MGOGORO ndani ya Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM),
unazidi kupamba moto huku mikakati ya kumng’oa Mwenyekiti, Sadifa Juma Khamis na
Makamu wake, Mboni Mhita, ikizidi kuanikwa.
Mikakati hiyo inadaiwa kusukwa na kundi moja ndani ya CCM, ikihusishwa na
mbio za urais za mwaka 2015.
Uchunguzi wa Tanzania Daima, umebaini kuwapo kwa kundi ambalo Mwenyekiti wa
UVCCM, analituhumu kupanga mikakati mbalimbali ya kumng’oa katika nafasi hiyo
kwa masilahi binafsi.
Mwanzoni mwa wiki hii, gazeti hili liliripoti kuhusu kundi hilo linalotumia
sababu za kuwepo vitendo vya rushwa katika uchaguzi wa umoja huo uliopita pamoja
na madai kwamba mwenyekiti alighushi umri.
Kundi hilo linadaiwa kufadhiliwa na mmoja wa vigogo wa chama hicho wanaotajwa
kuusaka urais mwaka 2015 kwa udi na uvumba, ambaye pia ni mjumbe wa Halmashauri
Kuu ya CCM (NEC) mwenye uhusiano wa karibu na Mwenyekiti wa chama hicho, Jakaya
Kikwete.
Chanzo chetu ndani ya UVCCM kimedokeza kuwa mjumbe huyo ndiye analiwezesha
kundi hilo kifedha katika mkakati huo wa kutaka kumng’oa Sadifa kwa vile si
miongoni mwa wafuasi wake katika kuelekea mbio za urais za mwaka 2015.
Akizungumza na gazeti hili, Sadifa ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Donge,
alisema: “Kuna kundi la vijana wapatao kumi kutoka mikoa mbalimbali (majina
tunayo), wananifanyia fitina na kuniingilia katika utendaji wangu wa kazi za
kila siku kinyume cha katiba ya jumuiya yetu.
“Ninahisi kuwa kundi hili linasaidiwa na mtu mwenye nguvu au mwenye mamlaka
kwenye chama. Nasema hivyo kwa sababu sasa hii ni mara ya tatu,” alisema.
Sadifa alisema kwa mara ya kwanza baada ya uchaguzi wao uliofanyika mjini
Dodoma, watu hao walikuja na mabango kwenye mapokezi yake jijini Dar es Salaam
ofisi ndogo za chama Lumumba.
Alisema kuwa kundi hilo liliandaa watu wakafanya fujo hadi kupigana, na
kufikia hatua ya kutosalimiana sasa.
“Nimefika makao makuu juzi, nikakuta vijana watatu waliokuwepo hapo
nikawasalimia, lakini mwingine alitaka kunishambulia nikakimbilia ofisini kwa
Nape Nnauye,” alisema.
Wakizungumza na Tanzania Daima kwa nyakati tofauti kwa masharti ya kutotajwa
majina yao, baadhi ya wajumbe wa baraza hilo walisema: “UVCCM kuna tatizo tena
kubwa.” Kwamba kilichotokea na kinachotokea sasa ni mwenyekiti wao kushindwa
kujibu hoja.
“Tulihoji utaratibu aliotumia katika uteuzi wa makatibu kwenye jumuiya yetu,
akasema sisi tunataka kuchanganya mapenzi na kazi, kitu kilichozua malumbano
katika kikao chetu,” walisema.
Walidai kuwa kauli hiyo iliwaudhi na sasa hata kama hawana mpango wa
kumwondoa madarakani, atajiondoa mwenyewe kwa kushindwa kusimamia yale ambayo
aliahidi.
“Mwenyekiti wetu ni tatizo,” alisema mmoja wa wajumbe wa UVCCM huku akionesha
ujumbe mfupi wa simu ambao amewahi kutumiwa na mwenyekiti huyo.
Ujumbe huo ulisomeka: “Usinitumie sms za kipumbavu, wananena respect
yourself, if you can not respect yourself no body will respect you… ukianza
nitamaliza.”
Mjumbe huyo aliongeza kuwa, Sadifa alishinda kwa rushwa, kwamba kila mjumbe
alipewa kati ya sh 50,000 hadi 100,000 ili kufanikisha uchaguzi.
“Mwenyekiti wa chama alikuja akaonya kuhusu rushwa, lakini alipotoka tu,
miguu yake ikafutwa kwa kugawiwa sh 20,000 za haraka haraka kwa kila mjumbe,”
alisema.
Alipotafutwa mmoja wa wajumbe wa kundi linalotuhumiwa na mwenyekiti, alisema:
“UVCCM ni mbovu yote, si suala la taasisi, huu ndio msimamo wangu”.
“Mimi baada ya uchaguzi nilisimama ukumbini na niliwaambia wajumbe kuwa kama
kuna mtoto wa mnyonge au maskini aliyepokea rushwa ili kupiga kura, atakuwa
amepanda mbegu na kizazi chake kitavuna. Heri kuanguka kwa heshima kuliko
kushinda kwa fedheha,” alisema.
Alisema kuwa mwenyekiti wao ambaye kwa sasa anawatuhumu kwenye vyombo vya
habari anakosea. Kwamba hana haja ya kupiga kelele za rushwa, vijana wamesaini
wazi kumshtaki kuwa alishinda kwa rushwa.
“Mimi tangu uchaguzi wetu umalizike sijaongea, nakwambia siku nikiongea hata
ardhi itajua,” alisema.
Wajumbe wengine waliohusishwa na mkakati wa kumng’oa mwenyekiti walikuwa
wakali kila walipopigiwa simu na hata kufikia hatua ya kuzikata.
Katibu wa UVCCM, Martine Shigela, alisema jumuiya hiyo ipo imara, hakuna
tatizo na kwamba wiki ijayo watakaa na kamati ya utekelezaji
Chanzo: Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment