kiongozi huyo akisema hayo, gazeti hili limepata taarifa kutoka vyanzo mbalimbali vya habari kuwa mkakati huo umeandaliwa mahsusi kwa ajili ya kuanza kuwarubuni wajumbe wa kikao cha Baraza Kuu la chama hicho ambacho huenda kikaitishwa kujadili suala la akina Zitto, Dk. Kitila Mkumbo na Samson Mwigamba ambao hivi karibuni walivuliwa nafasi zao za uongozi ndani ya chama na Kamati Kuu kwa makosa ya kinidhamu.
 
Taarifa hizo zimedai kuwa suala la makada hao baada ya kujadiliwa tena katika kikao cha Kamati Kuu ambacho hakijajulikana kitakaa lini ili kusikiliza utetezi wa mashtaka 11 waliyoandikiwa na kutakiwa kujibu, linaweza kufikishwa pia mbele ya kikao cha Baraza Kuu baada ya Zitto kukata rufaa kwenye chombo hicho.
 
Baadhi ya watoa taarifa wetu wamedokeza kuwa kuna mikakati ya kuwarubuni wajumbe wa kikao hicho ili waonekane wako kinyume na uamuzi wa Kamati Kuu, ambapo waraka unaosambazwa katika baadhi ya maeneo, umeambatanishwa na fomu ambazo hazijaandikwa kitu kuonesha zinahusu nini, ili baadaye saini zao zitumike (bila wao kujua) kuonyesha kuwa wanataka kuitishwa kikao cha dharura cha Baraza Kuu.
 
Mashabiki watamponza Zitto
Akijibu maswali ya papo kwa hapo kutoka kwa wananchi waliohudhuria mkutano wa Nzega mjini, Dk. Slaa aliwaambia wanachama wa chama hicho na Watanzania kwa ujumla kujifunza kusimamia masuala ya msingi katika uendeshaji wa taasisi kama chama cha siasa badala ya kufuata ushabiki.
 
Akizungumzia tatizo linalowahusu Dk. Mkumbo, Zitto na Mwigamba, alisema sio jambo la mzaha bali linahusu misingi ya chama hicho ambacho alisema kinajivunia uthubutu wa kufanya uamuzi sahihi na muhimu hasa katika kusimamia maadili na uadilifu ndani ya chama.
 
“Watu wengine, najua ni wachache, lakini wapo wanaofanya ushabiki katika suala hili, nawashauri badala ya watu hao kufanya ushabiki katika suala hili, wamshauri…kufanya ushabiki kunaweza kumponza. Sitaki kusema zaidi kwa sababu bado ni suala la vikao vya ndani.
 
“Wasifanye ushabiki katika masuala haya yanayohusu nidhamu. Ni lazima Watanzania waanze kuzoea kuwa bado kuna taasisi zinaweza kusimamia misingi yake ambayo watu mahali fulani wamekubaliana kuwa ndiyo inawaunganisha na kuwaweka pamoja,” alisema Dk. Slaa.
 
Ukiukwaji haki za binadamu
Wakati huo huo, Dk. Slaa alishindwa kujizuia kudondosha machozi baada ya kupewa taarifa za matukio mawili, yote yakihusisha ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu unaofanywa na vyombo vya dola kwa usimamizi wa baadhi ya watendaji wa serikali.
 
Akizungumza na wananchi wa Kata ya Lusu, katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Ngw’aluzwilo juzi asubuhi, Dk. Slaa alipewa malalamiko ya wakazi wa maeneo hayo wakiwemo wachimbaji wadogo namna ambavyo hawajanufaika na uliokuwa mgodi wa dhahabu uliokuwa ukimilikiwa na Kampuni ya Resolute Nzega.
 
Alishindwa kujizuia kutoa machozi, pale aliposimuliwa na kuonyeshwa majeraha ya mateso aliyopata mmoja wa vijana ambaye familia yake iligundua dhahabu katika shamba lao pembeni mwa eneo la mgodi, lakini viongozi wakuu wa serikali kutoka wilayani wameamua ‘kuliteka’ na kutumia askari polisi kuwashushia kipigo raia wanaofika hapo na kuwataka waondoke mara moja.
 
Akizungumzia suala hilo akiwa mjini Nzega, Dk. Slaa alisema kwa mambo yanayowatokea wananchi walioko karibu na rasilimali za nchi hii kama madini, yanatia huruma na kama serikali haiwezi kuchukua hatua kuwa upande wa wananchi wake, haitaweza kusafishika kwa mawaziri kujiuzulu.
 
Aliwaambia wananchi walioko karibu na uliokuwa mgodi wa Resolute kuwa chama hicho kitasimama kidete kuwatetea kwa sababu kimepata taarifa kuwa waliokuwa wawekezaji katika eneo hilo wanataka kumwaga maji kwenye mashimo ya machimbo hayo, hali ambayo itasababisha madhara makubwa kwa binadamu kutokana na kemikali kusambaa.
 
Akiwa katika Kijiji cha Nanga jana, Dk. Slaa pia alishindwa kujizuia kudondosha machozi baada ya wabunge wake wawili, Conchesta Rwamlaza na Dk. Gervas Mbasa kuelezea kwa kina na mifano hai, juu ya ripoti ya Operesheni Tokomeza Ujangili wakionyesha namna ambavyo wananchi wasiokuwa na hatia wamefanyiwa unyama wa kutisha.
 
Via: Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment