Na. Furaha Venance
Katika gazeti hili toleo Na.326 la novemba 20-26, 2013, kuna makala iliyoandikwa na Bwana Mrisho Gambo ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Korogwe yenye kichwa cha habari, “Sababu 11 za walimu kuichukia serikali.” Kiufupi kabla nami sijaingia katika mjadala huu, ni vema kwanza, nikaweka msimamo wangu kuhusu sababu zilizotolewa na Mrisho Gambo, nakubaliana na baadhi ya sababu alizotoa ambazo kiukweli zinachangia walimu wengi kuichukia Serikali, lakini baadhi sababu zake sikubaliani naye, na nitaeleza mbele ya safari kwa nini sikubaliani naye.
Labda niwakumbushe wasomaji wa makala hii, kama hawakuiosoma makala ya Gambo, kutaja baadhi ya sababu hizo 11 (lakini moja hakuisema) alizozitaja kama ndiyo sababu ya walimu kuichukia Serikali ili tuwe pamoja, sababu hizo ni:
- Kuwapandisha walimu madaraja
- malimbikizo ya madeni ya mishahara ya walimu
- kukosekana kwa motisha kwa walimu wa Sayansi
- Aina ya wanafunzi wa kidato cha kwanza
- Mafunzo kwa walimu
- Nyumba za walimu
- Walimu kusimamia mitihani
- walimu kulipia vitambulisho vya kazi
- Walimu kulipia ujazaji wa fomu za OPRAS
- Uhaba wa vitendea kazi
Katika sababu hizo, ni hoja mbili tu, yaani ya kwanza na ya pili lakini ni kwa kiasi kidogo kwa walimu wasiowaelewa huweza kuichukia Serikali, ni ukweli usiopingika kuwa, kama walimu wanafanya kazi kwa muda mrefu bila kupandishwa madaraja, huweza kusababisha walimu kuichukia Serikali yao, lakini hoja hii haina nguvu sana kwa sababu suala la upandishaji wa madaraja liko ngazi ya Wilaya, yaani Afisa Elimu, Mkurugenzi na TSD ndiyo kwa kiasi kikubwa wanahusika na upandishaji wa madaraja hayo, hivyo walimu wengi wanaoelewa utaratibu huu, huwa hawaichukii Serikali yao, bali chuki yao huionesha kwa watu hao niliowataja, na hapa utawasikia walimu wengi wakisema kuwa, Afisa elimu ‘amenibania’.
Katika sababu nyingine, kuwa malimbikizo ya madeni ya mishahara, kuwa ni sababu ya walimu kuichukia Serikali ni kweli, hapa nakubaliana naye, na hapa serikali imeshindwa kuwashughulikia Maofisa Watumishi wazembe ambao kwa kiasi kikubwa ndiyo wanaosababisha Serikali kila mara kuwa na madeni ya walimu, kwa mfano kuwahamisha walimu wakati pesa hakuna, kuwapandisha walimu madaraja na wakati huo huo kuzembea kuwasilisha mabadiliko hayo kwenye ngazi husika ili mwezi anaotakiwa mwalimu kulipwa mshahara mpya alipwe kwa wakati huo, matokeo yake utakuta miezi, miaka inakatika bila mwalimu huyo kulipwa mshahara mpya na hapo ni wazi kuwa serikali itakuwa na madeni na madeni yakiwa mengi Serikali itashindwa kuwalipa walimu wote kwa wakati na hapo ndipo chuki huanza dhidi ya serikali.
Lakini hoja zingine zote alizozitoa Gambo, kusema kweli, haziwezi kuwa hoja za msingi hadi kuzipa jina, sababu 11 za walimu kuichukia Serikali, sababu zifuatazo hazina ukweli wala uthibitisho wa kisayansi kuwa walimu wanaweza kujenga chuki na serikali yao,
Eti kukosekana kwa motisha kwa walimu wa Sayansi, ni sababu ya walimu kuichukia serikali! Hii si kweli kabisa, kwanza ieleweke wakati mtu anaenda kusomea Taaluma ya Ualimu iwe kwa masomo ya Sayansi au yale ya sanaa, wala hakujua wala kutegemea kuwa huwa kuna posho ya walimu wa sayansi, hivyo kukosekana kwa posho ya aina hii hakuwezi kuwa sababu ya walimu kuichukia Serikali, isipokuwa tu, walimu wanaiomba serikali yao kuwafikiria hilo, yaani kuwa na aina hiyo ya posho. Cha muhimu hapa ni kuboresha tu mshahara wa mwalimu tena walimu wote, haya mambo ya posho sijui za nini yatajifia tu yenyewe.
Sababu nyingine ya Aina ya wanafunzi wa kidato cha kwanza, hapa akiwa na maana wale wale wanaoanza kidato cha kwanza huku wakiwa hajui kusoma na kuandika kuwa ni sababu nyingine ya walimu kuichukia Serikali nayo haina mashiko kabisa, kwanini? Kwanza ukitumia sababu hii maana yake kuwa walimu wa shule za msingi na zile shile za “A-Level” wenyewe katika sababu hii hawahusika sababu hawana tatizo hili la kupokea wanafunzi wasiojua kusoma na kuandika. Na tatizo hilo si kwamba ni Serikali inaamua kuwapeleka hao watoto wasiojua kusoma na kuandika, huu ni ujanja ujanja unaofanywa na baadhi ya walimu wakuu wa shule za msingi kuwasaidia watoto hao kufaulu mitihani yao, tena kwa kuwatumia wanafunzi wengi kuwaandikia watoto hao huku wakuu hao wakiwa wamechukua chochote kutoka kwa wazazi au kutaka sifa tu za kufaulisha shule zao, na tatizo hili walimu wengi wa sekondari wanalifahamu vizuri sana hivyo hii haiwezi kuwa sababu ya walimu kuichukia serikali hata kidogo.
Mafunzo kwa walimu, pia imetajwa na mwandishi wa makala hiyo kuwa ni sababu ya walimu kuichukia Serikali, hakuna Mwalimu anayeichukia serikali eti kwa sababu ya aina ya mafunzo aliyoyapata huko chuoni, kumbuka suala kuna vyuo vya serikali na vyuo binafsi, hivi ni kweli mwalimu anaweza kuichukia serikali kwa sababu tu ya mafunzo anayoyapata katika chuo hicho kama yanafaa au hayafai, hivi mwalimu huyo anaweza kweli kuichukia serikali badala ya kukichukia chuo alichosoma!
Nyumba za walimu pia imetajwa na mwandishi wa makala hiyo kuwa nayo ni sababu ya walimu kuichukia Serikali, mwalimu hawezi kuichukia serikali eti kwa sababu tu hakuna nyumba ya shule sehemu anayofanyia kazi, hivi ni watumishi wote wa serikali wanakaa kwenye nyumba za serikali! Hapa muhimu ni serikali kuboresha mshahara wa mwalimu ili hata kama atakosa nyumba ya serikali, basi amudu kupanga nyumba na wakati huo huo kuweza kumudu mahitaji yake mengine.
Pia ametaja sababu ya walimu kutosimamia mitihani, eti ni sababu ya walimu kuichukia serikali, hili nayo si sababu hasa ya walimu kuichukia serikali, ieleweke kuwa, si kila mwalimu anaweza kuwa msimamizi wa mitihani ya Taifa, hii inaenda sambamba na usahishaji wa mitihani hiyo, hapa kinachoangiliwa ni uadilifu wa mwalimu kazini, nidhamu yake, utunzaji wa siri na kuaminika kwake na mamlaka husika kuanzia mkuu wa wake wa kituo anayependekeza majina, na afisa elimu pia.
Hapa mwalimu hawezi ‘kuinunia’ serikali eti kwa sababu tangu aanze kazi hajawahi kusimamia mtihani, nah ii ni kwa sababu majina hupendekezwa na wakuu wa shule, ambao anadhani wanasifa, anaweza akapendekeza majina, afisa elimu akawachukua au asiwachukue kabisa kwa sababu anazozifahamu yeye, na hapa walimu huonesha chuki zao kwa wakuu wao yaani walimu wakuu katika vituo vyao au Maafisa Elimu wakiamini kuwa ‘wamewabania’ na wala si Serikali kama mwandishi wa makala hiyo anavyotaka kutuaminisha.
Sababu nyingine zilizotajwa ambazo naziweka pamoja ni, Walimu kulipia vitambulisho vya kazi na kulipia ujazaji wa fomu za OPRAS, sababu hizi nazo hazina mashiko kabisa, kuonesha kuwa chuki ya walimu kwa serikali kunasabishwa na kulipia vitambulisho na hizo fomu ambazo kwa zote jumla haziwezi kuzidi hata Tsh. 5000/= na kama kuna sehemu wanakotoza hizo gharama ni wizi, na wizi huu haufanywi na Serikali bali watumishi wasiokuwa waaminifu, na walimu wanalijua hili, hivyo walimu hawawezi kuichukia Serikali yao kwa sabubu hizi.
Napenda kuhitimisha kwa kusema, ukiangalia katika makala ya Gambo, ameacha jambo la msingi ambalo kwa kiasi kikubwa ndilo linalobeba asilimia kubwa ya walimu kuichukia serikali, na sababu hiyo ni Mishahara duni ya walimu, na hata ukiziangalia hoja za Gumbo zinajitokeza kwa ajili ya masalihi kuwa duni. Walimu kufikiria au kuwa na dhana kuwa, Serikali inawachukulia walimu kama watumishi wa kada ya chini kabisa kaliko kada zote serikalini. Walimu wanaona kama serikali haiwathamini kimaslahi, hoja za kulipia vitambulisho, fumu za OPRAS, kusimamia mitihani, n.k. ni hoja zinazoweza kuwafanya watu waone kuwa walimu ni watu wa njaa njaa tu ndo maana wanalilia hadi kusimamia mitihani jambo ambalo halina ukweli wowote ule.
Na ushauri wangu kwa Gambo na wakuu wengine wa Wilaya nchini, akitumia cheo chake cha Ukuu wa Wilaya kuwachukulia hatua hao wanaosababisha walimu kuwa na chuki kwa serikali yao, maana walimu wakiwa na chuki na serikali ni rahisi sana kupandikiza chuki hizo hata kwa wanafunzi wanaowafundisha na wakajaa chuki na serikali yao jambo ambalo si sahihi hata kidogo.
Mwandishi wa makala hii, Furaha Venance, ni Mwalimu katika Shule ya Sekondari Mwanzi iliyopo wilayani Manyoni, Mkoani Singida na msomaji wa gazeti hili Anapatikana kwa simu: 0787 33 55 53, O715 33 55 58. barua pepe: venancefuraha@gmail.com [Makala hii imechapwa katika gazeti la Raia Tanzania, Gazeti jipya la Raia Mwema]
Makala hii imetokana na makala ya Mrisho Gambo hii hapa
Sababu 11 za walimu kuichukia Serikali
LEO nimeona nami nianze kuweka mawazo yangu kwenye maandishi. Japokuwa kwa sasa ni kiongozi wa serikali, naamini nafasi hiyo haininyimi fursa ya kutoa mchango wangu wa mawazo kwa mustakabali wa taifa langu.
Nimekuwa nakiandika kwenye mitandao ya kijamii kama facebook pamoja na kutoa hotuba mbalimbali kwa watumishi na wananchi wilayani Korogwe. Nimeona niandike baadhi tu ya changamoto zinazowakabili walimu kwa kuwa nimekuwa nikijiuliza sana; mbona serikali inafanya mambo mengi kwa walimu lakini bado kuna baadhi ya walimu wanaichukia serikali yao?
Ninaandika masuala ambayo naamini yangefanyiwa kazi walimu wasingekuwa na manung’uniko makubwa. Sitazungumzia lile la kutaka kupandishwa mshahara kwa asilimia 100 ambalo kwa sasa naamini halitekelezeki.
Baada ya kutafakari yote hayo nimeona niandike uchambuzi ambao kwa kiasi kikubwa utazungumzia changamoto za kiutumishi za walimu wetu.
Kuwapandisha walimu madaraja
Hii ni changamoto inayowakabili walimu wetu Tanzania nzima. Wakati mwingine inasababishwa na ufinyu wa bajeti ya serikali pamoja na uzembe wa baadhi ya watendaji serikalini. Serikali mara nyingi imekuwa ikitoa maelekezo ngazi za halmashauri lakini mara nyingi yamekuwa hayafanyiwi kazi kwa uzito unaostahili.
Katika kipengele hiki nitatoa mfano hai, nina ushahidi wa uzembe uliofanywa na Halimashauri ya Mji Korogwe kwenye bajeti ya mwaka 2012/2013. Walisahau kuwapandisha madaraja walimu zaidi ya 30 wa sekondari walioajiriwa mwaka 2009.
Walimu hao walitakiwa kupanda daraja kwenye bajeti ya mwaka 2012/2013, lakini wakasahaulika kwa uzembe pamoja na serikali kutoa muongozo kuwa watumishi wote wanaostahili kupanda daraja wapande wote.
Lakini wao wakawaweka kwenye bajeti ya 2013/2014 badala ya 2012/2013, nini tafsiri yake? Walimu hawa wataachwa nyuma kwa mwaka mmoja kimaslahi na walimu wenzao walioanza kazi pamoja, ikiwa ni pamoja na kutolipwa malimbikizo yao kwa sababu serikali ilikwishatoa muongozo kuwa wote wawekwe kwenye bajeti.
Kitendo kama hiki cha uzembe wa watu wachache (mkurugenzi na wenzake) kinawafanya walimu kuichukia serikali yao. Pia kuna malalamiko ya walimu kushushwa madaraja bila hatia yoyote pamoja na wengine waliokuja baada ya wao kuajiriwa, kupanda daraja na wa zamani kubaki pale pale.
Hii ni changamoto kubwa na jambo hili ni kilio cha walimu wilayani Korogwe hadi leo. Halimashauri ya Korogwe Vijijini hawana tatizo hili japokuwa wao wana eneo kubwa la utawala (Kilomita za mraba 3574 wakati za halmashauri ya mji ni kilomita za mraba 212), wao walifanikiwa kuwapandisha daraja walimu wote walioajiriwa mwaka 2009. Hili linawafanya walimu waichukie serikali yao.
Malimbikizo ya madeni ya mshahara kwa walimu
Suala hili linahitaji kubadili mazoea katika utendaji. Kwa mtazamo wangu serikali kuu na serikali za mtaa zote ni serikali za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Lazima halmashauri zetu zibadilike na kubeba jukumu hili la malimbikizo ya madeni ya walimu ya mishahara na si kukusanya tu na kupeleka serikali kuu.
Sasa umefika wakati watenge pesa kutokana na mapato ya ndani ya halmashauri kwa ajili ya kumaliza madeni ya walimu.
Nimekuwa nikitoa mfano kuwa kama wameajiriwa walimu 30 wa sekondari kwa ngazi ya shahada ambao mshahara wao ni 532,000 kwa mwezi kwa kila mmoja kwa walimu wa shahada, jumla yake hapa ni shilingi 15,960,000.
Unakuta halmashauri wanalipeleka deni hilo serikali kuu na inachukua zaidi ya miaka mitatu bila kulipwa, kumbe halmashauri wangeweza kulipa kupitia mapato ya ndani na kama serikali kuu italeta, halmashauri itawataka walimu walipe pole pole kwa kuwakata kwenye mishahara yao.
Hii ni muhimu kwa kuwa utakuta mwalimu katoka Kigoma na kupangiwa kazi Korogwe ambako hana ndugu na hakuna nyumba ya serikali ya kufikia. Mwalimu huyu na wenzie utakuwa umewaharibu kisaikolojia na wataiona serikali yote haina maana kwa sababu ya shilingi 15,960,000. Jambo hili lina wafanya walimu waichukie serikali yao.
Kukosekana motisha kwa walimu wa sayansi
Kwanza naunga mkono agizo la Rais Jakaya Kikwete, pamoja na jitihada za serikali na wananchi kujenga maabara kwa kila sekondari ya kata nchini. Wilayani Korogwe tunaendelea kwa kasi na mchakato huu.
Jitihada hizi zitatuondolea changamoto ya upungufu wa walimu wa sayansi mbele ya safari. Kwa sasa tunatakiwa kuwapa motisha walimu wa sayansi kutokana na uchache wao unaosababisha kupangiwa vipindi vingi kuliko wenzao wa masomo ya sanaa.
Mfano, kwa wiki mwalimu wa sanaa anakuwa na vipindi vinne hadi saba, wakati mwalimu wa sayansi anakuwa na vipindi kati ya 22 hadi 30 bila motisha yoyote. Mwalimu huyu lazima akate tamaa na ajione kama ananyonywa na serikali yake.
Jambo hili pia linawafanya walimu wa sayansi waichukie serikali yao. Lazima tutafakari namna ya kuwapa motisha walimu wetu wa masomo ya sayansi. Ni dhahiri, jambo hili linawafanya walimu wa sayansi waichukie serikali yao.
Aina ya wanafunzi wa kidato cha kwanza
Tunapeleka wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi waliopata alama 70 chini ya 250 ambayo ni sawa na asilimia 28 ambayo ni alama D.
Mwaka huu kwenye Mock wamesema angalau alama 100 chini ya 250 ambayo ni sawa na asilimia 40 na yenyewe kwangu pia ni D, kwa sababu nimezoea kuwa C inaanzia asilimia 41. Humu humu inasemekana wamo wasiojua kusoma na kuandika, maana hata hesabu zenyewe ni za kuchagua, inakutosha kuambia eti umefaulu.
Kwa mwanafunzi huyu pia mwalimu anawekewa Big Result Now (BRN). Kama anaingia kidato cha kwanza amefeli maana kapata D, tunatarajia nini kidato cha nne? Sisi tuliosoma teknolojia ya kompyuta tunasema kinachoingia ndicho kinachotoka.
Tunahitaji kupitia upya utaratibu wetu wa kuwapata wanafunzi wetu wa kidato cha kwanza. Lazima wizara iweke mikakati madhubuti kwenye jambo hili, ili kumsaidia Rais wetu aache alama ya kukumbukwa na Watanzania kwenye dhana ya BRN.
Mafunzo kwa walimu
Mafunzo kwa walimu ni muhimu sana. Kwenye vyuo vya ualimu walimu hufundishwa mbinu za kufundishia, ambazo kwa mazingira ya sasa zinahitaji kuboreshwa zaidi.
Ni vema serikali ikaliangalia vema jambo hili ili walimu wetu waendane na mahitaji ya elimu yetu ya sasa.
Nyumba za walimu
Nyumba za walimu ni muhimu sana. Kuna maeneo mengine hata nyumba za kupangisha walimu hakuna kutokana na mazingira yenyewe. Lazima halmashauri itambue maeneo kama haya wakati wa kutekeleza jambo hili.
Kwenye bajeti ya mwaka huu kila halimashauri itapewa shilingi milion 500 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za walimu. Fedha hizi lazima zisimamiwe vizuri na tuachane na mambo ya wakandarasi ili tupate nyumba nyingi zaidi jambo ambalo limechangia halmashauri zetu kuwa mchwa na shamba la bibi.
Walimu kusimamia mitihani
Kulikuwa na utaratibu uliozoeleka kwa kikundi fulani cha walimu tu ndio waliokuwa wakisimamia mitihani. Kipindi fulani niliwahi kuuliza hivi kuna walimu waliosomea somo la kusimamia mitihani kiasi ambacho wengine wanakosa sifa hiyo?
Kama vigezo ni kuwa kazini miaka mitatu na kuwa na TSD namba pamoja ma vigezo vingine, sasa kwa nini kila mwaka wajirudie hao hao? Jambo hili linafanya walimu waichukie serikali yao.
Walimu kulipia vitambulisho vya kazi
Kumekuwa na utaratibu wa kuwalipisha walimu shilingi 2,000 kwa ajili ya vitambulisho, kitambulisho ni mali ya mwajiri ambaye ni serikali. Kuwalipisha walimu ni kinyume cha utaratibu. Halimashauri zimekuwa zikiwachangisha walimu wetu.
Nauliza, mbona vitambulisho vya taifa ni gharama zaidi lakini serikali inatoa bure? Jambo hili linawafanya walimu waichukie serikali yao.
Walimu kulipia ujazaji wa fomu za OPRAS
Kumekuwa na utaratibu wa baadhi ya halmashauri nchini kuwataka walimu walipie gharama za photocopy za fomu za Opras. Fomu hizi ni mali ya serikali kwa ajili ya kupima utendaji kazi wa watumishi. Kumlipisha mwalimu kwa ajili ya fomu hizi ni kinyume cha utaratibu. Jambo hili linawafanya walimu waichukie serikali yao.
Uhaba wa vitendea kazi
Hapa serikali inastahili pongezi maana imefanya kazi kubwa kwa upande wa vitabu. Jitihada zinatakiwa ziongezeke kwenye upande wa ofisi za walimu na maeneo mengine.
Nimegundua mambo kama haya ambayo yapo ndani ya uwezo wa serikali yanachangia kuongeza chuki kwa walimu dhidi ya serikali yao. Umefika wakati sasa wa kuwachukulia hatua za makusudi watumishi wote wanaoikwamisha serikali na watumishi wenzao, kwa sababu kila mwaka changamoto zimekuwa ni zilezile.
Sasa kwenye elimu tunazungumzia (Big Results Now- BRN - (Matokeo makubwa sasa), lakini kwa kweli bila kuangalia maslahi ya walimu itakuwa ni sawa na kutwanga maji kwenye kinu.
BRN kwenye elimu ni zaidi ya mjadala wa daraja sifuri (division 0) na daraja la tano (division 5) kwenye jamii yetu. BRN naikubali kwa asilimia 100, baadhi ya watendaji wa serikali tusikubali kuipotosha dhana hii nzuri kwa wananchi na kudhoofisha juhudi za serikali yetu, badala yake tujielekeze kwenye matatizo ya msingi ya walimu wetu.
Mwandishi wa makala hii, Mrisho Gambo ni Mkuu wa Wilaya Korogwe, mkoani Tanga na msomaji wa gazeti hili. Anapatikana kwa simu: +255766757575. barupepe; mrishogambo@gmail.com
No comments:
Post a Comment