SERIKALI imewakataza watumishi wake waandamizi wakiwemo wanaoongoza mashirika ya umma, wakala na taasisi zake kuwa viongozi ndani ya vyama vya wafanyakazi na kuonya kuwa, atakayekiuka agizo hilo atashushwa cheo au kuchukuliwa hatua nyingine za kinidhamu.
Kwa mujibu wa waraka wa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, wa Aprili mosi, mwaka huu, ambao hawapaswi kujiunga na vyama hivyo ni pamoja wakuu wa idara, vitengo, walimu wakuu (shule za msingi), wakuu wa shule za sekondari, wakuu wa vyuo na wakaguzi wa shule.
Sehemu ya waraka huo inasomeka; “Hairuhusiwi kwa mtu ambaye ameajiriwa katika taasisi za umma akiwa mwenye nyadhifa ya juu wakati huo huo awe kiongozi wa vyama vya wafanyakazi.”
Hata hivyo, wakati Balozi Ombeni akitoa maelezo hayo kupitia waraka huo, Kaimu Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Ezekiah Oluoch, amezungumzia suala hilo akisema, serikali inapingana na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara 20.
“Ibara ya 20 inatoa Uhuru wa mtu yeyote, kikundi chochote kujiunga ama kuunda na chama chochote kinachotetea imani, masilahi au mawazo yake ambayo ndivyo vitu vya msingi, “Katika huu waraka , nawazungumzia walimu wakuu, wakuu wa shule na wakaguzi wa shule . Hawa hawatungi sera, kuwaweka katika kifungu hiki ni makosa, sheria ya Bunge haipaswi kupingana na Katiba ambayo ndiyo sheria mama. Kwa hiyo sheria hiyo haiwahusu kwa kuwa wanaotunga sera ni makatibu wakuu na wakurugenzi kwa niaba ya serikali.
“Chini ya Sheria kuna kanuni ambayo haipaswi kupingana na sheria ya Bunge. Chini ya kanuni kuna nyaraka (miongozo). Waraka huu ni batili unapingana na kifungu cha 9 (6) (b) (i) (ii) cha sheria ya ajira na uhusiano kazini ya mwaka 2004.
“Waraka , pia unapingana na kifungu 30 na 31 vya sheria ya majadiliano ya pamoja kwenye utumishi wa umma ya mwaka 2003 kinachowataja wawakilishi wa vyama vya wafanyakazi kushiriki katika mabaraza ya wafanyakazi “Kanuni ya kudumu kifungu F.22 na 23 imezuia baadhi ya watu kuwa viongozi ndani ya vyama vya wafanyakazi ambacho pia ni batili kwa kuwa kinapingana na sheria ya Bunge.
Kutokana na kutofautiana huko kati ya Katibu Mkuu Kiongozi kupitia waraka wake huo na CWT, chama hicho cha walimu kimepanga kumuandikia Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) kumuarifu kwamba waraka ni batili na hivyo amshauri mtoa waraka aufute baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wanachama wao kudai kuingiliwa uhuru wao.
“Tumepokea barua kutoka kwa wanachama wanaolalamikia waraka huu kwamba kunaingilia uhuru wao. Baada ya kupata malalamiko hayo, tunayo haki ya kuupeleka mahakamani ikiwa Mwanasheria Mkuu hatamshauri mhusika kuufuta,” anaeleza kiongozi huyo wa CWT.
Katika hatua nyingine, Septemba 2013, CWT na Serikali vinatarajia kukutana kwa majadiliano ikielezwa kwamba matarajio ya chama hicho cha walimu ni kuwapo kwa ongezeko la mshahara angalau kwa kiwango cha asilimia 65.
Katika Afrika Mashariki imewahi kushuhudiwa walimu nchini Kenya wakishiinikiza serikali yao kuongeza mishahara ya walimu na katika kushinikiza mgomo wa siku kadhaa ulifanyika hadi serikali kukubaliana na walimu hao.
via: Raia Mwema
No comments:
Post a Comment