CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema kuwa Balozi wa China nchini, Lu Youqing, amekiuka mkataba wa kimataifa wa Vienna kwa kuanza kushiriki kazi ya uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kama alivyoonekana akiwa mkoani Shinyanga.
Wakati CHADEMA ikitoa madai hayo, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa imekiri balozi huyo kuvunja mkataba huo unaoongoza uhusiano wa kidiplomasia na kuahidi kuchukua hatua.
Septemba 12 mwaka huu, balozi huyo alihudhuria mkutano wa hadhara wa CCM uliofanyika uwanja wa Shycom mkoani Shinyanga na baadaye katika eneo la mnada wa Mhunze Jimbo la Kishapu.
Balozi Youquing alitambulishwa kwa wananchi na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, na kisha kuwahutubia akisema China imevutiwa na sera za CCM na hivyo itawekeza katika soko la pamba katika mkoa huo.
Ni katika mkutano huo, balozi huyo alicheza nyimbo za CCM za kubeza vyama vya upinzani huku akiwa amevalia kofia ya chama hicho.
Akizunguza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa CHADEMA, Ezekia Wenje, alisema balozi huyo amekiuka mkataba wa kimataifa wa Vienna kuhusu mambo ya kidiplomasia kifungu cha 41 (i).
Alisema kifungu hicho kinakataza mabalozi wa nchi kujiingiza katika masuala ya ndani ya nchi nyingine.
Wenje alibainisha kuwa mkataba huo unataka kazi za balozi kuwa ni kuwakilisha nchi na si chama.
“Balozi wa China yuko hapa kuwakilisha China nchini Tanzania, si Chama cha Kikomunisti kwa CCM,” alisema.
Wenje aliongeza kuwa haamini kama huo ndio msimamo wa serikali ya China na pia CCM kwani Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe, alinukuliwa akiwaonya mabalozi kuingilia mambo ya ndani ya nchi kwa nyakati tofauti wanapokuwa wameongea na vyama vya upinzani.
Alisema kuwa CHADEMA imeazimia kuiandikia barua serikali ya China ili kuweza kupata msimamo wake kwa tabia ya balozi huyu kuandamana na chama kimoja na kutumia vifaa vyake vya uenezi katika mikutano ya hadhara.
Aliongeza kuwa wataiandikia pia serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kuomba ufafanuzi wa jambo hili na pia kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ambaye ndiye msimamizi halali wa mkataba wa Vienna.
Naye Mkurugenzi wa Bunge na Hamashauri wa CHADEMA, John Mrema, alisema tabia hiyo inahatarisha uhusiano wa China na Tanzania endapo CHADEMA au chama kingine kitaingia madarakani.
Mrema Aliongeza kuwa kitendo hicho kinaongeza mazingira hatari kwa wawekezaji wa Kichina waliopo nchini hasa kwenye maeneo ambayo CCM haikubaliki.
Mkurugenzi wa Mafunzo na Oganaizesheni, Benson Kigaila naye alisema kuwa wanawashangaa CCM kwa kuwa wanafanya mzaha na kila kitu.
“Wametumia wafanyakazi wa serikali katika siasa kwa muda mrefu bila mafanikio hadi wameanza kutumia mabalozi ili waweze kukubalika kwa wananchi,” alisema.
CCM wajitetea
Alipotafutwa Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC) Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema kuwa ziara ya balozi huyo mkoani Shinyanga haikuwa ya kisiasa bali ilitokana na mazungumzo kati ya chama hicho na Chama cha Kikomunisti cha China.
Alisema kuwa lengo lilikuwa ni China kuweza kuwekeza katika kilimo cha pamba na mifugo kuongeza ajira.
“Katika suala hilo CCM ilikuwa nyuma ya kuhamasisha wawekezaji, Katibu wetu alipokwenda China aliomba wawekezaj na watawekeza katika viwanda kumi na sasa wameanza na vitatu, ndio sababu Balozi wa China alienda kumwonyesha Kinana.
Nape aliongeza kuwa balozi huyo alipita katika mkutano wa hadhara na kuomba kusalimia wananchi kuelezea uwekezaji utakaofanywa na China.
“CHADEMA kulalamika ni kwamba wameweweseka kwa kuwa wamezoea kutumia matatizo ya wananchi kama mtaji wa kisiasa, tatizo la bei ya pamba likiendelea ni mtaji kwao na likiisha watakosa mtaji wa kisiasa,” alisema.
Wizara yacharuka
Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe, hakupokea simu yake kufafanua suala hilo lakini alipoandikiwa ujumbe na kupigiwa tena simu ilipokelewa na msaidizi wake ambaye aliahidi kutuma taarifa.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyotolewa na Togolani Mavura kwa niaba ya Waziri Membe ilisema kuwa imefuatilia suala hilo kwenye vyombo vya habari kuhusu kushiriki kwa Balozi wa China nchini kwenye mkutano wa hadhara wa CCM.
“Taarifa hizo zimeambatana na picha zinazomuonyesha balozi huyo akiwa amevaa kofia yenye nembo ya CCM. Habari zinaeleza kuwa alikwenda Shinyanga kuhudhuria uzinduzi wa mradi wa viwanda vya kuchambulia pamba vinavyojengwa na mwekezaji wa Kichina anayeitwa Tahong.”
“Viwanda hivyo vitakuwa na uwezo wa kuchambua tani 120,000 za pamba kwa mwaka, vitakapokamilika mwakani,” alisema.
Aliongeza kuwa wizara inapenda kutamka kwamba kitendo cha balozi yeyote kuhudhuria mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa na kuvaa sare zenye nembo ya vyama sio sahihi.
Ni kukiuka kifungu cha 41(1) cha mkataba wa Vienna wa mwaka 1961, unaoongoza uhusiano wa kidiplomasia.
“Katika kipindi cha mwaka 2010 hadi 2012 wizara ilikumbana na vitendo vinavyofanana na kitendo hiki na ikachukua hatua stahiki.
“Kadhalika kwa tukio hili, waziri anakusudia kuchukua hatua za kidiplomasia zinazostahili ili kuzuia jambo hili lisitokee tena,” alisema.
Via - Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment