Blog ya kijanja kwa ajili ya watu wajanja

Blog ya kijanja kwa ajili ya watu wajanja

Monday, October 28, 2013

SHULE NYINGI ZA SEKONDARI ZA SERIKALI ZINANGOZWA NA WAKUU WA SHULE WASIOKUWA NA SIFA

Dar es Salaam. Wakati Serikali ikiendelea kuikalia ripoti ya Tume ya Kuchunguza Matokeo ya Kidato cha Nne iliyoundwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda mapema mwaka huu, baadhi ya wajumbe wake wameanika madudu mengi yaliyobainika katika uchunguzi huo.
 
 
Mmoja wa wajumbe waliounda Tume hiyo ameliambia gazeti hili hivi karibuni kuwa waligundua mambo mengi yanayodhihirisha udhaifu mkubwa katika uendeshaji wa sekta ya elimu nchini, ikiwa ni pamoja na kubaini kuwa idadi kubwa ya wakuu wa shule hawana elimu ya shahada.
 
 
Alieleza kuwa kiutaratibu mkuu wa shule anatakiwa kuwa na elimu isiyopungua shahada pamoja na mafunzo ya uongozi na usimamizi. “Kumbukumbu zilionyesha kuwa elimu ya sekondari ya kawaidaina jumla ya shule 4,528. Wakuu wa shule 1,498 wana shahada ya kwanza au zaidi, 1,703 wana stashahada, 33 wana sifa nyingine” alisema.
 
 
Sehemu kubwa ya matokeo ya uchunguzi huo inasemekana yamejikita zaidi katika kuzitupia lawama taasisi za Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) na Taasisi ya Elimu Tanzania (TIE).
 
Udhaifu wa kiutendaji kati ya taasisi hizo mbili unadaiwa umechangia kwa wanafunzi wengi kufanya vibaya kwenye mitihani ya kidato cha nne mwaka jana, kiasi cha kuilazimisha Serikali kuunda tume kuchunguza tatizo kutokana na kilio kikubwa cha wadau wa elimu na wananchi.
 
 
Matokeo hayo ya mtihani wa kidato cha nne uliofanyika mwaka jana yanaonyesha kuwa watahiniwa 240,903 sawa na asilimia 60.6 walipata sifuri, huku wanafunzi 23,520 tu ambao ni sawa na asilimia 5.16 ndiyo waliofaulu na wengine 103,327 sawa na asilimia 26.02 wakiwa wamepata daraja la nne.
Katika mtihani huo, watahiniwa 397,136 walikuwa wa shuleni na 68,806 wa kujitegemea.
 
 
Kutokana na hali hiyo, Waziri Mkuu Pinda aliamua kuunda Tume iliyoanza kufanya kazi kuanzia Machi hadi Juni mwaka huu. Tume hiyo iliyokuwa inaongozwa na Profesa Sifuni Mchome ilimkabidhi Waziri Mkuu ripoti Juni 15, mwaka huu.
 
 
Hata hivyo, ripoti hiyo haijawahi kutolewa hadharani baada ya Tume kumaliza kazi yake, huku Profesa Mchome ambaye alikuwa Katibu Mtendaji wa Taasisi ya Vyuo Vikuu Tanzania akipandishwa cheo na kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi.
 
Kauli ya Profesa Mchome 
Profesa Mchome alipotafutwa jana kuzungumzia kuhusu upatikanaji wa wakuu wa shule alisema, “Mimi hivi sasa ni katibu mkuu wa wizara siwezi kuzungumzia hilo, kwanza sijaiona hiyo ripoti. Ukitaka ufafanuzi mzuri mtafute Kamishna wa Elimu.”
 
Gazeti hili lilimtafuta kamishna huyo pamoja na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa, Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Philipo Mulugo bila mafanikio kwani simu zao zilikuwa zikiita bila majibu.
 
 
Akifafanua zaidi kuhusu viwango vya elimu, uzoefu na uwezo wa wakuu wa shule za sekondari mjumbe huyo alisema, “Mkuu wa shule anatakiwa achaguliwe kwa vigezo maalumu na apewe muda wa miaka mitano katika nafasi hiyo na kila baada ya miaka mitano apimwe utendaji wake kabla ya kumuongezea kipindi kingine.”
 
Alisema kuwa bado malengo ya sera ya kuwa na wakuu wa shule wenye kiwango cha shahada ya kwanza au zaidi haujafanikiwa.
 
“Hivi sasa kuna shule za sekondari 4,528 wakati rekodi zinaonyesha jumla ya wakuu wa shule ni 3,238 hivyo kuwa na tofauti ya shule 1,294. Wakuu wa shule wengi hawajaandaliwa katika fani ya utawala na hawapati mafunzo yenye tija ya kujenga umahiri wakiwa kazini” alisema na kuongeza;
“Baadhi yao kubaki wakiogelea na kufanikiwa kwa juhudi zao wenyewe. Kukosekana kwa utaratibu wa upimaji kwa wakuu wa shule za umma kumewafanya walimu hao kukosa motisha na hivyo kutojitahidi katika kuifanya shule yake kuwa ya kwanza au ya mfano katika elimu.”
 
 
Alisema kuwa utaratibu wa kuteua na kutokuwapima wakuu wa shule umekuwepo kwa muda mrefu tangu wakati idadi ya shule, wanafunzi na walimu ilipokuwa ndogo.
 
“Kwa hali ya sasa, kuna ongezeko la idadi ya shule, walimu na wanafunzi hivyo mkuu wa shule hawezi kuchaguliwa na kuachwa bila kujengewa umahiri na akategemewa kufaulu katika kazi yake” alisema.
 
 
Alisema kuwa vigezo vya kumchagua mkuu wa shule vitumike, wapimwe weledi wao kila mara na wapate motisha pale wanapofanya vizuri na kuleta maendeleo katika shule zao.
 
 
Alisema kuwa utaratibu wa kupata wakuu wa shule katika shule za binafsi na tofauti na shule za umma, kusisitiza kuwa sasa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) inatakiwa kuandaa na kutekeleza utaratibu wa kupima utendaji wa wakuu wa shule na taarifa za utendaji wao zijadiliwe katika vikao husika vya Halmashauri.
 
 
“Shule za Serikali za sekondari zinapata wakuu wa shule kutokana na mfumo wa uteuzi. Shule nyingi za binafsi hasa zile zinazofanya vizuri katika masomo na mitihani zina mifumo endelevu ya kumpata mwalimu mkuu,” alisema na kuongeza:
 
“Baadhi ya shule za binafsi pia bado hazina uwezo wa kupata Wakuu wa Shule kwa mfumo wa aina hii kwa sababu ya uwezo mdogo wa kulipa mishahara kwa Wakuu wa Shule wenye sifa za juu na wanaoleta matokeo yanayotarajiwa na mwajiri.”
 
Alisema kwa kiasi kikubwa sekta binafsi imekuwa ikiitegemea sekta ya umma katika kupata Wakuu wa Shule walio mahiri.
 
Alisema kutokana na mazingira kubadilika, ualimu mkuu sasa ni fani na siyo cheo tu, kwamba hauna kipindi maalumu na hivyo mtu anaweza kuwa mwalimu mkuu kwa muda wake wote wa ajira.
“Mfumo wa aina hii hautoi fursa ya ubunifu katika maendeleo ya shule. Shule nyingi za binafsi zinaendeshwa kwa misingi ya mkataba wakati za serikali zina mfumo wa ajira ya umma wa kudumu. Mifumo hii ni tofauti na inahitaji mifumo ya uwajibikaji tofauti” alisema
 
Alisema walimu katika sekta ya umma ni wengi na hivyo huhitaji umahiri mkubwa katika kuwasimamia, kuwaendeleza na kushughulikia masilahi yao kuliko kwenye sekta binafsi.
Alifafanua kwamba hali hiyo inatokana na shule binafsi kulipa mishahara mikubwa kuliko ya Serikali na hivyo walimu wa Serikali kuhamia huko kwa sababu ya tofauti katika masilahi.

Via: MCL

No comments:

Post a Comment