Yadaiwa ni mkakati wa CCM kuipora CHADEMA kata
TUKIO la kukamatwa na kuwekwa mahabusu kwa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless
Lema (CHADEMA), kwa madai ya uchochezi, limeibua sura mpya baada ya Chama Cha
Mapinduzi (CCM) kutajwa kuwa nyuma ya mkakati huo, Tanzania Daima Jumapili
limedokezwa.
Lema ambaye bado anaendelea kusota rumande siku ya tatu baada ya kunyimwa
dhamana, ameanza kufanyiwa vituko na Jeshi la Polisi baada ya jana asubuhi mkewe
kuzuiliwa asimpe mswaki wala chai.
Mbunge huyo alikamatwa kutokana na amri ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa
Mulongo, aliyedai kuwa aliwachochea wanafunzi wa Chuo cha Uhasibu Arusha
kumzomea kiongozi huyo na kupopoa gari lake kwa mawe.
Hata hivyo, siku moja kabla ya kukamatwa Lema aliwaonesha waandishi wa habari
ujumbe mfupi wa simu ya kiganjani aliyotumiwa na Mulongo akimtishia kuwa
atamfungulia kesi yoyote anayoitaka.
“Umeruka kihunzi cha kwanza, nitakuonesha kuwa mimi ni serikali, ulikojificha
nitakupata na nitakupa kesi ninayotaka mimi,’’ ulisomeka ujumbe huo uliotumwa
kupitia simu namba 0752 960276 ambayo Lema alidai ni ya Mulungo.
Pia nguvu kubwa iliyotumika kumkamata mbunge huyo usiku saa 5:30 kwa kutumia
askari na maofisa wa usalama kuzingira nyumba yake, imehojiwa na baadhi ya
wananchi, wakitilia shaka kuwa kuna siri ndani yake.
Madai ya Mulongo kuwa Lema alichochea wanafunzi hao yanakinzana na ushahidi
wa video unaoonesha kuwa mbunge huyo alitumia kila aina ya ushawishi kuwasihi
wasiandamane baada ya mwenzao, Elly Kago (22), kuuawa na watu wasiojulikana
jirani na chuo hicho.
Akizungumza na gazeti hili jana, mke wa Lema, Neema, alisema kuwa alifika
kituo cha polisi asubuhi akipeleka chai, lakini akaelezwa kuwa haruhusiwi
kumpelekea chai.
Alisema kuwa alipiga simu kwa mkuu wa upelelezi wa mkoa ndipo akaambiwa
ampelekee na alipofika tena kituoni askari aliyekuwa zamu alianza kupekua mfuko
wa Neema kwa fimbo, kisha akaamuru Lema apewe, ila anywe kwa dakika tatu.
Wakati anafungua chupa ya chai na kumimina kwenye kikombe, askari alimweleza
kuwa imebaki dakika moja, hatua iliyomuudhi Lema akidai ni udhalilishaji, hivyo
akashindwa kunywa.
Alipotaka kupewa mswaki, askari alikataa kuwa vifaa hivyo vinaweza kutumika
kama silaha, hivyo haruhusiwi kupewa.
Tanzania Daima Jumapili lilizungumza na wanasheria kadhaa pamoja na wanasiasa
wabobezi kuhusu sakata hilo, ambapo baadhi walidai huo ni mkakati wa CCM kutaka
kuidhoofisha CHADEMA katika uchaguzi mdogo wa madiwani ujao kwenye kata nne.
“Kesho mnaweza kusikia Lema akifunguliwa kesi ya ajabu ya kutunga halafu kwa
kipindi hiki kampeni zikianza mahakama itakuwa ikiisikiliza mfululizo ili
asipate nafasi ya kushiriki kikamilifu.
“Huu mkakati si wa Mulongo peke yake bali ni mbinu za CCM zilizobakia katika
kuhakikisha wanaikamata Arusha. Lakini naona kama wanazidi kujimaliza,” alisema
mwanasiasa mmoja aliyeomba kuhifadhiwa jina lake.
Mwanasiasa huyo kutoka mkoani Arusha aligusia pia mkanganyiko wa Tume ya
Taifa ya Uchaguzi (NEC) hivi karibuni kutangaza kata nne kurudia uchaguzi na
kuiacha moja ya Sombetini ambayo diwani wa CCM alihamia CHADEMA.
“Ujue CCM wanafanya mambo bila kupima athari, Arusha ni mji wa kitalii lakini
kwa sasa unaogopeka kwa fujo za polisi na wanasiasa, hata kesho utaona wakati
Lema akipelekwa mahakamani.
“Hapa ni ngome ya CHADEMA hata kama Lema hayupo, sasa NEC wameibana Sombetini
kwa hofu kuwa kata zote zikienda CHADEMA watakuwa na madiwani zaidi ya CCM,
hivyo ishu ya meya kufufuka upya, ndiyo wakaamua kumtumia Mulongo kufanya mchezo
huu wa hatari,” alisema.
Alipopigiwa simu jana jioni na kuulizwa juu ya madai hayo, Mulongo
alizungumza kwa ukali akisema: “Wewe mhariri unaweza kunipigia simu kuniuliza
swali kana hilo?”
Aliendelea kufoka akisema: “Acheni kufanya kila kitu siasa, wewe ni polisi
kujua Lema kwanini akamatwe hivyo, niache mimi niko na wageni wangu,” alisema na
kukata simu.
Mwenyekiti wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), Francis Stolla,
alizungumzia suala la kukamatwa kwa Lema akisema kuwa nguvu kubwa na utaratibu
uliotumika kumkamata haukuwa wa busara.
Stolla alisema: “Kwa mujibu wa kifungu cha 58 na 59 vya sheria ya ushahidi,
Jeshi la Polisi au hata kama ni kwa amri ya mkuu wa mkoa ya kukamata walipaswa
kuchagua njia nyingine ya busara.
“Jeshi linaweza kuwa na mamlaka mapana ya kukamata au hata kama ni kwa amri
ya mahakama, busara huhitajika kutumika. Lema ni mbunge, anafahamika na
upatikanaji wake hauna utata, anapotuhumiwa kuhitajika polisi busara inatumika
kumwita au kumwandikia aende, si kumvizia kama walivyofanya,” alisema.
Mwanasheria mwingine ambaye aliomba kuhifadhiwa jina, alifafanua kuwa: “Rais
peke yake ndiye Amiri Jeshi. Uamiri jeshi wa rais haugawanyiki mpaka kwa wakuu
wa mikoa.
“Uamiri jeshi wa rais upo kikatiba, hauwezi kuwa wa wakuu wa mikoa au wa
wilaya. Ndiyo maana anayeamrisha polisi katika mkoa ni Kamanda wa Polisi wa
Mkoa, na wilayani anakuwapo ofisa anayeamrisha (OCD),” alisema.
Aliongeza kuwa sheria zinaruhusu mkuu wa mkoa na wilaya kutoa amri ya
kukamata mtu kama hakuna askari lakini mtuhumiwa anapokamatwa sharti aambiwe
anakamatwa kwa kosa lipi na anayemkamata ajitambulishe.
Alisema kuwa siku ya tukio chuoni, polisi walikuwapo wakati Lema akizungumza
na wanafunzi na hawakuona kosa lolote kwake ndiyo maana hawakumkamata, sasa
iweje mkuu wa mkoa aje na amri.
Akizungumzia nguvu iliyotumika katika kumkamata Lema, Mwenyekiti wa Baraza la
Vijana CHADEMA (BAVICHA) Mkoa wa Tanga, Aaron Mashuve, aliliomba Jeshi la Polisi
kuelekeza nguvu kama hizo katika kusaidia watu wenye ulemavu wa ngozi
(albino).
Alisema nguvu hiyo kama ingetumika wauaji hao wangekuwa wamekamatwa badala ya
polisi kupoteza muda kuhangaika na wanasiasa ambao wanaweza hata kuitwa kituoni
wakaenda kwa hiari yao.
Katika hatua nyingine, CHADEMA mkoani Arusha kimetangaza kumfungulia mashtaka
mkuu wa mkoa huo kwa tuhuma za kumtishia mbunge wao kwa ujumbe wa maandishi, pia
kumtaka athibitishe madai ya kuwa kifo cha mwanafunzi kina uhusiano na masuala
ya kisiasa.
Katibu wa mkoa wa chama hicho, Amani Golugwa, alisema taratibu za
kuyashughulikia masuala hayo yote mawili zinaendelea chini ya jopo la wanasheria
wa chama hicho.
Chanzo: Tanzania Daima Jumapili
Picha imepakuliwa kutoka facebook
No comments:
Post a Comment