KIJIJI cha Sasajila, kilichopo Wilaya ya Manyoni, Singida, hakina zahanati wala duka la dawa tangu kuanzishwa kwake miaka 37 iliyopita.
Diwani wa Viti Maalumu, Christina Ndahani, alibainisha hayo alipozungumza na Tanzania Daima katika kijiji hicho kilichopo Jimbo la Manyoni Mashariki.
Alisema wananchi wa eneo hilo hutumia zahanati ya Makasuku na Chibumwaga ambako hulazimika kutembea zaidi ya saa mbili ili kufika ama kutumia nyingine ya Mpandagani ambayo hutumia saa tatu.
Diwani huyo alieleza kuwa wananchi wanapolazimika kwenda hospitali kubwa ya Kilimatinde hutembea saa tano kwa mguu ili kufika na kupata huduma.
Alisema wanaoteseka zaidi ni wanawake wajawazito na watoto, kwani baadhi yao hufariki dunia njiani.
“Mwezi huu wanawake wawili walijifungua njiani, vifo vingi ni kutokana na hali hiyo. Kama wahisani watapatikana tukanyanyua saizi ya lenta katika jengo la zahanati itakuwa mkombozi mkubwa kwa kijiji, kwani serikali itaona na kuimalizia,” alisema diwani huyo.
Alieleza kuwa kutokana na kutokuwapo kwa zahanati katika kijiji hicho, baadhi ya wananchi hukimbilia kwa waganga wa jadi kupata matibabu, matokeo yake vifo vinaongezeka.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk. Parseko Kone alisema kutokana na agizo la Rais Jakaya Kikwete kuwa kila kijiji kiwe na zahanati, wamehamasisha wananchi kuanza michango kwa ajili hiyo, ili serikali nayo iunge mkono.
Chanzo: Tanzana Daima
No comments:
Post a Comment