MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mkoa wa Arusha
ambaye amesimamishwa uongozi kwa tuhuma za usaliti, Samson Mwigamba, amesema
kuwa hakupigana na Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, Freeman Mbowe, kama
ilivyodaiwa na baadhi ya magazeti.
Mwigamba alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari
jijini hapa kuelezea kile kilichojiri mwishoni mwa wiki hadi akapigwa na baadhi
ya wajumbe wa kikao, wakimtuhumu kwamba aliandika taarifa za uongo kwenye
mtandao wa kijamii wa Jamii Forums akizungumzia masuala ya uongozi ndani ya
chama.
Mwigamba alisema kuwa hata wakati akivutana na walinzi wa chama Mbowe hakuwa
ndani ya chumba cha mkutano, hivyo akadai kuwa anashangazwa na wale waliosambaza
taarifa hizo kwamba alipigana na kiongozi huyo ambaye pia ni Mbunge wa Hai na
Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.
Aliwataja wale aliodai walimpiga kuwa ni Katibu wa Bavicha Wilaya ya Arusha,
Noel OLovaroya, walinzi wa chama pamoja na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless
Lema, kwamba alijaribu bila mafanikio kumpiga na kitofali ambapo alikikwepa kwa
kujiangusha chini na kujigonga kisogoni.
“Wakati vurugu zikianza Mbowe hakuwa ukumbini, nilimuona akija Lema na
Olevaroya, ambapo Lema alishikwa kabla hajanifikia huku Olevaroya akiruka juu ya
meza na kuja kunipiga ngumi, mimi kwa kujitetea ilibidi nimpige ngumi kabla
hatujaamuliwa,” alisema.
Mwigamba alimtuhumu Lema kuwa amekuwa akimtishia kumuua kwa kipindi kirefu,
ambapo siku ya tukio alirudia kauli hiyo kabla hajaenda kuchukua kitofali na
kujaribu kumpiga nacho ambapo alikikwepa.
Alisema kuwa tayari alishatoa taarifa polisi na kupewa kumbukumbu:
AR/RB/1759/2013 aliyoifungua Februari 12, mwaka huu, baada ya kuwa anapokea
vitisho vya kuuawa kutoka kwa Lema kupitia simu yake ya kiganjani.
Kuhusu kusimamishwa uongozi, Mwigamba alisema kuwa ametii licha ya kuwa kikao
kilichomsimamisha hakina mamlaka kisheria, huku akiweka wazi kuwa hayuko tayari
kukihama chama hicho, kwani bado anaamini ndicho chenye uwezo wa kuleta
mabadiliko nchini.
Hata hivyo, tuhuma za Mwigamba zilikanushwa na Katibu wa CHADEMA wa mkoa,
Amani Golugwa, akisema ni uongo dhidi ya Lema, kwani kwenye taarifa yake
aliyowasilisha juzi kwenye kikao cha uongozi wa kanda alimsifu mbunge huyo
kwamba ameongoza harakati mbalimbali za ujenzi wa chama kwa mafanikio makubwa,
zikiwamo kampeni za ushindi wa kata nne zilizofanya uchaguzi mdogo hivi
karibuni.
“Kwa kipindi chote ambacho amekuwa hayuko kazini Lema amekuwa akimsaidia hata
kukamilisha ujenzi wa nyumba yake maeneo ya Sokon 1, hata anavyokwenda kwenye
kesi zake Dar es Salaam ni Lema amekuwa akimsaidia gharama.
“Hicho alichokizungumza kwenye mkutano wake juu ya malalamiko ndiyo
anatudhihirishia kuwa amekuwa nyoka na mnafiki ndani ya kundi letu,” alifafanua
katibu huyo huku akisema hakuna malalamiko yoyote juu ya suala hilo ndani ya
chama.
Golugwa aliongeza kuwa baada ya kupitia kompyuta ya Mwigamba wamebaini mambo
mengi machafu na ya hatari kwa mustakabali wa chama ambayo yanawagusa watu
wengi.
Hata hivyo hakutaka kuingia kwa undani wala kuyafafanua akisema yatakisaidia
chama katika uchunguzi wake zaidi, na kwamba tayari kikao cha Baraza la mkoa
kimeshakaa na kimemwandikia Mwigamba barua ya ajieleze ni kwa nini asivuliwe
uongozi ikiwa ni sehemu ya mchakato wa kulifikisha suala hilo mbele ya kikao cha
Kamati Kuu ya Taifa.
Chanzo: Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment