Wanamgambo wa al-Shabab wamedhibiti hali katika mji wa Barawe,
ambako makomando wa Marekani walijaribu kumkamata mmoja wa viongozi wa kundi
hilo mnamo Jumamosi.
Wenyeji wa mji huo wameambia BBC kuwa takriban makomando 200 waliojifunika
nyuso zao wamewasili mjini humo wakiwa na silaha nzito.
Inaarifiwa kuwa operesheni ya makomando hao ilikuwa inamlenga raia mmoja
msomali kwa jina Abdikadir Mohamed Abdikadir akijulikana kwa jina lengine kama
Ikrima.
Operesheni hiyo inafanyika baada ya shambulizi la kigaidi nchini Kenya mwezi
jana. Al-Shabab, ambayo ni tawi la al-Qaeda, imekiri kutekeleza shambulizi hilo
ambalo lilisababisha vifo vya watu 67.
Hata hivyo maafisa wa eneo hilo bado hawajathibitisha ambako operesheni hiyo
ya jumamosi iliyotibuka ilikofanyika
Siku hiyo hiyo majeshi ya Marekani yalimkamata kiongozi wa Al al-Qaeda Anas
al-Liby mjini Tripoli.
Anashukiwa kuongoza mashambulizi ya kigaidi dhidi ya balozi za Marekani
nchini Kenya na Tanzania mwaka 1998 .
Wenyeji wanasema kuwa Ikrima ni mmoja wa viongozi wa al-Shabab akiwa na
jukumu la kupanga mikakati ya kundi hilo na kuwa huwa amezingirwa na walinzi 20
walio na silaha nzito.
Mapema Jumamosi, wanajeshi wa Marekani waliwasili katika nyumba yake karibu
na bahari hindi ambako Ikrima hukaa mara kwa mara.
Walipokuwa wanaweka ngazi nje ya nyumba, mlinzi alitoa kilio kuhusu watu
kuingia katika eneo hilo na kusababisha ufyatulianaji wa risasi uliodumu kwa
dakika 20
Wanajeshi hao hata hivyo walirejea baharini na kuingia katika boti zao. Al-Shabab imesema kuwa mmoja wa wapiganaji wake aliuawa wakati wa
ukabilianaji huo wa risasi.
Mwandishi wa BBC Mohammed Moalimu anasema kuwa wenyeji sasa wanahofia kutumia
simu zao wasije wakadaiwa kuwa wapelelezi wa Marekani.
Al-Shabab imekuwa ikidhibiti eneo hilo tangu mwaka 2008. Walipoulizwa ikiwa serikali ilifahamu kuhusu uvamizi huo, serikali ilisema
kuwa ushirikiano wao na washirika wao wa kimataifa kupambana na ugaidi sio
siri.
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry alisema kuwa harakati dhidi ya
ugaidi nchini Libya na Somalia zilionyesha kuwa Marekani kamwe haitachoka
kuwachukulia hatua wanaofanya vitendo vya kigaidi.
Al-Shabab wamelazimia kutoroka miji mikubwa nchini Somalia kwa miaka miwili
iliyopita kufuatia operesheni za jeshi la Muungano wa Afrika ingawa bado
linadhibiti maeneo mengi ya mashinani.
Vi: bbc swahili
No comments:
Post a Comment