WAKATI wadau mbalimbali wa sekta ya habari wakifanya harakati za kuitaka serikali kubadilisha Sheria ya Magazeti ya Mwaka 1976, serikali juzi imeyafungia magazeti ya Mwananchi na Mtanzania.
Sheria ya Magazeti ya Mwaka 1976 inampa ruhusa waziri mwenye dhamana ya habari kupiga marufuku uchapaji na matumizi ya gazeti lolote ambalo anafikiri liko kinyume cha masilahi ya umma.
Gazeti la Mtanzania limefungiwa kwa siku 90, huku Mwananchi likifungiwa kwa siku 14, yote adhabu zao zimeanza juzi Septemba 27, 2013.
Uamuzi huo wa serikali umekuja mwaka mmoja baada ya kufanya hivyo kwa gazeti la Mwanahalisi ililolifungia kwa muda usiojulikana, kwa kuandika habari na makala ilizodai ni za uchochezi, uhasama na uzushi.
Taarifa iliyosambazwa kwa vyombo vya habari jana jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Idara ya Habari, Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Assah Mwambene, adhabu hiyo imeanza juzi.
Taarifa hiyo imebainisha kuwa magazeti hayo yamepewa adhabu hizo kutokana na mwenendo wa magazeti hayo kuandika habari na makala za uchochezi na uhasama, kwa nia ya kusababisha wananchi wakose imani kwa vyombo vya dola, hivyo kuhatarisha amani na mshikamano uliopo nchini.
Mwananchi
Mwambene alisema tangazo la kufungiwa kwa gazeti hilo limetangazwa kwa Tangazo la Serikali namba 333 la Septemba, 27, 2013.
Alisema Mwananchi limepewa adhabu hiyo kutokana na hivi karibuni kuchapisha habari zenye mwelekeo wa uchochezi na uvunjifu wa amani.
Taarifa hiyo iliongeza kuwa Julai, 17, 2013 katika toleo Namba 4774, lilichapisha habari isemayo: ‘Mishahara mipya serikalini 2013’, kwa kuchapisha waraka uliozuiliwa kwa matumizi ya vyombo vya habari, kwakuwa ulikuwa siri na haukupaswa kuchapishwa magazetini.
Alisema katika toleo la Jumamosi, la Agosti, 17, 2013 lilichapisha habari yenye kichwa kisemacho: ‘Waislamu wasali chini ya ulinzi mkali.”
Mwambene alisema habari hiyo ilikolezwa na picha ya mbwa mkali mwenye hasira, ambapo picha hiyo ilitoa tafsiri ya kuwa Jeshi la Polisi lilipeleka mbwa katika maeneo ya ibada ya waumini wa dini ya Kiislamu.
Alisema jambo hilo halikuwa la ukweli kwa sababu Jeshi la Polisi katika doria siku hiyo halikupeleka mbwa katika maeneo ya misikiti.
Alibainisha kuwa serikali na Jeshi la Polisi linaheshimu na kuzingatia maadili ya dini ya Kiislamu na haliwezi kupitisha au kuingiza mbwa katika maeneo ya ibada.
Aliongeza kuwa kuchapisha habari hiyo iliyokolezwa na picha ya mbwa ni uchochezi wa kulichonganisha Jeshi la Polisi na waumini wa dini ya Kiislamu. Mbwa ni najisi, hapaswi kuingia katika maeneo ya ibada.
Mwananchi wangoja barua
Akizungumza na Tanzania Daima Jumapili, Mhariri Mtendaji Mkuu wa Mwananchi, Bakari Machumu, alisema mpaka jana jioni hawakuwa wamepata barua hiyo na wanaisubiri ili waangalie hatua za kuchukua.
Machumu alisema wataijibu serikali kulingana na hoja walizowaandikia na hawatafanya hivyo kupitia tamko la Mkurugenzi wa Idara ya Habari alilolitoka katika mkutano wake na waandishi wa habari jana.
“Siwezi kukueleza hatua tutakazozichukua dhidi ya uamuzi wa serikali mpaka pale watakapotuandikia barua, mimi nimeona tamko lakini hawajatuletea barua rasmi,” alisema.
Kibano cha Mtanzania
Mwambene alisema Mtanzania limefungiwa kutochapishwa kwa kuchapisha habari zenye uchochezi na serikali inadai imeshalionya mara nyingi lirekebishe mtindo wake wa uandishi wa kichochezi na lizingatie maadili, sheria na kanuni za fani ya habari.
Alisema pamoja na kuonywa, gazeti hilo halikuonesha kuzingatia maelekezo ya Msajili wa Magazeti.
Mwambene alisema katika toleo Namba 7262 la Machi 20, 2013, liliandika habari yenye kichwa kisemacho: ‘Urais wa damu’.
Juni 12, 2013,toleo Namba 7344, lilichapisha makala isemayo: ‘Mapinduzi hayaepukiki.’
Alisema Septemba 18, 2013 katika toleo Namba 73414 ukurasa wa mbele lilichapisha kichwa cha habari kisemacho: ‘Serikali yanuka damu.’
Alibainisha kuwa taarifa hiyo ya serikali ilikolezwa na picha zilizounganishwa kwa ustadi mkubwa, kwa kutumia kompyuta kutapakaza rangi nyekundu mithili ya damu nyingi kumwagika.
Mwambene alisema katika habari hiyo gazeti hilo limedai bila uthibitisho kuwa Jeshi la Polisi linahusika na wahanga walioumizwa na watu wasiojulikana kwa kumwagiwa tindikali na waliovamiwa na kujeruhiwa vibaya.
Aliongeza kuwa gazeti hilo limeishutumu serikali kuwa goigoi katika kushughulikia matukio yenye sura ya kigaidi.
Mwambene alisema habari hiyo ni ya kichochezi na ina lengo la kuwafanya wananchi wavichukie vyombo vya ulinzi na usalama, wavione kuwa haviwasaidii.
Alibainisha kuwa kutokana na makosa yaliyotajwa hapo juu, serikali imelifungia gazeti la Mtanzania kutochapishwa kwa muda wa siku tisini (90) kwa Tangazo la Serikali Namba 332 la Septemba 27, 2013.
Mtanzania wang’aka
Mtendaji Mkuu wa New Habari 2006, Hussein Bashe, alisema uamuzi huo wa serikali si wa haki na si sahihi.
“Wamelifungia kimya kimya, tarehe 27, hatujaona barua wala hatujaitwa, hii inashangaza sana. Tumeiona katika mitandao, hii imetusikitisha. Hii ni taswira ya aina ya viongozi tulionao katika nchi hii, wizara hiyo hiyo naibu waziri wake alitutaka tuandike barua ya kuomba radhi kutokana na stori yetu, tulifanya hivyo. .. lakini leo mkurugenzi ametuandikia barua ya kutufungia,” alisema Bashe.
Bashe alisema adhabu hiyo inawapa funzo la kufanya kazi na aina ya viongozi na watendaji wa serikali wanaoamua mambo bila kuwahoji watuhumiwa.
“Nawaomba wenzangu tuungane kupambana na sheria hii kandamizi, la sivyo wataendelea kuitumia vibaya,” alisema.
Sheria ya Magazeti
Sheria ya Magazeti ya Mwaka 1976 inampa ruhusa waziri mwenye dhamana ya habari mamlaka makubwa ya kuweza kupiga marufuku uchapaji na matumizi ya gazeti lolote ambalo anafikiri liko kinyume cha masilahi ya umma.
Kwa vile sheria haitoi orodha halisi ya vigezo vya kutumika ili kupiga marufuku, inampa waziri hiari ambayo anaweza kuitumia bila sababu za msingi, ama hata kuitumia kwa sababu binafsi kunyamazisha magazeti yaliyo makini na uandishi wa habari za kitafiti. Katika sehemu ya pili ya sheria hii, kipengele cha 5(2), waziri anapewa mamlaka kama ya kutoa tangazo kupitia Gazeti la Serikali, kulizuia gazeti lolote kufanya kazi zihusianazo na baadhi ya vipengele ama vipengele vyote vya sehemu hii, aidha moja kwa moja ama kwa kuzingatia masharti ambayo waziri ataona yanafaa.
Katika mwelekeo huohuo, kipengele cha 25(1) cha sheria hiyohiyo kinampa waziri uwezo wa kupiga marufuku uchapaji wa gazeti lolote, wakati wowote atakaoona inafaa. Kipengele kinasema:
‘Pale waziri anapoona kwamba ni kwa masilahi ya umma, ama ni kwa masilahi ya amani na utulivu kufanya hivyo, anaweza, kwa kutoa agizo kupitia Gazeti la Serikali kuagiza kwamba gazeti lililotajwa katika agizo hilo liache kuchapwa tangu tarehe ile iliyoelezwa katika agizo.
Mamlaka hayo makubwa aliyonayo waziri yanaweza kutumiwa kinyume cha masilahi ya umma, tofauti na ilivyokusudiwa.
Wakitoa maoni yao kuhusu kufungiwa kwa magazeti hayo, Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Bara, Zitto Kabwe na Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa chama hicho, John Mnyika, wamelaani kitendo cha kufungiwa kwa magazeti ya Mwananchi na Mtanzania, wakisema ni dalili za utawala unaoanguka.
Walisema hayo walipokuwa wakihutubia mkutano wa hadhara eneo la Ugindoni, Kata ya Mji Mwema, Jimbo la Kigamboni. Wamewaomba wananchi kutokubali jambo hilo, kwani halikubaliki. Zitto alisema kwamba watawala wanaendelea kupata nguvu ya kuendelea kufungia vyombo vya habari kwa sababu ya ukimya wa wananchi.
“Wananchi mkichukua mamlaka yenu kama inavyosema Katiba ya nchi, chukueni mamlaka yenu hata mambo ya hovyo wanayofanya CCM bungeni yatakwisha. Leo nikiwa jukwaani hapa nimesikia magazeti ya Mwananchi na Mtanzania yamefungiwa, yaani watawala walipofungia MwanaHalisi na wananchi mkakubali kuwa kimya, wanaweza kufungia magazeti yote ili yaache kuripoti habari.
Via: Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment