Wasema hawatapokea tena makapi ya CCM
Mkakati wa kuidhoofisha Chadema waanikwa
WAKATI Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, akisema kuwa chama chake sasa hakitawapokea na kuwapa nafasi za uongozi wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanaofukuzwa, mkakati wa kukivuruga chama chake umebainika, MTANZANIA Jumapili linaripoti.
Mbowe, wakati akitoa kauli hiyo jana mkoani Tabora, taarifa zilizolifikia gazeti hili zinaeleza kuwa mkakati unaodaiwa kuandaliwa na chama dola kukidhoofisha Chadema unaendelea kuratibiwa kwa karibu na ‘virusi’ (mashushu) waliopenyezwa ndani ya chama hicho na huenda yakaibuliwa mambo mengi zaidi yanayodaiwa kufanywa na chama hicho.
Aidha matukio yanayotokea bungeni, nguvu za dola kutumika kupita kiasi, uwepo wa ‘virusi’ ndani ya chama hicho ni miongoni mwa mambo yanayotajwa na baadhi ya maofisa wa ngazi za juu wa vyombo vya ulinzi na usalama kwamba chama hicho kinaandaliwa anguko.
Taarifa zilizolifikia gazeti hili zinaeleza kuwa mkakati wa kukidhoofisha Chadema ulianza tangu siku nyingi na unaratibiwa kwa ukaribu na ‘virusi’ wanaodaiwa kupenyezwa ndani ya chama hicho, ambacho katika siku za hivi karibuni kimepata uungwaji mkono mkubwa.
Inaelezwa kuwa kumekuwa na juhudi kubwa zinazofanywa na mahasimu wa Chadema kutaka kukidhoofisha chama hicho kupitia harakati zake za kisiasa, ambazo imekuwa ikizifanya kwenye mwanga na gizani.
Kwamba matukio ya sasa yanayotokea bungeni, wanachama wake kuundiwa kesi na hata kukamatwa kwa Mbunge wake wa Arusha Mjini, Godbless Lema, ni matokeo ya mkakati huo.
Inadaiwa kuwa mahasimu wa Chadema wamekuwa wakifanya juu chini kuhakikisha wanakibana chama hicho kuanzia bungeni, ambako imeonekana wazi kuwa umaarufu wa chama hicho kwa kiasi kikubwa umechangiwa na wabunge wake kuibana vilivyo serikali pindi wanapowasilisha hoja mbalimbali ndani ya vikao vya Bunge.
Tayari hali kama hiyo imeshuhudiwa Bungeni hivi karibuni, baada ya wabunge wake watano kusimamishwa kwa kukaidi kiti cha spika, wakati kiti hicho kikishindwa kuwachukulia hatua wabunge wa CCM wanaokwenda kinyume na kanuni zake.
Inaelezwa kuwa hatua hiyo ni mkakati wa kukifanya Chadema kishindwe kutekeleza majukumu yake sawa sawa.
Kuibuka kwa matukio ya wana Chadema wawili, mmoja akidaiwa kumrekodi mwingine wakidaiwa kupanga mikakati ya kutisha, nako kunaelezwa wazi kwamba chama hicho hakipo salama kama kinavyofikiri.
Hata hivyo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Azaveli Lwaitama, kwa upande wake anasema mizengwe inayofanywa dhidi ya Chadema si ya kukidhoofisha kama wanavyofikiri, bali ni kukipandisha juu chama hicho.
Akitolea mfano tukio la kukamatwa kwa Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema) Godbless Lema kwa tuhuma za kuchochea vurugu katika Chuo cha Uhasibu, Dk. Lwaitama alihoji mamlaka ya Mkuu wa Mkoa kumkamata mbunge aliyechaguliwa kwa kura za wananchi, akidai kuwa ni ya kipuuzi.
“Wenzetu wa Kenya wameshaondoka katika mfumo huu wa kipuuzi, eti mkuu wa mkoa ambaye hakuchaguliwa na wananchi anajipa mamlaka ya kumkamata mbunge aliyewekwa madarakani na wananchi..huu mimi nasema ni upuuzi,” alisema Dk Lwaitama.
Wakati hayo yakitokea, Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, amesema chama chake hakitawapokea na kuwapa nafasi za uongozi wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanaofukuzwa.
Amesema utaratibu wa awali wa kuwapokea na kuwapa nafasi za uongozi wanaCCM wanaofukuzwa au kujiondoa wenyewe kwenye chama hicho na kukimbilia Chadema, sasa umesitishwa.
Mbowe aliyasema hayo jana, katika mkutano wa ndani wa chama hicho uliofanyika kwenye ukumbi wa Chuo cha Ualimu, Tabora na kuhudhuriwa na makada wake wa Kanda ya Magharibi, inayojumuisha mikoa ya Kigoma, Katavi na Tabora.
Katika hotuba yake hiyo, alisema dhamira ya Chadema kwa sasa ni kukiimarisha na kukipatia viongozi walioandaliwa tofauti na vyama vingine vya kisiasa nchini.
Alitoa mfano wa viongozi wa CCM aliodai kuwa idadi kubwa ya viongozi wake wanapatikana kutokana na uwezo wao wa fedha badala ya ule wa kiuongozi.
Alisema Chadema inajipanga kuhakikisha viongozi wake kuanzia ngazi za chini wanawajibika na kuwatumikia wananchi na kuonya kuwa yeyote atakayebainika kutowajibika katika kutekeleza majukumu yake, chama hakitasita kumchukulia hatua kwa mujibu wa Katiba.
Akizungumzia lengo la kuanzishwa kwa Kanda za majimbo za chama hicho, alisema ni kuzidi kukijengea uwezo na kuimarisha utoaji wa huduma bora kwa wananchi, jambo ambalo limekuwa gumu kwa serikali ya CCM.
Aidha, Mbowe aliwaonya wabunge wa chama hicho kwa kueleza kuwa kuanzia sasa watapimwa kwa uwezo wao wa uongozi kutokana na utaratibu mpya wa kanda na namna wanavyotekeleza majukumu yao kwa kusaidiana kati ya mbunge na mbunge, ambao watakuwa katika kanda moja, licha ya kutofautiana majimbo.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe, ambaye aliambatana na Mbowe katika mkutano huo, alisema viongozi wa Chadema Kanda ya Magharibi wanapaswa kuwa tayari kujitolea kwa ajili ya chama chao.
Zitto alisema Chadema kinapita katika kipindi kigumu, hivyo viongozi wake wanapaswa kukiimarisha katika ngazi ya kanda ili kuwaenzi wote waliokipigania kwa muda wa miaka 22 ya uhai wake.
“Ndugu zangu wana kanda ya magharibi, viongozi wa Chadema na wanachama, katu msije kukubali mtu yeyote awagawe kwa misingi na malengo yake binafsi, kwani chama chetu sasa kina maadui wengi wasiokitakia mema,” alisema Zitto.
Aliwataka viongozi wenzake kuwa makini na watu ambao kila wakilala wanawaza kuiangamiza Chadema au kuipoteza kabisa katika siasa kwa kuwagonganisha viongozi wake.
Wakati huo huo, CHADEMA Mkoa wa Arusha kinakusudia kumshtaki mahakamani Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo.
Uamuzi huo umefikiwa siku mbili kabla ya Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema) kupandishwa kizimbani kesho kwa tuhuma za uchochezi katika Chuo cha Uhasibu Arusha.
Hata hivyo, wakati Lema akitarajiwa kufikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha kesho, taarifa kutoka ndani ya Chadema zimedai kuwepo kwa mpango wa kumbambikizia Mbunge Lema, kesi ya mauaji ya mwanafunzi wa Chuo cha Uhasibu Arusha, Henry Kago (22), aliyeuawa nje ya Chuo hicho.
Akizungumza jijini hapa jana, Katibu wa Chadema Mkoa wa Arusha, Amani Golugwa, alisema uamuzi wa kumfungulia kesi Mulongo umekuja baada ya kujiridhisha dhidi ya mwenendo wake wa kutaka kukidhoofisha chama hicho.
“Tunaendelea kukamilisha taratibu zetu, tayari tumewasiliana na wanasheria wetu juu ya hiki na wametuhakikishia kuwa ni lazima afikishwe mahakamani,” alisema Golugwa.
Alisema uchunguzi wao umebaini kwa kipindi kirefu Mulongo amekuwa akitumia lugha za kejeli, dharau na hata vitisho dhidi ya viongozi wa Chadema, jambo ambalo hawataendelea kulivumilia.
Golugwa alisema Mulongo amekuwa akimtuhumu Lema kwa mambo mbalimbali ya uongo kwa lengo la kumchafua na kumshughulikia.
“Kama tutapuuzia hali hii, ninaamini ipo siku itazidi zaidi ya hapa, kwani mbali na hili, pia tumepata taarifa za kumbambikizia kesi ya mauaji ya kule Uhasibu.”
Kwa upande wake, Wakili wa Lema, Humphrey Mtui, ambaye alizungumza na waandishi wa habari jana, alieleza kushangazwa na Jeshi la Polisi kumvunjia heshima mteja wake.
“Nimeshangaa hatua zilizochukuliwa dhidi ya mteja wangu, amechukuliwa kama mhalifu wa mtaani, wakati ana heshima mbele ya jamii na wapiga kura wa Jimbo la Arusha.
“Nimesikitishwa na hatua iliyochukuliwa kwa mteja wangu ya kunyimwa haki za msingi, kama kunywa chai na kuswaki, huu ndiyo utawala bora katika sheria hata kwa wahalifu?
“Mteja wangu alipaswa kuitwa polisi, kama angeendelea kukataa sheria ingechukua mkondo wake na si kufanya uamuzi wa kuvamia usiku nyumbani kwake,” alisema.
Wakati huo huo, baadhi ya wananchi wa Jiji la Arusha waliozungumza na MTANZANIA Jumapili jana walidai kuwa wanajipanga kufika kwa wingi katika viwanja vya Mahakama kwa ajili ya kumpokea kamanda wao kesho.
Chanzo: Gazeti la Mtanzania Jumapili