TAARIFA KWA UMMA
KUKAMATWA KWA MBUNGE WA ARUSHA MJINI MHE GODBLESS LEMA NA MASHTAKA YA UCHOCHEZI WA VURUGU ZILIZOTOKEA CHUO CHA UHASIBU ARUSHA.
Juzi usiku wa kuamkia tarehe 26 Aprili 2013, jeshi la polisi walifika nyumbani kwa Mhe Lema kwa lengo la kumkamata. Awali kufika kwao muda huo wa usiku wa manane kulileta mashaka kwenye familia ya mbunge mpaka ilipojiridhihirisha kuwa waliofika ni polisi kweli na sio wavamizi au majambazi. Katika kufika kwao polisi walikuwa wameweka tishio la kutaka kutumia nguvu usiku huo wa manane kwa kupiga mabomu na kuvunja nyumba iwapo mhe Lema asingefungua mlango na kujisalimisha kwa polisi. Walileta mbwa zaidi ya 15 na vikosi vya askari ambao waliizunguka nyumba wakiwa na mabomu na silaha nzito. Hata hivyo umati mkubwa sana wa watu yaani wapiga kura ulijitokeza, jambo ambalo liliashiria kuwa hatua zozote za nguvu ya polisi ingeweza kuzaa balaa ambalo lisingeweza kubebeka. Nguvu kubwa hii ya polisi yenye sura ya kuonyesha ubabe na uonevu imetufedhehesha sana na inatupa wasiwasi kuwa itakuja kusababisha hali ambayo sio nzuri siku si nyingi.
Mimi mwenyewe nilifika eneo la tukio muda huo, nilifanya mazungumzo ya kirefu sana na RPC kamanda Sabas pamoja na RCO kamanda Wambura. NIlizungumza pia na Mhe Lema na mawakili wetu juu ya jambo hili ndipo mida ya saa tisa usiku mhe Lema alifungua mlango na moja kwa moja tulielekea kituo cha polisi. Kwa mazingira ya muda wenyewe OCD aliagiza maelezo ya Mhe Lema yachukuliwe asubuhi ya siku ya terehe 26 Aprili.
Kuanzia saa nane mchana siku ya jana, ndipo jeshi la polisi walipoanza kumhoji Mhe Lema na chama tulimwomba wakili Humphrey kuwepo kwa ajili ya kumsaidia mhe Lema katika mahojiano hayo.
Mpaka sasa mhe Lema yupo mahabusu baada ya kunyimwa dhamana. Shitaka la msingi ambalo amefunguliwa ni la uchochezi (Shitaka namba 390) katika chuo cha uhasibu na kupelekea mkuu wa mkoa wa Arusha kuzomewa na wanachuo na hatimaye polisi kuanza kupiga mabomu hali iliyopelekea kufika hapo ilipofika.
Sasa vigezo vya shauri hili la uchochezi kwa mujibu wa mashtaka rasmi yaliyopo polisi limesababishwa na maneno yafuatayo ambayo inadaiwa mhe Lema aliyasema siku ya tukio hapo chuo cha uhasibu;
“Dhambi mbaya na kubwa kuliko zote duniani ni woga” na hivyo kuwataka wanachuo wasiwe waoga.
Wakati anaongea na wanachuo kuhusu ujio wa mkuu wa mkoa mhe mulongo ambaye alionekana kuchelewa, inadaiwa mhe Lema aliwaambia wanachuo, “NImepata taarifa kuwa ndani ya dakika 15 mkuu wa mkuu atafika, asipofika ndani ya muda huo nitawaongoza kwenda kudai haki yenu ya msingi ya kupatiwa ulinzi.
Baada ya mkuu wa mkoa kufika aligoma kuongea na wanachuo bila kuwa na kipaza sauti akataka PA system ifungwe ndio aweze kuongea, alipose,a maneno hayo wanafunzi wakaanza kuguna kuwa anaringa, mkuu wa mkoa akasema, kwa hali hii hataweza kuongea na wanafunzi wasio na adabu. Baada ya hapo mhe Lema akasema mbele ya wanachuo, “Hawa ndio viongozi wetu tunaowategemea wanakuja wanajivuta utafikiri wanakwenda kwenye send-off”?.
Katika kuchukuliwa maelezo yake mhe Lema amesisitiza kauli yake hiyo na kuwa hata mazingira ya namna ilivyotumika ni kauli njema kabisa.
Propaganda na upotoshwaji unaonezwa na mkuu wa mkoa kuwa mhe Lema alikimbia na kujificha na kwamba kwa nini alilitelekeza gari lake hapo chuoni na kwa nini hakuja polisi kulichukua gari lake ni kauli ya kufilisika sana kifikra na la kukosa mambo ya msingi ya kuongea. Baada ya vurugu hizi kutokea hata yeye mkuu wa mkoa alikimbia na kuondoka na gari yake, Mhe Lema alishindwa kulifikia gari lake kutokana na mabomu hayo, Mhe Lema alijikuta mwenyewe baada ya msaidizi wake kuzidiwa na moshi wa bomu liloanguka karibu yake akiwa katika jitihada za kumuokoa mhe Lema ambaye bomu lilikuwa limeelekea usawa wake, ndipo wanausalama watatu asiowafahamu walimficha na kisha walimtoa chuoni kwenye gari kwa utaratibu ambao haukuwa rasmi.
Ukweli, mkuu wa mkoa amelikoroga vibaya, hakuna mahali katika jambo hili lote Mhe Lema amewaambia wanachuo mzomeeni mkuu wa mkoa, hakuna mahali mhe Lema amewaambia wanachuo mtupieni chupa mkuu wa mkoa. Wote waliokuwep kwenye eneo la tukio wanashangaa na kujiuliza maswali mengi sana. Inashangaza kwa nini ajenda ya mauaji ya kutisha na kuhuzunisha na kilio cha wanachuo cha kudai kupatiwa ulinzi kimeyeyeyuka na sasa kila kitu ni Lema Lema!!
Mhe Lema amenyimwa dhamana na hivyo shauri hili litapelekwa mahakamani siku ya jumatatu ambako ndiko atakapopata dhamana.
Mhe Lema amenyimwa dhamana na hivyo shauri hili litapelekwa mahakamani siku ya jumatatu ambako ndiko atakapopata dhamana.
Mpaka sasa, hatujui aliyeleta malalamiko haya polisi ni nani ili kufungua mashataka dhidi ya Lema. Hata hivyo shitaka la uchochezi lina dhamana. Wakili wetu alipohoji na kuuliza kwa nini mhe Lema asipate dhamana maana ipo wazi kabisa kuwa ni shitaka lenye kuweza kupata dhamana alijibiwa hivi, “Ndio hivyo hatapata dhamana, ataipata jumatatu mahakamani”. Kauli hii aliisema Kamanda RCO Wambura akiwa na Kamanda RPC Sabas. Aidha wakili wetu alifedheheshwa na kauli hii ya kibabe kuwa, “unaliona kosa hili kuwa ni dogo lakini Lema ametufanya tumeshinda usiku kucha nyimbani kwake na mpaka sasa tupo hapa tumeacha familia zetu, atakaa ndani”. Nasi pia tumesikitishwa sana na kauli hii.
Makosa ambayo hayana dhamana (Capital offence) ni pamoja na kosa mauaji (Murder), Uhaini (Traeason), Ugaidi (Terrorism), Ubakaji, uhalifu kwa kutumia silaha na makosa mengine kama yalivyotajwa katika sheria zetu. Kosa hili lina dhamana lakini kuna mamlaka zimeamua kufanya ubabe ili kuonyesha umwamba. Hatuna ugomvi na jeshi la polisi, tunafahamu na tumetambua kiini cha tatizo kiko wapi. SISI TUTASHUGHULIKA NA KIINI.
Kama chama, tunaendelea na tafakari juu ya mambo yote haya. Tumeshawasiliana na mawakili wetu ambao kwenye kesi hii watakuwa mawakili wa kutosha kabisa kumtetea mhe Lema. Sambamba na hilo mawakili wetu wanaendelea na utaratibu wa kufungua kesi ya kumshtaki mkuu wa mkoa wa Arusha mhe Magesa mulongo kwa kosa la kumtishia kwa maneno makali mhe Lema na pia kutoa maneno ya uzushi, upotoshaji na uongo kwa jamii kuwa mauaji ya mwanachuo Henry Kago yalikuwa yamepangwa na wanasiasa ili kujipatia umaarufu.
Kwa ujumla jambo hili mpaka lilipofika hatua hii ya mashtaka kwa mhe Lema, limegubikwa na hila, ubabe na nia mbaya katika kulishughulikia. Hii inatupa mashaka makubwa kwamba, tutavumiliana kwa hali hii mpaka lini? Tutafumba macho na kuacha mambo yapite hivi hivi mpaka lini?
Tunaliomba jeshi la polisi lisikie kilio cha vijana hawa wa chuo cha uhasibu na waimarishe ulinzi kwenye maeneo ya makazi yao. Tuwaombe pia na uongozi wa chuo cha uhasibu kuharakisha mchakato wa kuwarudisha wanachuo hawa kuendelea na kumalizia masomo yao kwa mwaka wao huu wa masomo. Walikuwa na madai ya msingi sana, walihitaji kusikilizwa na sio kupigwa vimaneno ya vijembe na kufyatuliwa mabomu. Tunawaomba walimu wa chuo cha uhasibu wawe wakweli na waungwana sana kwa kueleza kile kilichotokea siku ya tukio na wasifanye kwa shinikizo lolote kupindisha ukweli.
Mwisho tunawaomba wakazi wa Arusha waendelee kuwa wapole na watulivu, wajue wazi kabisa hakuna hila itakayoshinda haki na ukweli. CHADEMA ni chama kikubwa na majaribu yetu ni makubwa sio ya kitoto, hata na hili tutashinda tu.
Nimalizie kwa kusema, “Dhambi mbaya na kubwa kuliko zote duniani ni woga”. Vitabu vya dini vinasema hivyo na sisi tunasema hivyo hivyo. Wakazi wa Arusha na Watanzania kwa ujumla, tusiogope kuitaja dhambi kuwa ni dhambi. Pasipo kuvunja sheria za nchi na pia bila kuathiri misingi ya kudumisha heshima kwa mamlaka zilizopo bado tunaweka wazi na kuwaambia na kusisitiza kuwa Watanzania tusiwe waoga.
Imetolewa leo tarehe 27 Aprili 2013
Amani Golugwa
KATIBU WA CHADEMA – KANDA YA KASKAZINI.
Amani Golugwa
KATIBU WA CHADEMA – KANDA YA KASKAZINI.
No comments:
Post a Comment