BARAZA la uongozi la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Kanda ya Kaskazini limemsimamisha uongozi Mwenyekiti wake wa Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba kwa tuhuma za kukisaliti chama hicho.
Uamuzi huo umefikiwa juzi katika kikao cha dharura cha baraza hilo baada ya mwenyekiti huyo akiwa ndani ya kikao kutuma ujumbe katika mtandao wa kijamii unaolenga kuwachonganisha viongozi na wanachama wa chama hicho.
Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari jana juu ya uamuzi huo, Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Kaskazini ambaye pia ni mbunge wa Karatu, Mchungaji Israeli Natse, alisema wameamua kuchukua uamuzi huo mgumu kutokana na tuhuma zinazomkabili Mwigamba na kuhitaji uchunguzi wa kina.
Natse alisema kuwa Mwigamba ametenda kosa hilo kupitia taarifa yake aliyotuma kupitia mtandao huo kwa jina la ‘Kwanini mabadiliko CHADEMA ni lazima’ na kusema kuwa viongozi wa chama wamechakachua katiba ili kuendelea kubaki madarakani.
Alitaja tuhuma hizo kuwa ni za usaliti, uzushi, uzandiki na uchonganishi kwa viongozi, ambazo zinahitaji uchunguzi makini, na hivyo kulazimu kumsimamisha wakati uchunguzi huo ukiendelea.
Kwa makosa hayo amekiuka Katiba ya CHADEMA sura ya 10 kuanzia kifungu cha 8, 9 na 10 ambavyo vinamzuia kiongozi kuchafua viongozi wenzake na wanachama kwa ujumla.
Alisema licha ya CHADEMA kuendesha uchunguzi, lakini pia uongozi wa Kanda ya Kaskazini ulimfikisha Mwigamba polisi kwa kutumia mtandao wa kijamii kukichafua chama hicho na viongozi wake ambapo ni kosa kisheria.
Naye Katibu wa CHADEMA wa kanda hiyo, Amani Golugwa, alisema baada ya kufikia uamuzi huo wanaandaa barua rasmi kumkabidhi Mwigamba, ikimaanisha kuwa amepoteza sifa ya kuingia katika vikao vyote alivyokuwa akiingia kupitia wadhifa wake wa uenyekiti.
“Tutakapomkabidhi barua inamaanisha kuwa anapoteza sifa ya kuingia katika vikao vya Baraza la Kanda kama mjumbe, vikao vya Baraza Kuu Taifa, Mkutano Mkuu Taifa na vingine vyote vya mkoa alivyokuwa akihudhuria kwa wadhifa wake wa uenyekiti,’’ alisema.
Kuhusu kumfikisha polisi, Golugwa alisema licha ya kumshitaki kwa tuhuma zinazomkabili, lakini ilikuwa ni kwa usalama wake kwa sababu chama kina wanachama wengi na kila mmoja ana hisia zake binafsi juu ya chama, hivyo ingeweza kuhatarisha usalama wake.
“Mimi kama katibu ambaye nimefanya kazi kwa karibu na Mwigamba akiwa mwenyekiti wangu wa mkoa, suala hili limeniumiza sana kwa kuwa sikutegemea kama angeweza kufanya alivyofanya,’’ alisema.
Alisema wakiwa katika kikao, walishangaa kuona ujumbe ukiingia katika mtandao wa kijamii na kushtushwa, hatua iliyowalazimu kufuatilia ili kumbaini aliyeutuma.
“Haikuwa rahisi kwake kukubali kuhusika kutuma ujumbe huo, na alitaka kuzua vurugu kikaoni, lakini baada ya kutakiwa kukabidhisha kompyuta mpakato ‘laptop’ na ilipokaguliwa kitaalamu na kupata uthibitisho ndipo alipobaki ameshangaa na kukiri kutenda kosa hilo,’’ alisema.
Aidha, tuhuma nyingine zilizotajwa ni kitendo chake cha kuwatuhumu mwenyekiti wa taifa na maofisa wengine wa chama kutumia fedha nyingi kuzunguka na kufanya vitu visivyo na msingi.
“Baada ya kutafakari hayo yote, chama kimeona hakiwezi kuendelea kuishi na mayai viza ama kulea mizoga kwa kuwa tunaamini amedanganywa na watu ambao hawalitakii mema taifa hili,” alisema Golugwa.
Via Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment