TAFSIRI NA UKALIMANI
Tafsiri [Translation]
Imeandaliwa na Mwl. Venance. F
Anapatikana kwa simu: 0715 33 55 58,
barua pepe: furahavenance@gmail.com
Imeandaliwa na Mwl. Venance. F
Anapatikana kwa simu: 0715 33 55 58,
barua pepe: furahavenance@gmail.com
Dhana ya Tafsiri.
Tafsiri imefasiliwa kuwa, ni Kutoa mawazo kutoka katika lugha moja kwenda
lugha nyingine bila ya kubadilisha maana. [TUKI 2002: 271]
Catford [1965:20] anasema tafsiri
ni, “Kuchukua mawazo yaliyo katika maandishi kutoka lugha moja {lugha
chanzi} na kuweka badala yake mawazo yanayolingana katika lugha nyingine {lugha
lengwa}.
Vilevile imefasiliwa kuwa ni “Mawazo
yaliyotolewa kutoka lugha moja hadi lugha nyingine.”
TUKI [2002: 271] Tafsiri ni kueleza maana ya maneno kutoka lugha moja
kwenda lugha nyingine.
Maana zote hizo tulizoziangalia,
utaona kuwa, kuna mambo matatu muhimu yanayojitokeza, mambo hayo ni:
(i)
Mawazo
yanayotakiwa kutafsiriwa sharti yawe katika maandishi.
(ii)
Mawazo au
ujumbe kati ya lugha chanzi na lugha lengwa sharti yalingane.
(iii)
Tafsiri
inaweza kuwa kutoa maana ya maneno au mawazo.
Baada ya kuangalia maana ya
tafsiri, sasa tuangalie maana ya mfasiri na sifa anazotakiwa kuwa nazo mfasiri:
Mfasiri
Mfasiri ni mtu anayefanya tafsiri
kutoka lugha moja hadi lugha nyinge.[TUKI:2000:165]
Kwa ujumla tunaweza kusema kuwa,
mfasiri ni mtu anayehamisha mawazo kutoka lugha moja (lugha chanzi) kwa kutumia
lugha nyingine ili mawazo hayo yaeleweke na watu wasiojua au kuielewa lugha
chanzi, na mawazo hayo sharti yawe katika maandishi.
Sifa za mfasiri bora
Mfasiri bora anatakiwa kuwa na
sifa zifuatazo:
Ø
Awe na
ujuzi wa lugha fasaha, hii ina maana kuwa awe anajua kwa ufasaha lugha zote
mbili, yaani lugha chanzi na lugha lengwa.
Ø
Awe na
ufahamu mkamilifu wa ujumbe au mada iliyoandikwa katika matini chanzi na uwezo
au jinsi ya kuelezea ujumbe au mada hiyo kwa ufasaha katika lugha lengwa.
Ø
Awe
amesoma maandishi ya matini chanzi hadi ayafahamu kinaga ubaga halafu aweze
kuyafikiria katika lugha lengwa.
Historia ya Tafsiri Afrika mashariki
Taaluma hii ya tafsiri ina
historia ndefu hapa dunia tangu kale, lakini kwa hapa Tanzania na Afrika
mashariki kwa ujumla historia hii ya tafsiri haina historia ndefu kwani
inaanzia karne ya 19 ambapo wamisionari walitafsiri vitabu mbalimbali vya
kikristo ikiwemo biblia kutoka lugha
ya kiingereza kwenda Kiswahili na lugha nyingine za makabila makubwa nchini
Tanzania.
Na hata wakati wa utawala wa
kikoloni hasa waingereza walitafsiri maandiko mbalimbali ya taaluma na fasihi
ya Ulaya kwa lugha ya Kiswahili Na hata baada ya uhuru wapo wazalendo
waliofanya juhudi za kutafsiri vitabu mbalimbali kwa lugha ya Kiswahili mfano
mzuri ni Rais wa kwanza wa Tanzania Mwalimu Julius K. Nyerere ambaye alitafsiri
vitabu viwili vya mwandishi mashuhuri wa tamthiliya wa Uingereza William
Shakespeare ambavyo ni: Juliasi Kaizari [1963]
na Mabepari wa Venisi[1969] {Tazama
pia Mwansoko na wenzake 2006 : 5}
Mfano wa
tafsiri ambazo zimetafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili ni pamoja na ya,Ayi Kwei
Armah, Wema Hawajazaliwa ambayo
imetafsiriwa na Abdilatif Abdalla, House
boy ya Ferdinand Oyono iliyotafsiriwa na Raphael Khasao na Nathan Mwele. Juliasi Kaizari na Mabepari wa Venisiza zaWilliam Shakespeare zilizotafsiriwa na
Julius K. Nyerere, Hekaya za Abunuwasi,
Kimetafsiriwa na Interterritorial Language Committee, East Africa, Alfu Lela Ulela: Kimetafsiriwa na Sir
Richard Burton na Mashimo ya Mfalme
Suleiman kilichotafsiriwa na Sir Rider Haggard, Takadini,kimetafsiriwa na Mathews Bookstore and Stationers, Nitaolewa Nikipenda ambacho
kimetafsiriwa na Crement M. Kabugi. vitabu vingine vilivyotafsiriwa ni kama
vile; Orodha, Barua Ndefu Kama Hii n.k.
Mpaka sasa wataalamu mbalimbali
wamekuwa wakiendelea kutafsiri maandiko mbalimbali kama vile mikataba na ripoti
mbalimbali za kimataifa, sheria ambazo mwanzo zilikuwa zikiandikwa kwa lugha ya
kiingereza, vitabu vya kiada na ziada, kazi za kifasihi, n.k
Mambo ya kuzingatia katika tafsiri
Katika sehemu hii tutaangalia
mambo muhimu yanayotakiwa kuzingatiwa katika tafsiri, hivyo basi, tutagawa
mambo hayo ya kuzingatia katika sehemu mbili, sehemu ya kwanza ni mambo ya
kuzingatia kabla ya kuanza mchakato wa kutafsiri na sehemu ya pili, tutaangalia
mambo muhimu ya kuzingatia wakati wa mchakato wa kutafsiri. Tukianza na:
[a] Mambo ya kuzingatia kabla ya
kuanza mchakato wa kutafsiri.
1.
Kwanza
unatakiwa kusoma matini nzima.
Mtu anayetaka
kutafsiri matini yoyote ile jambo la msingi la kuzingatia ni kuisoma matini
nzima tena kwa umakini ili kuelewa maudhui ya matini chanzi, kuweka alama
sehemu za matini zenye utata au zisizoeleweka vizuri, hii itamsaidia kubaini ni aina gani ya
marejeo muhimu yatakayomsaidia kutafsiri mfano wa marejeo hayo ni kama kamusi,
ensiklopedia, orodha ya msamiati na istilahi mpya.
2.
Unatakiwa
kubaini lengo la matini chanzi
Baada ya kuisoma
matini chanzi, je! Umeweza kubaini lengo la matini chanzi ni nini? Kubaini
lengo la matini kutakusaidia kuweza kutafsiri bila kutofautiana/kukinzana na
lengo la matini chanzi, mathalani, matini mbili tofauti zinaweza kueleza jambo
lilelile na kutumia data zilezile lakini mtindo wa lugha uliotumika unaweza
ukaonesha mitazamo miwili tofauti.
Hebu angalia
tamthilia ya Mercant of Venice, iliyoandikwa
na William Shakespeare na kutafsiriwa
na Mwalimu J.K. Nyerere kwa lugha ya Kiswahili na kuitwa Mabepari wa Venisi, kumbuka kuwa tamthiliya hiyo ingeweza kuitwa
pia Wafanyabiashara wa Venisi lakini
ukiangalia tafsiri ya kwanza [Ya Mwalimu Nyerere] inatupa hisia hasi wakati ya
pili huwezi kupata hisia yoyote.{Mwansoko na wenzake 2006:15}
3.
Unatakiwa
kubaini hadhira/ wasomaji lengwa.
Kabla ya mfasiri
hajabaini wasomaji au hadhira ya wasomaji wa matini yake ya tafsiri ni vema
kwanza akaibaini hadhira ya matini chanzi na ndipo abaini hadhira/ wasomaji
mahususi wa matini yake ya tafsiri, maswali anayotakiwa kujiuliza mfasiri ili
aweze kuibaini hadhira ya matini yake ya tafsiri ni: je msomaji wa tafsiri yake
ni nani? Ana kiwango gani cha elimu, ni msomi wa kawaida au msomi aliyebobea?
Wana umri gani na ni jinsia gani? Je hadhira yake imo katika tabaka gani katika
jamii? Baada ya kupata majibu ya maswali hayo, mfasiri atakuwa ameibaini
hadhira yake,na hii itamsaidia mfasiri kuamua umbo la matini yake, kama ataamua
iwe katika umbo la gazeti, jarida, kijarida, n.k. jambo la kuzingatia umbo la
matini ya tafsiri ishabihiane na hadhi ya umbo la matini chanzi. Kwa kuibaini
hadhira ya matini lengwa itamsaidia mfasiri kuamua kuirahisisha tafsiri yake au
kuifanya iwe ngumu kutegemeana na uwezo wa hadhira ya tafsiri lengwa.
4.
Unatakiwa
kubaini mtindo wa matini chanzi.
Vilevile,
mfasiri anatakiwa kujua, matini chanzi imetumia mtindo gani katika kuwasilisha
maudhui yake, imetumia mtindo wa kirasimu? Au imetumia mtindo wa kitaaluma? Je
imetumia mtindo wa kiuandishi wa habari au mtindo wa kimawasiliano yasiyo
rasmi? Je ametumia lugha rasmi au ya mtaani? Na inatakiwa mtindo wa matini
chanzi ilingane na ile ya matini lengwa. Tazama mifano ifuatayo:
Kingereza: Please, Sir do no mind it! If I arrive earlier I’ll wait for you
Kiswahili: Mkubwa! Kausha tu! Na kama nitatia maguu mapema,
nitakusikilizia Palepale
Ukiangalia mfano
huo, utaona kuwa, mitindo iliyotumika katika sentensi hizo ni mitindo miwili
tofauti, katika mfano tuliouangalia katika lugha chanzi, mtindo wa lugha
uliotumika ni mtindo rasmi, wakati katika tafsiri [lugha lengwa] mtindo
uliotumika ni mtindo wa lugha ya mtaani, jambo ambalo si zuri katika tafsiri. Mtindo
wa lugha lengwa sharti ulingane na mtindo wa lugha chanzi.
hivyo katika
mfano huo, mtindo sahihi ungetakiwa kuwa;
Tafadhari! usijali! kama nitafika mapema,
nitakusubiri.
5.
Kusoma
matini kwa mara ya mwisho
Jambo lingine la
kuzingatia ni kuisoma upya matini chanzi. Katika kipengele hiki, mfasiri
anashauriwa aisome matini chanzi kwa mara ya mwisho huku akipigia mstari au
kuandika katika kidaftari kidogo msamiati, istilahi na misemo muhimu ya matini
chanzi kama vile, methali, nahau maneno ya kitamaduni yasiyotafsirika, majina
maalumu, n.k. kwa kupigia mstari au kuyaandika katika kidaftari kidogo ili iwe
rahisi kwa mfasiri kuyatafutia visawe vyake kabla hata ya kuanza kutafsiri lakini pia kumsaidia mfasiri asiyasahau
wakati wa kutafsiri.
Hayo ndiyo mambo
ambayo, mfasiri anatakiwa kuyazingatia kabla hajaanza mchakato wa kutafsiri.
Hivyo basi, sasa tugeukie upande wa pili ambao ni:
[b] Mambo ya kuzingatia wakati wa mchakato wa kutafsiri.
1.
Maandalizi ya kutafsiri
Katika hatua
hii, mfasiri anatakiwa kufahamu vizuri maudhui ya matini chanzi, ujumbe wake,
mtindo wa matini na kuwekea alama sehemu zenye utata au zisizoeleweka vizuri,
anashauriwa kupigia mstari au kuandika katika kidaftari kidogo msamiati,
istilahi na misemo muhimu ya matini chanzi kama vile, methali, nahau maneno ya
kitamaduni yasiyotafsirika, majina maalumu, n.k. kwa kupigia mstari au
kuyaandika katika kidaftari kidogo ili iwe rahisi kwa mfasiri kuyatafutia
visawe vyake kabla hata ya kuanza kutafsiri
lakini pia kumsaidia mfasiri asiyasahau wakati wa kutafsiri au kuyatolea
ufafanuzi zaidi katika tafsiri yake.
2.
Uchambuzi wa matini chanzi
Katika hatua
hii, mfasiri anatakiwa kuchunguza kwa makini maneno, methali, nahau, misemo
pamoja na maelezo mengine ya matini chanzi aliyoyaandika au kuyapigia mstari
katika hatua ya maandalizi na kuyatafutia visawe vyake katika lugha lengwa,
hapa mfasiri anashauriwa kutumia marejeo mbalimbali kama vile, kamusi,
ensiklopedia, orodha ya msamiati na istilahi mpya.
Mfasiri
anatakiwa kuwa na shajara au daftari dogo kwa ajili ya kuandika na kuhifadhi
maneno na maelezo muhimu ya matini chanzi na visawe vyake, visawe
vinavyoonekana kufaa viorodheshwe vizuri ili iwe rahisi kuvirejelea wakati wa
kutafsiri, vilevile mfasiri kama ataona kuwa matini chanzi ni ndefu sana,
anashauriwa kuigawa matini hiyo katika sehemu ndogondogo kama vile, sura, aya
au sentensi na kuanza kushughulikia sehemu moja baada ya nyingine.
3.
Uhawilishaji
Uhawilishaji ni
uhamishaji wa mawazo kutoka lugha chanzi kwenda lugha lengwa, au uhamishaji wa
mawazo au ujumbe kutoka matini asilia kwenda matini ya tafsiri. Hii ina maana
kuwa katika hatua hii, visawe vya kisemantiki [kimaana] vya matini chanzi
vilivyobainishwa katika hatua ya uchambuzi huamishwa katika matini lengwa
[kutoka lugha chanzi kwenda lugha lengwa] na kupangwa vizuri kisarufi na
kimantiki ili fasiri hiyo iwe na maana kwa wasomaji wake.
4.
Kusawidi /Kuandaa rasimu ya kwanza ya
tafsiri.
Katika hatua
hii, mfasiri huandika rasimu yake ya kwanza ili kupata picha fulani ya matini
aliyoikusudia, katika uandaaji wa rasimu ya kwanza, kwa kufanya hivi, mfasiri
anaweza kugundua kuwa anahitaji taarifa zaidi tofauti na alizozipata katika
hatua ya uchambuzi, na hivyo kulazimika kuchunguza zaidi matini chanzi na hata
kupekua zaidi na zaidi marejeo yake aliyoyaandaa kwa kuyatumia katika tafsiri.
Jambo la kuzingatia, mfasiri anatakiwa wakati akihamisha mawazo au ujumbe
azingatie umbo na lengo la matini chanzi ili kutoathiri tafsiri yake.
5.
Kudurusu / kuipitia rasimu ya kwanza
Baada ya
kusawidi rasimu ya kwanza, mfasiri anatakiwa kuivundika rasimu yake ya tafsiri
kati ya juma moja hadi mawili baada ya kukamilika kwake na kuanza kuidurusu/
kuipitia rasimu hiyo kwa jicho la kihakiki zaidi na kuangalia kama kuna makosa
ambayo yamejitokeza katika rasimu yake au la na kuyafanyia marekebisho pale inapobidi.
6.
Kusomwa kwa rasimu ya tafsiri na mtu/watu
wengine
Baada ya mfasiri
kuipitia rasimu yake ya kwanza, na kuifanyia masahihisho kwa makosa
yaliyojitokeza, anatakiwa kuwapa watu wengine waidurusu rasimu hiyo
iliyofanyiwa marekebisho ili waipitie tena na kuirekebisha, hivyo basi wasomaji
hao wanaweza wakahakiki,wakashauri, n.k.
Wasomaji hawa husaidia kuona kama tafsiri iko sahihi, inaeleweka na ina
mtiririko mzuri wenye mantiki.
7.
Usawidi /Kuandika rasimu ya mwisho
Baada ya kupata
maoni kutoka kwa wasomaji wa pili, mfasiri anaweza kuyatumia maoni, mapendekezo
na maelekezo yao kusahihisha tena tafsiri yake na hatimaye kuandaa na kutoa
rasimu ya mwisho ambayo itakuwa tayari kwa kusomwa na wasomaji.
Njia / mbinu za Tafsiri
Zipo njia mbalimbali ambazo
hutumika katika kutafsiri, baadhi ya njia hizo ni kama vile:
(i)
Tafsiri ya neno kwa neno. [Word to word
translation]
(ii)
Tafsiri sisisi.[ Literal translation]
(iii)
Tafsiri ya kimaana/uwazi.[ Semantic translation]
(iv)
Tafsiri ya kimawasiliano.[Communicative
translation]
(i)
Tafsiri ya neno kwa neno [Word to word translation]
Hii ni aina ya tafsiri ambayo
mofimu na maneno hufasiriwa yakiwa pweke pweke kwa kuzingatia maana zake za
msingi bila kujali muktadha. Katika aina hii ya tafsiri mpangilio wa mofimu na
maneno wa lugha chanzi hubakia vilevile bila kubadilika. Na kwa kawaida matini
inayotafsiriwa huandikwa chini ya matini ya lugha chanzi. Tazama mifano
ifuatayo ya tafsiri ya neno kwa neno:
Kiswahili: Alisoma hadi asubuhi
Kingereza: He/past/study/until/morning
Kiswahili: Alikimbia mpaka ofisini kwake
Kingereza: He/past/run/until/office/his
Kiswahili: Anasoma kitabu changu
Kingereza: He/present/book/my
Kiswahili: Walikula chakula chote
Kingereza: They/past/eat/food/all
Umuhimu wa njia hii, humsaidia
mtu kuelewa muundo wa lugha chanzi na jinsi lugha chanzi inavyofanya kazi,
kaina hii ya tafsiri hutumiwa na wataalamu wa lugha kuonesha namna maumbo au muundo wa lugha chanzi ulivyo, lakini
mapungufu yake ni kuwa, aina hii ya tafsiri huwa haitoi maana inayokusudiwa kwa
uwazi zaidi.
(ii)
Tafsiri sisisi [ Literal translation]
Hii ni aina ya tafsiri ambayo
maneno hufasiriwa yakiwa pweke pweke kwa kuzingatia maana za msingi katika
lugha chanzi bila kujali sana muktadha lakini ni tafsiri inayofuata mfumo wa
kisarufi hasa kipengele cha kisintaksia ya lugha lengwa. Ebu tuangalie mifano
ifuatayo:
Kingereza: He was taken at the Central Police Station
Kiswahili: Alipelekwa kwenye kituo cha kati cha police.
Badala ya kuwa:
Alipelekwa
kituo kikuu cha polisi
(iii)
Tafsiri ya kisemantiki/maana au uwazi
[Semantic Translation]
Hii ni aina ya tafsiri ambayo
mfasiri huegemea zaidi kwenye lugha chanzi. Katika aina hii ya tafsiri, mfasiri
hufasiri kila neno katika sentensi jinsi lilivyo lakini kwa kufuata sarufi
hususani vipengele vya kisemantiki na kisintaksia ya lugha chanzi. Inaitwa
tafsiri ya kisemantiki kwa sababu, mfasiri anapofasiri hutakiwa kuweka mkazo
kwenye maana ya matini kama ilivyokusudiwa na mwandishi wa matini chanzi.
Katika aina hii ya tafsiri,
masahihisho au urekebishaji wa neno au jambo lolote unalodhani limekosewa
haliruhusiwi isipokuwa unaweza kuweka hayo marekebisho au ufafanuzi katika
tanbihi. Sasa tuangalie baadhi ya mifano ya aina hii ya tafsiri:
Kiswahili: Alikwenda mpaka hospitali
Kingereza: He went up to hospital
Kingereza: Jane married John
Kiswahili: Jane alimwoa John
Aina hii ya tafsiri, ina faida
kubwa katika ukuaji wa lugha lengwa kwa kuingiza miundo ya misemo kutoka lugha
chanzi, mathalani, lugha ya Kiswahili imepokea miundo mipya ya misemo kutoka
lugha ya Kingereza, baadhi ya miundo hiyo ni kama vile:
Kiswahili: Usiku mwema à kutoka Kingereza:
Good night
Kiswhili: Mabibi na mabwana à
kutoka Kingereza: ladies and gentlemen
Kiswahili: Wako
mtiifu à Kutoka Kiingereza: Yours Sincerel
Kiswahili:
Naomba nichukue nafasi hii.. à
Kutoka Kiingereza: May I take this opportunity…
[Tazama pia Mwansoko na
wenzake: 2006]
(iv)
Tafsiri ya kimawasiliano/ huru
[Communicative Translation]
Hii ni aina ya tafsiri
inayomlenga msomaji [hadhira] wa matini lengwa, ambaye katika aina hii ya
tafsiri hatarajii kukutana na ugumu wowote katika matini atakayoisoma, bali
hutarajia kukutana na tafsiri nyepesi ya dhana za kigeni katika utamaduni na lugha
yake kwa kadiri itakavyoonekana. Hivyo basi, mfasiri wa aina hii ya tafsiri
yuko huru kutafuta maneno na mafungu ya maneno yanayolingana na maneno,
methali, nahau, utamaduni na mazingira ya lugha lengwa, pamoja na kuwa tafsiri
ya kimawasiliano kufuata sarufi ya lugha lengwa ni lazima pia ifuate utamaduni,
mazingira na historia ya jamii ya lugha lengwa. Tuangalie mifano ifuatayo:
Kingereza: Jane married John
Kiswahili: John alimwoa Jane
Kingereza: No need to cry over spilt milk
Kiswahili: Maji yakimwagika hayazoleki
Kiingereza: What comes around goes arround
Kiswahili: Mla vya watu, naye vyake huliwa.
Kiswahili: Akufaaye kwa dhiki ndiye rafiki wa kweli
Kiingereza: A friend in need is a friend in need
Kiswahili: Bahati haiji mara mbili
Kiingereza: Golden chance never comes twice
Aina hii ya tafsiri hulenga kutoa
athari ile ile au inayokaribiana kwa hadhira ya matini lengwa kama ilivyo kwa
hadhira ya matini chanzi[ matini asilia], hii ni aina ya tafsiri ambayo
hutumika sana kufasiri mawazo ya kigeni katika lugha na mazingira mapya, mawazo
ambayo huelezwa katika misingi ya lugha, utamaduni na mazingira yanayoeleweka
kwa hadhira ya matini lengwa.
Ebu tuangalie baadhi ya mifano
tuliyoiangalia katika tafsiri ya Kisemantiki [maana] tunavyoweza kutafsiri
katika njia ya tafsiri ya kimawasiliano:
Kiingereza Kiswahili
Good night
Lala salama
Ladies and Gentlemen Ndugu zangu
Yours Sincerely Ni mimi
May I take this opportunity
to… Naomba mnisikilize
Hivyo basi, katika aina hii ya
tafsiri, mfasiri hutafuta methali au misemo inayopatikana katika lugha lengwa
inayohusiana au kukaribiana na ile ya lugha chanzi. Ebu jaribu kutafsiri
misemo/methali zifuatayo ya lugha ya Kiswahili kwenda lugha ya Kiingereza:
Adhabu ya kaburi aijuaye maiti
Asiyekubali kushindwa si mshindani
Asiyefunzwa na mamaye hufunzwa
Chema chajiuza kibaya chajitembeza
Dua la kuku halimpati mwewe
Bandubandu humaliza gogo
Jogoo wa shamba hawiki mjini
La kuvunda halina ubani
Mtegemea cha nduguye hufa masikini
Faida ya aina hii ya tafsiri,
humfanya mfasiri kuwa huru kutumia maneno au mafungu ya maneno ambayo huweza
kutoa athari ile ile au inayokaribiana na maneno au mafungu ya maneno katika
matini ya lugha chanzi, lakini mapungufu ya aina hii ya tafsiri huweza kutokea
iwapo mfasiri ataamua kuegemea mno kwenye mawazo, historia, mazingira au
itikadi ya lugha lengwa. Ebu tuangalie mifano ifuatayo:
Kingereza: The Merchant of Venice
Kiswahili: Mabepari wa Venisi
Ukiangalia mfano huo utaona kuwa,
The Merchant of Venice, tamthiliya iliyoandikwa na William Shakespeare, ingefaa
pia kufasiriwa kuwa, Wafanyabiashara wa Venisi, lakini Mwalimu J.K Nyerere
aliamua kuifasiri kuwa, Mabepari wa Venisi kutokana na kuwa Nyerere ndiye
mwasisi wa itikadi ya Ujamaa nchini Tanzania, hivyo aliegemea katika itikadi
kufasiri.
Hivyo basi, mtu anapokuwa
anafanya kazi ya kufasiri, maandishi yo yote kutoka lugha moja kwenda lugha
nyingine atajikuta akiangukia katika moja wapo ya njia tulizozijadili hapo juu,
lakini ikumbukwe tafsiri ya neno kwa neno ni nadra sana kutumiwa na wafasiri
wengi, na njia hizo huweza kuingiliana katika matini moja ya tafsiri.
Ukalimani [Interpritation]
Ukalimani ni nini?
Ukalimani
imefasiliwa kuwa ni, uhusishaji wa kuhamisha maana kutoka lugha moja (lugha
chanzi) kwenda lugha nyingine (lugha lengwa) katika mazungumzo. Hivyo basi
tunaweza kusema pia, ukalimani ni hali ya mtu kuhamisha mawazo ya
kinachozungumzwa kutoka lugha moja kwenda lugha nyingine katika mazungumzo. Hii
ina maana kuwa ukalimani ni lazima uhusishe pande mbili, upande wa kwanza
sharti awepo mtu anayezungumza lugha fulani na upande mwingine kunakuwa na mtu
ambaye anasikiliza hicho kinachozungumzwa na kuyarudia hayo yanayozungumzwa kwa
kutumia lugha nyingine tofauti na ile iliyotumiwa na mazungumzaji wa kwanza.
Hivyo basi,
ukiangalia, maana hiyo tuliyoiangalia utaona kuwa, ukalimani ni taaluma
inayohusu mazungumzo wakati tafsiri yenyewe uhusu maanadishi, kwa maana hiyo
huwa tunatafsiri maandishi kutoka lugha moja kwenda lugha nyingine na
tunakalimani mazungumzo kutoka lugha moja kwenda lugha nyingine.
Ukalimani
ulianza pale ambapo mataifa mbalimbali yenye kuzungumza lugha tofauti tofauti
yalipoanza kuingiliana na kushirikiana katika shughuli mbalimbali za kijamii,
kisiasa, kichumi na kiutamaduni, kwa mfano ujio wa wageni Afrika Mashariki kama
vile Waarabu, Wajerumani na Waingereza ili waweze kuwasiliana na wenyeji wao
waliambatana na watu ambao walikuwa wakiwatumia kama wakilamani wao.
Kwa sasa hivi
ukalimani umekuwa kama taaluma muhimu, ukalimani unafanyika katika mahakama,
kanisani, katika mikutano ya kimataifa, mahubiri ya kidini, n.k na kutokana na
maendeleo ya sayansi na teknolojia, kuna vifaa maalumu ambayo hutumika
kukalimani mazungunzo kutoka lugha moja kwenda lugha nyingine, ambayo huvaliwa
masikioni katika kumbi za mikutano. Na sasa ni taaluma inayofundishwa katika
shule za sekondari na elimu ya juu kama ilivyo kwa tafsiri kutokana na umuhimu
wake.
Mkalimani ni mtu muhumi sana katika
kufanikisha mawasiliano kwa watu wanaotumia lugha mbili tofauti, au lugha
inayotumika katika eneo hilo msikilizaji haielewi na haijui na ndiyo maana
utakuta wakalimani wakihitajika mahakamni, mikutano ya kimataifa, katika
mahubiri ya kidini au mahali popote pale ambapo wazungumzaji hawawezi kuelewana
kwa kuwa wanatumia lugha tofauti.
Sifa za mkalimani bora
Ø
Awe mtu anayezielewa lugha chanzi na lugha
lengwa vizuri
Ø
Awe ni mtu ambaye ameishi pande zote za lugha
anazozikalimani ili kuelewa mila na desturi za watumiaji wa lugha hizo.
Ø
Awe stadi wa ukalimani, hapa inatakiwa awe na
uhodari wa kukalimani, kuzungumza vizuri, maneno kusikika, awe na uwezo wa
kukalimani neno kwa neno au sentensi na sentensi, kutumia ishara zinazoambatana
na ishara za mzungumzaji wa lugha chanzi na hata kutumia mtindo anaodhani
unaweza kuwavutia wasikilizaji wake.
Ø
Muadirifu, ambaye hawezi kupotosha au kubadili
ukweli wa kinachozungumzwa, nah ii ni muhimu kwa sababu wakalimani hutumika
hadi mahakami hivyo kama si mwadirifu huweza kuufanya upande mmoja ukakosa haki
inayostahiri.
Ø
Asiwe mbaguzi, hapa ina maana mkalimani asiamue
kupotosha ukweli wa kile kinachozungumzwa kwa kuwa tu kinaendana kinyume na
itikadi yake ya kisiasa, kidini, kiutamaduni, n.k. wala asiangalie jinsia ya
mtu umri au hali ya mtu anayemfanyia ukalimani.
Kielelezo: 1
Namna mkalimani
anavyotakiwa kuwa
sambamba na mzungumzaji
Mambo ya kuzingatia katika Ukalimani
Kwa ujumla yapo
mambo kadha wa kadha, ambayo mkalimani anatakiwa kuyazingatia anapotaka kufanya
ukalimani, mambo hayo tunaweza kuyagawa katika makundi mawili, ambayo ni:
- Kabla ya kuanza ukalimani
Katika hatua
hii, mkalimani anatakiwa kuzingatia mambo yafuatayo:
(a) Awe na uelewa mzuri wa lugha zote anazotaka
kukalimani, hapa tuna maana kuwa awe na uwezo wa kuzungumza na kuelewa lugha
chanzi na lugha lengw, hii itasaidia mkalimani kutopotosha kile
kinachozungumzwa na mzungumzaji wa lugha chanzi.
(b)
Awe anaijua
historia na utamaduni wa jamii zote mbili, yaani ile ya lugha chanzi na ile ya
lugha lengwa.
(c) Kama ni ukalimani rasmi, ni vizuri kwa
mkalimani akamjua mzungumzaji wa lugha chanzi, ni vema pia ukafanya naye
mazungumzo kidogo ili kumzoea, na kutambua vionjo vyake ili iwe rahisi kwa
mkalimani pindi atakapokuwa anafanya ukalimani asionekane kama mgeni.
(d) Vilevile ni muhimu kwa mtu anayekalimani,
akawa na uelewa mzuri wa mada inayozungumzwa, hii itamrahisishia mkalimani
katika ukalimani wake.
- Katika ukalimani wenyewe
Mkalamani
anapokuwa amesimama mbele ya hadhira [wasikilizaji] pamoja na mzungumzaji wa
lugha chanzi kwa ajili ya kuanza ukalimani, anatakiwa kuzingatia mambo
yafuatayo:
(a) Kuwa makini katika kusikiliza kile
kinachozungumzwa na mzungumzaji wa lugha chanzi ili kuepuka kuachwa mahali na
kuepuka kumuomba mzungumzaji kurudia mara kwa mara.
(b) Itambue hadhira ya lugha lengwa, ni watu wa
namna gani, wana kiwango gani cha elimu, ni wasomi wa kawaida au waliobobea, ni
watu wa jinsia na umri gani,? Hii itakusaidi kujua aina ya msamiati na miundo
ya tungo utakayoitumia, kama iwe rahisi au migumu kutokana na hadhira yako
ilivyo.
(c) Tumia mitindo unayodhani itaeleweka vema na
hadhira/ wasikilizaji wa lugha lengwa, kwa mfano kama hadhira yako ni vijana,
jaribu kutumia mitindo inayopendwa na vijana, kama wasikilizaji wako ni watu
rasmi na we huna budi kuwa rasmi.
(d) Weka mkazo sehemu ambazo mzungumzaji wa
lugha chanzi anaweka mkazo ili kuepuka utofauti yako na mzungumzaji wa lugha
chanzi, na hata kuepuka kuathiri lengo la mzungumzaji wa lugha chanzi.
(e) Unatakiwa pia kutumia ishara zinazotumiwa na
mzungumzaji wa lugha chanzi, hii itawafanya wasikilizaji waamini kile
kinachozungumzwa na mzungumzaji wa lugha chanzi ndiyo kilekile kinachozungumzwa
na mkalimani.
Mkalimani anatakiwa kutumia ishara
zinazotumiwa na mzungumzaji.
na si kama inavyoonekana katika mchoro huu.
Tazama kielelezo na. 2
(f) Usiwe muda mwingi unamtazama mzungumzaji wa
lugha chanzi na kusahahu kuitazama hadhira yako, hivyo unatakiwa kuitazama
hadhira yako ili kugundua kama wako pamoja na wewe au kuna sehemu hawajakuelewa
ili uweze kuwafafanulia zaidi.
(g) Muombe mzungumzaji wa lugha chanzi kurudia
sehemu unayodhani hujaisikia au hujaielewa vizuri, kwani ni makosa kwa
mkalimani kukalimani sehemu au jambo ambalo hukulisikia vizuri au kulielewa.
Hivyo basi hayo
ndiyo mambo muhimu ambayo mkalimani anatakiwa kuyazingatia anapokuwa anafanya
ukalimani. Jambo la kuzingatia, mkalimani hutakiwa kuingiza hisia zako
unapokuwa anafanya ukalimani. na ukalimani mzuri unawezekana kwa kiwango
ambacho mila na desturi zote yaani za lugha chanzi na lugha lengwa zinalingana
ama kushabihiana.
Dhima za Tafsiri na Ukalimani
Tafsiri na Ukalimani ina dhima
zifuatazo:
F
Hutuwezesha kujifunza lugha tofauti.
Kati ya mazoezi mazuri anayoweza
kutumia mtu katika kujifunza lugha nyingine, basi zoezi la kutafsiri au
kukalimani mara kwa mara humsaidia mtu kujifunza lugha kwa urahisi zaidi, kwani
kwa kufanya tafsiri ya mara kwa mara kutamsaidia mtu kugundua miundo na
vipengele mbalimbali vya lugha na jinsi vinavyofanya kazi katika lugha
anayojifunza.
F
Hutumika kama njia ya mawasiliano.
Kutokana na maingiliano ya
mataifa mbalimbali yanayotumia lugha tofauti tofauti, tafsiri hutumika
kurahisisha mawasiliano baina ya makundi ya watu wanaotumia lugha tofauti
tofauti, hutumika kutolea maelezo ya kibiashara kama vile maelekezo ya jinsi ya
kutumia bidhaa mbalimbali zinazozalishwa nje au zinazouzwa nje ya nchi, katika
matangazo ya kitalii ili kuwavutia watalii kutoka mataifa mbalimbali, vilevile
hutumika katika vyombo vya habari, tafsiri pia inatumika katika nyaraka rasmi,
mikataba, vitabu vya ziada na kiada, lakini pia ukalimani hulahisisha
mawasiliano miongoni mwa watu wanaozungumza lugha tofauti.
F
Tafsiri na Ukalimani hutumika kueneza
utamaduni.
Tafsiri imekutanisha lugha na
tamaduni mbalimbali duniani na kusababisha tamaduni na lugha hizo kuathiriana,
kwa mfano mara baada ya waarabu kuingia Afrika Mashariki na vitabu mbalimbali
vya Kiarabu na Kiislamu kutafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili ilisababisha
utamaduni wa Kiswahili kuathiriwa na utamaduni wa Kiarabu na Kiislamu kutoka na
kuiga kwa mambo mengi kutoka huko, lakini pia hata walipokuja wazungu na
kutafsiri vitabu vyao vya kifasihi, kutafsiriwa kwa Biblia, n.k. ilisababisha
pia utamaduni wa Mswahili kuathiriwa na utamaduni wa Ulaya.
F
Tafsiri na Ukalimani ina dhima ya
kuwasilisha ujumbe wa manufaa kwa watu ambao hawafahamu lugha chanzi [lugha
asilia]
Changamoto/
mapungufu katika tafsiri na Ukalimani
Mfasiri katika kazi yake ya
kufasiri hukumbana na changamoto mbalimbali, ambazo huweza kusababisha tafsiri
kuwa na mapungufu ya hapa na pale. Baadhi ya changamoto au mapungufu hayo ni
kama vile:
(i)
Tofauti za
kiisimu kati ya lugha chanzi na lugha lengwa.
Tofautui za maumbo, miundo na
maana kati ya lugha ya Kiswahili na lugha ya Kingereza wakati mwingine
husababisha matatizo au upungufu katika tafsiri na ukalimani. Kwa mfano maumbo
ya vitenzi vya Kiingereza huruhusu kauli nyingi elekezi kutoonesha umoja au
wingi wa wahusika wala majina ya vitu mahususi vinavyoambatana na maelekezo
yanayotolewa tofauti maumbo ya vitenzi vya Kiswahili ambavyo huonesha umoja na
wingi wa wahusika na hata kuwa na majina ya vitu husika, tazama mifano ifuatayo
kama ilivyotolewa na, Mwansoko [2006]
Kingereza
Kiswahili
No parking à Usiegeshe gari hapa [je
kisichoruhusiwa kuegeshwa ni gari tu?]
No Smoking à Usivute sigara[ Je ni sigara
tundiyo hairuhusiwi kuvutwa?]
Arrivals à Wanaowasili
Departures à Wanaosafiri
Vilevile tofauti za maana kati ya
lugha ya Kingereza na Kiswahili huweza kuathiri tafsiri au ukalimani,
mathalani:
Kiswahili
Kingereza
Wasiojiweza à Disabled [Siyo wote wasiojiweza ni
walemavu]
[na siyo walimavu wote hawajiwezi]
Wezi wa mifukonià
Pickpockets [Hawaibi kwenye mifuko, wanaiba kutoka mifukoni]
(ii)
Tofauti za mitindo kati lugha chanzi na
lugha lengwa
Tofauti za mitindo ya uzungumzaji
pia, huweza kuathiri tafsiri na ukalimani na hii ni kwa sababu unaweza kukuta
kuna mitindo fulani inaweza kutumika katika muktadha fulani lakini ikishindwa
kupata tafsiri katika lugha nyingine katika muktadha ule ule.mathalani:
Kingereza:
Kiswahili
(i)
Thou shalt not
steal [mtindo wa kidini] à Usiibe
Do not steal
[mtindo wa kawaida] à
Usiibe
(ii)
Lend me your
ears [mtindo wa kishairi] à Naomba mnisikilize
May I have your attention [kawaida] à Naomba
mnisikilize
Tafsiri zote tulizoziangalia
katika mfano wa (i) na (ii) zimetoa maana au taarifa ili ile iliyomo katika
matini chanzi lakini tafsiri hizo hazikuzingatia mtindo wa lugha iliyotumika
katika matini chanzi.
(iii)
Tofauti za kitamaduni kati ya lugha chanzi
na lugha lengwa
Tofauti za kiutamaduni, yaani
taofauti za kimila, desturi na mazingira ya watumiaji wa lugha chanzi na lugha
lengwa huweza kufanya tafsiri au ukalimani kuwa mgumu, kwa mfano, katika
utamaduni wa Waingereza wana milo minne wakati Waswahili wana milo mitatu na
hii hupelekea kuwa vigumu kupata dhana za milo ya hiyo ya Waingereza katika
dhana ya Kiswahili. Mfano:
Waingereza wana: Waswahili wana:
Breakfast ------------------ Kifungua kinywa
Lunch …………………... Chakula cha
mchana
High tea ……………………?
Dinner ……………………Chakula cha
jioni
Supper …………………….?
Kwa hiyo ukiangalia mifano hiyo,
utaona kuwa, high tea na supper kuzipata dhana zake katika lugha
ya Kiswahili ni ngumu kutokana na kutokuwa na utamaduni wa kuwa na milo kama
hiyo kwa siku. Lakini pia inakuwa vigumu kupata tafsiri ya vyakula kama vile
ugali, makande katika lugha ya Kiingereza kutokana na kutokuwa na vyakula vya
aina hiyo.
(iv)
Tofauti za kiitikadi kati ya lugha chanzi na
lugha lengwa
Tofauti za kiitikadi pia huweza
kuathiri tafsiri na ukalimani, na hii ni kwa sababu, utakuta wafasiri wengi
hususani waandishi wa habari kuegemea katika itikadi zaidi, kwa mfano:
Kingereza
Kiswahili
Bussnessman à
mlanguzi
[tafsiri hii inatokana mfasiri kuathiriwa na itikadi
ya ujamaa]
mfanyabiashara [tafsiri hii inatokana
mfasiri kuathiriwa na
itikadi
ya ubepari]
Freedom fighter à
wapigania uhuru [Tafsiri ya
vyombo vya habari vya
Tanzania wakati wa kupigania uhuru]
Magaidi [Tafsiri ya idhaa ya BBC na
Radio za Afrika
Kusini wakati huo]
Hivyo basi kwa
kuhitimisha tunaweza kusema kuwa, ukalimani mzuri unawezekana kwa kiwango
ambacho mila na desturi zote yaana za lugha chanzi na lugha lengwa zinalingana
ama kushabihiana.
Na kutokana na
umuhimu wa taaluma hii ya tafsiri na ukalimani, serikali kupitia Baraza la
Kiswahili la Taifa Bakita [BAKITA] imeanzisha idara maalumu ya Tafsiri na
Ukalimani, na idara hiyo ina majukumu yafuatayo:
Ø
Kutoa huduma za tafsiri na ukalimani kwa lugha
mbalimbali kwa masharika, idara, wizara, balozi na watu binafsi.
Ø
Kuratibu na kutoa huduma za ukalimani kwenye
mikutano ya kitaifa na kimataifa na katika shughuli za masharika, makampuni na
watu binafsi.
Ø
Kupitia na kuthibitisha tafsiri zilizofanywa na
asasi mbalimbali au wafasiri wa nje.
Ø
Kutoa ushauri kuhusu masula ya tafsiri na
ukalimani.
MAZOEZI
&
Zoezi la kwanza
(a) Tafsiri
matini ifuatayo ya Kiswahili kwenda lugha ya Kiingereza.
MTO
(Siku ifuatayo, asubuhi. Ngoswe na Mitomingi wako kazini. Wanafika
nyumba moja).
MITOMINGI: Hodi! Hodi! Wenyewe! (Kimya, hakuna sauti itokayo). Hodi wenyewe
(Kimya) Labda hawajaamka.
NGOSWE: Kama bado wamelala tuwaache kwanza
tuwarudie baadaye.
MITOMINGI: Mimi naona itakuwa shida shida kwani nyumba
za hapa zimesambaa
mno.hebu nibishe
tena.hodi! hodi! Wenyewe mpo?(Akinyamaza
na
kunapita kimya. Punde mlango wafunguka na kipande cha
mwanamke chatokeza). Habari za asubuhi mama?
MAMA: Salama, mwaonaje?
MITOMINGI} Hatujambo
NGOSWE
MAMA: Sijui niwasaidie nini akina baba?
MITOMINGI: Mwenyewe yupo sijui?
MAMA: (Akitazama chini mwenye huzuni anatingisha kichwa). Hayupo
MITOMINGI: Katoka kitambo?
MAMA: (Akimtazama
Mitomingi kwa jicho kali). Ni marehemu.
MITOMINGI: (Amtazama Ngoswe ambaye kainamisha kichwa na wote
wanamtazama
kwa
jicho la huruma). Pole mama.
NGOSWE: Pole mama.
MAMA: Nimekwisha poa.
MITOMINGI: Samahani mama , hata sikufahamu.
MAMA: Sio neno baba sio kosa lako.
MITOMINGI: Mungu mkubwa.
MAMA: Nifanyeje; kazi ya Mungu haina
dosari. (Ananyamaza kwa kitambo). Je
niwasaidie nini?
MITOMINGI: Jambo moja dogo tu. Samahani kama
nitakusumbua maana kwanza ni
asubuhi tena yenyewe
ni msiba,
MAMA: Sio kitu baba.
MITOMINGI: Nadhani umepata kumsikia Balozi Mitomingi.
MAMA: Nimemsikia lakini kumwona bado.
MITOMINGI: Basi mama, huyo Mitomingi, Ngengemkeni
Mitomingi ndiye mimi.
MAMA: (Kwa
mshangao): Karibuni ndani mpumzike
MITOMINGI: Hatukai sana mama.
MAMA: Basi ngoja niwatolee viti make. (Aingia ndani na kutoka na viti viwili
kuwapatia wageni. Yeye aketi chini).
MITOMINGI: Mama!
MAMA: Baba!
MITOMINGI: Nadhani una habari juu ya kuhesabu watu.
MAMA: (Kwa mshangao): Kuhesabu watu?
MITOMINGI: Ndiyo kuhesabu watu.
MAMA: Kuhesabu watu! (Akitingisha kichwa) Hapana.
MITOMINGI: Balozi wenu hakuwajulisha?
MAMA: Hata kidogo.
MITOMINGI: Kweli?
MAMA: Kwani Tambitambi naye mtu yule!
Pombe na yeye ni
pete na chanda!
Hajali Balozi wake
wala nyumba yake.
MITOMINGI: Ni sawa usemayo mama. Tambitambi yule akili
hazimtoshi. Tumefika
kwake wala hajulikani
aliko!
MAMA: Kama kuna wanaume mabwege yule
ametia for a.
MITOMINGI: Usizidi kunambia mama, Tambitambi mambo yake
hakuna
asiyeyafahamu…. Sasa
mama!....
MAMA: Ndiyo baba.
MTOMINGI: Sisi kama utuonavyo tuko shughulini,
shughuli hiyo si nyingine bali hiyo
niliyoisema sasa hivi
kuhesabu watu. Na huyu kijana ndiye karani
mwenyewe ahusikaye.
Ingekuwa bora kama wewe na wanao wote
mngetoka nje ili
tufanye kazi yetu.
MAMA: Sasa baba mbona itakuwa vigumu.
MITOMINGI: Kwa vipi?
MAMA: Sasa baba utahesabu vipi?
MITOMINGI: Kwa nini?
MAMA: Kama utatuhesabu wewe basi u
mchawi.
MITOMINGI: Mbona sikuelewi!
MAMA: Mchawi ndiye anayehesabu watoto wa
wenzake ili awaroge. Sasa wewe
umchawi? Hata
kama u mchawi siwezi kukubali utuhesabui
maana
siwezi kujua nia
yako ni mbaya au nzuri.
MITOMINGI: Mtu akuwaniae uovu haji kweupe.
MAMA: Sawa usemayo baba.
NGOSWE: Sasa mama hebu walete wanao na yeyote
yule aliye ndani.
MAMA: Wanangu hawapo wamekwenda shamba
kuwania mpunga.
NGOSWE: Wote?
MAMA: Ndiyo.
NGOSWE: Ndio kusema hakuna kiumbe hata kimoja?
MAMA; Yuko mke mwenzangu.
NGOSWE; Tuitie.(Mama anasimama kwa unyonge na kuingia ndani. Anarudi peke
yake
baada ya muda mfupi). Yu wapi?
MAMA: Aja (Punde mama mwingine atokea. Yu kariby rika moja na mama wa
kwanza
isipokuwa huyu mbichimbichi).
MITOMINGI: Habari mama?
NGOSWE: (Wakati
huohuo) Shikamoo.
MAMA WA PILI: Nzuri (Atazama
chini kwa aibu huku akiketi).
NGOSWE: (Akimtazama mama wa kwanza).
Basi; hakuna mtu mwingine ndani?
MAMA WA PILI: (Akikataa
kwa kichwa)
MITOMINGI: (Kwa
mama wa kwanza). Lakini nyie wanawake mbona waoga sana!
Hivyo mnataka
kuniambia motto wa mgongoni anaweza kwenda
kuwania mpunga? (Mama agutuka). Hebu niambie mwanao
mchanga
yu wapi?
MAMA WA KWANZA: Sina mtoto mchanga.
MITOMINGI: Hivyo mama wasema kweli?
MAMA WA KWANZA: Haki vile.(Mara kwasikika sauti ya mtoto
akilia ndani ya
nyumba).
MITOMINGI: Na huyo anayelia kama si mtoto ni nini/ (Mama ainuka wakawaka na
kuingia ndani kwa aibu. Muda wapiti na harudi). Mama! Njoo basi
tumalize shughuli.
Usijali mambo ya motto kulia, ni jambo la kawaida.
(Mama atokea amepakata mtoto mchanga. Aketi
chini na sasa uso wake
umejaa hasira na chuki)…
[Imenukuliwa kutoka, Ngoswe, Penzi Kitovu
cha Uzembe. Uk 13-15]
2. Jadili hatua
za kuzingatia katika mchakato wa kutafsiri.
& Zoezi
la pili
1. Linganisha
na linganua kati ya taaluma ya tafsiri na ukalimani.
2. (a) Tafsiri sentensi zifuatazo kwenda lugha
ya Kiingereza
(i) Dua la kuku halimpati mwewe
(ii) Bandu bandu humaliza gogo
(iii) La kuvunda halina ubani
(iv) Mla vya watu naye vyake huliwa
(v) Akufaaye kwa dhiki ndiye rafiki wa kweli
(b) Ni njia
gani umetumia katika tafsiri ulizotoa hapo juu, unadhani ni kwa nini?
& Zoezi
la tatu
1. [a] Kwa
kutumia mifano, fafanua istilahi zifuatazo:
[i] Matini chanzi
[ii] Matini lengwa
[iii] Lugha chanzi
[iv] Lugha lengwa
[b] Tafsiri
sentensi zifuatazo kwenda lugha ya Kiswahili
(i) All that glister is not gold
(ii) Looser casn't be a chooser
(iii) When you make your bed you must lie on
it
(iv) There is no incense for something
rotting
(v) When in Rome do, do as Romans do
(b) Ni njia
gani umetumia katika tafsiri hizo ulizotoa hapo juu, unadhani ni kwanini?
2. "Mfasiri
au mkalimani hukabiliana na changamoto mbalimbali katika kufanikisha kazi
yake." Huku ukitumia mifano
thibitisha kauli hiyo.
MAREJEO
Cartford [1995]
A linguistic Theory Translation
Mwansoko, H.J.M na wenzake [2006] Kitangulizi cha Tafsiri, Nadharia na
Mbinu.TUKI.Dar-es-salaam
Newmark, P [1982] Approaches to Translation, Oxford, Pergamon Press
Newmark, P [1988] A Text book of
Translation, London, Prentice Hall.
Oxford University Press Dar-es-salaam
Semzaba, E [2006] Ngoswe, Penzi Kitovu cha Uzembe. The General Booksellers
LTD.
D.S.M
TUKI [2002] Kamusi ya Kiswahili Sanifu. TUKI, Dar-es-salaam
TUKI [1985] Kiswahili, Jarida la Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili.
www.bakita.org.tz retrieved on
Monday 04th July 2011
www.jim-mission.org.uk
retrieved on Monday, 04th July 2011
www.ajol.inf retrieved on Monday, 04th
July 2011
Vitabu vilivyotafsiriwa ambavyo
vimetumika kama marejeo
Ayi Kwei Armah, Wema Hawajazaliwa, kimetafsiriwa na Abdilatif Abdalla
Ferdinand Oyono: House boy, Kimetafsiriwa na Raphael Khasao na Nathan
Mwele.
William Shakespeare: Juliasi Kaizari: Kimetafsiria na Julius K. Nyerere
Mabepari wa Venisi: Kimetafsiriwa na Julius K. Nyerere
Hekaya za
Abunuwasi: Kimetafsiriwa na Interterritorial Language Committee, East Africa
Alfu Lela Ulela: Kimetafsiriwa na Sir Richard Burton
Sir Rider Haggard: Mashimo ya Mfalme Suleiman
Takadini,kimetafsiriwa na Mathews Bookstore and
Stationers,
Nitaolewa
Nikipenda ambacho kimetafsiriwa na
Crement M. Kabugi. vitabu vingine vilivyotafsiriwa ni kama vile; Orodha, Barua Ndefu Kama Hii n.k.
No comments:
Post a Comment