Blog ya kijanja kwa ajili ya watu wajanja

Blog ya kijanja kwa ajili ya watu wajanja

Sunday, September 1, 2013

HAWA NDIYO WANAOIVURUGA UVCCM

 
 
Lowassa, Membe waivuruga UVCCM
Mikakati ya kumng’oa Sadifa yasukwa
 
 
 

WANASIASA wanaotajwa kutaka kuwania urais mwaka 2015 kwa tiketi ya CCM, Edward Lowassa na Bernard Membe, wanadaiwa kuuvuruga Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM).

 
Tanzania Daima Jumapili, limedokezwa kuwa umoja huo umegawanyika katika makundi mawili, ambapo moja linamuunga mkono Lowassa na jingine Membe.


Inadaiwa uteuzi wa Katibu Mkuu mpya wa UVCCM, Sixtus Mapunda, uliofanyika wiki iliyopita umelenga kupunguza nguvu ya Lowassa kwenye umoja huo.


Sixtus aliteuliwa na Halmashauri Kuu (NEC) akirithi mikoba ya Martine Shigela, anayedaiwa kuwa upande wa Lowassa.


Wakati Mapunda akitarajiwa kuidhinishwa na Baraza la Umoja linalofanya kikao chake leo visiwani Zanzibar, tayari kumekuwa na minong’ono kuwa wadhifa huo amepewa ili kudhibiti kasi ya Lowassa ndani ya UVCCM.


Mapunda inadaiwa yupo katika kundi linalomuunga mkono Membe ndiyo maana baadhi ya vijana wanapinga uteuzi wake kwa madai utazidisha mpasuko ndani ya UVCCM.


Inadaiwa kuwa wakuu wa wilaya, Eribariki Kingu, Mrisho Gambo na Anthony Mtaka, mmoja wao alitarajiwa kumrithi Shigela aliyedumu kwenye nafasi hiyo kwa miaka mitano.


Tanzania Daima Jumapili limedokezwa kuwa kigogo mmoja ndani ya CCM tayari alishampigia simu mmoja wa wakuu hao wa wilaya akimtaarifu jina lake ndilo litakalopitishwa na NEC.


Inadaiwa jina hilo halikuweza kupenya katika vikao vya NEC kwa sababu kigogo mwingine alifanikiwa kuwashawishi wajumbe wampitishe Mapunda kwa madai hana makundi kama wakuu wa wilaya hao waliokuwa wakipigiwa chapuo.


Tanzania Daima Jumapili liliwasiliana na Mapunda, kuhusu uteuzi wake ambapo alisema ameteuliwa kuongeza umoja, mshikamano na ushirikiano.
Alibainisha kuwa wanaomhusisha na makundi wanafanya hivyo kwa lengo la kumpaka matope ili asitekeleze malengo ya kuuimarisha na kuuendeleza umoja huo.

“Kwa muda mrefu tumekuwa tukilumbana wenyewe kwa wenyewe, mimi nataka hali hii imalizike, nataka kuwaunganisha vijana, sitakubali tuvurugane,” alisema.

Tanzania Daima Jumapili limedokezwa kuwa baadhi ya wajumbe wa Baraza la UVCCM leo wamejipanga kumng’oa Sadifa kwa madai kuwa ameboronga katika wadhifa wake huo.

Sadifa alirithi kiti hicho kutoka kwa Hamad Masauni Yussuf, aliyelazimika kujiuzulu mwaka 2010, baada ya kukumbwa na kashfa ya kughushi cheti cha kuzaliwa kwa lengo la kudanganya umri.

Mmoja wa wajumbe wa Baraza la UVCCM (jina kapuni) alisema walitarajia Sadifa angeung’arisha umoja huo lakini amezalisha mizozo inayoizorotesha Jumuiya hiyo.

“Huyu ndugu yetu kaboronga sana, tunataka ang’oke ili tumtafute mtu mwingine, si kweli kuwa tunatumika na kundi la watu wanaotaka urais bali tunataka tusafishe UVCCM,” alisema.

Chanzo kimoja kutoka CCM kimelidokeza Tanzania Daima Jumapili kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Emmanuel Nchimbi, alikwenda visiwani Zanzibar kutuliza upepo wa kumng’oa Sadifa.

Nchimbi ambaye alishawahi kuwa Mwenyekiti wa UVCCM inaaminika ndiye kinara wa kutuliza mambo yanapochafuka ndani ya umoja huo.


Jitihada za Tanzania Daima Jumapili kuzungumza na Nchimbi, hazikuweza kuzaa matunda kwa kuwa muda mrefu simu yake ilikuwa ikiiita bila majibu.
Tanzania Daima Jumapili pia lilishindwa kuwasiliana na Sadifa kutokana na muda mrefu simu yake kuonesha ikiongea, hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa maneno (sms) hakujibu.
 
 
Chanzo: Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment