WAKAZI 1,904 wa Kata ya Saranda, Tarafa ya Kilimatinde, wilayani Manyoni wanakabiliwa na upungufu wa chakula.
Diwani wa Kata ya Saranda, Juma Ramadhani aliyasema hayo alipokuwa akielezea hali ya chakula katika kata hiyo katika kipindi ambacho wananchi wanaendelea na shughuli za kilimo hadi wakati wa mavuno ya msimu ujao wa kilimo.
Alisema mazao ya chakula katika vijiji vya kata ya Saranda si nzuri kulingana na msimu wa 2012/2013 kuwa na mvua chache na hivyo kusababisha malengo kutofikiwa.
Kwa mujibu wa Diwani wa Kata hiyo kati ya kaya 2,124 zilizopo, zinazokabiliwa na tatizo la upungufu wa chakula ni 272 zenye jumla ya wakazi 1,904.
“Kaya zenye upungufu wa chakula ni kaya 70 za Kijiji cha Saranda zenye watu 490, Ilaloo ni kaya 54 zenye watu 378, Sukamahela ni kaya 68 zenye watu 476 na Ilucha chenye kaya 80 zenye watu 560,” alifafanua diwani huyo.
Kuhusu bei za mazao katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka 2013/2014, diwani huyo alibainisha kwamba debe la mahindi linauzwa kwa sh 8,000; debe la mtama sh 7,000 na mpunga sh 8,000.
Akizungumzia hali ya mavuno kwa msimu wa 2012/2013, diwani huyo alisema kata hiyo ilitarajia kuvuna tani 2,509.6 na badala yake ilivuna tani 111.5 kwa mazao ya chakula wakati kwa mazao ya biashara ilitarajia kuvuna tani 1,255 lakini ilivuna tani 390 tu.
Kata ya Saranda ina vitongoji 16, vijiji vinne, kaya 2,124 zenye wakazi wapatao 12,412 wakiwemo wanaume 6,590 na wanawake 5,822 huku kukiwa na kaya 2,092 tu zinazoshiriki kazi za kilimo.
Via: Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment