Blog ya kijanja kwa ajili ya watu wajanja

Blog ya kijanja kwa ajili ya watu wajanja

Wednesday, October 9, 2013

MAANDAMANO YA UPINZANI YAIPA KIWEWE SERIKALI, SASA WAGEUKANA


MTIKISIKO mkubwa umeikumba serikali huku Rais Jakaya Kikwete akibanwa pande zote kutokana na mvutano mkubwa unaodaiwa kuibuka baina ya mawaziri na viongozi waandamizi wa CCM.

Habari za kuaminika kutoka ndani ya serikali na Chama Cha Mapinduzi, zimebainisha kuwapo kwa kutoelewana na kusukumiana lawama miongoni mwa watendaji wa serikali, kuhusu kile kilichoitwa ‘kusalitiwa’ kwa makubaliano yaliyofikiwa juu ya msimamo wa chama hicho, kuhusiana na suala zima la mabadiliko ya Katiba.

Katika msuguano huo, baadhi ya vigogo ndani ya CCM wamekaririwa wakisukuma lawama kwa Mwenyekiti wao, Rais Kikwete kwa kukubali haraka kusikiliza hoja za wapinzani huku akijua kuwa walifikia uamuzi wa pamoja kama chama na kukubali kupeleka muswada huo bungeni unaotokana na maoni ya wanachama.

Mmoja wa vigogo hao alikaririwa akisema Jumamosi ya wiki iliyopita kuwa hakutegemea kama Rais Kikwete angekiuka makubaliano hayo, kwa sababu yamewapa ‘kichwa’ viongozi wa vyama vya upinzani.
“Tumejimaliza wenyewe bila sababu. Hakukuwa na haja ya kurejea mazungumzo na hawa watu (wapinzani) kwa sababu, kila kitu kilitendeka kisheria na wao ndio waliosusia mjadala.

“Tunawakatisha tamaa wanachama wetu, na hawataweza kutuelewa wala kutupokea tena tutakapowaendea na jambo jingine, kwa sababu tunaamua hivi na kutenda vile,” alikaririwa akizungumza mmoja wa viongozi wa chama hicho katika mazungumzo yasiyo rasmi yaliyowakutanisha viongozi watano waandamizi katika moja ya hoteli za kitalii jijini Dar es Salaam.

Mbali na msuguano huo, baadhi ya watendaji wa serikali kwa upande wao wamesigana vikali, wengine wakiwasukumia lawama wenzao wanaodaiwa kutoa matamshi kuhusiana na madai ya wapinzani ya kutaka kuwepo meza ya mazungumzo.

Mawaziri, Stephen Wassira na Mathias Chikawe, walikaririwa hivi karibuni wakisema kuwa hakuna nafasi kwa Rais Kikwete kukutana na wapinzani katika jambo lililopitishwa kisheria na Bunge.

Wassira kwa upande wake alikwenda mbali zaidi na kutoa kauli ya kejeli kwamba, rais hana muda wa kukutana na wapinzani waliokuwa na hamu ya kwenda kunywa juisi Ikulu.

Mmoja wa mawaziri anayedaiwa kuchukizwa na kauli za watendaji wenzake, inadaiwa amekuwa akihaha kuwashawishi wenzake kumshauri Rais Kikwete awatimue ama awaombe mawaziri Wassira na Chikawe wajiuzulu ili kulinda heshima yao, ya serikali na chama kutokana na kauli zao.

Hata hivyo, kuna habari kuwa baadhi ya vigogo wa CCM wameanza kuingiwa hofu baada ya kuwapo taarifa za mipango ya kuungana kwa wapinzani katika Uchaguzi Mkuu ujao.

Hata hivyo, uchunguzi wa Tanzania Daima Jumatano umebaini kuwa hadi sasa hakujafanyika mazungumzo yenye mwelekeo wa kuungana kwa vyama hivyo katika suala la kumsimamisha mgombea mmoja wa urais ama kushirikiana na kuweka mtu mmoja katika nafasi za ubunge.

Msimamo wa wapinzani
Wakati hali ikiwa hivyo, Umoja wa Vyama vya Upinzani vya NCCR-Mageuzi, CUF na CHADEMA, umetangaza kusitisha maandamano ya kisiasa yaliyokuwa yafanyike kesho.

Kusitishwa kwa maandamano hayo kumetokana na kauli ya Rais Jakaya Kikwete kupitia vyombo mbalimbali vya habari kwamba atakutana nao kati ya Oktoba 13 au 15 ili kuzungumzia madai ya kasoro walizoziona kwenye Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2013 yaliyopitishwa bungeni hivi karibuni.

Lengo la maandamano hayo ilikuwa kumshinikiza Rais Kikwete asisaini marekebisho ya sheria hiyo iliyopitishwa na wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kuwa vipengele vingi vimewekwa kwa masilahi yao badala ya taifa.

Akitoa tamko hilo kwa waandishi wa habari kwa niaba ya wenyeviti wenzake, Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lupumba, alisema umoja huo kupitia Kamati yake ya Ufundi umesitisha maandamano hayo baada ya Ikulu kutoa taarifa kwamba ipo tayari kukutana nao.
“Tumesikia kupitia vyombo vya habari ambavyo navyo vimenukuu taarifa kutoka Ikulu kwamba Rais Kikwete amepanga kukutana na viongozi wa upinzani kuanzia Oktoba 13 hadi 15 ili kujadili na kupata muafaka wa suala la Katiba kwa vipengele tunavyovipinga.

“Tunaamini kuwa taarifa hizi ni sahihi kabisa, hivyo tumeamua kusitisha maandamano yetu yaliyolenga kushinikiza nguvu ya umma kuungana nasi katika kudai mchakato wa kuipata Katiba shirikishi na kushinikiza rais kutosaini kabisa muswada huo wa Katiba kwa kuwa una upungufu,” alisisitiza.

Alisema kutokana na nia aliyoionesha Rais Kikwete ya kulipatia ufumbuzi suala hilo, vyama hivyo havina budi kusitisha kwanza mchakato mzima wa maandamano na mikutano hiyo ya hadhara hadi pale mazungumzo na rais yatakapokamilika na kutoa dira ya kinachoendelea.

“Pamoja na kusitisha maandamano haya tunapendekeza huo mkutano ulioahidiwa na rais ufanyike mapema ili mchakato wa Katiba unaosuasua kwa sasa uendelee kwa ufanisi na kuwezesha kupatikana kwa Katiba iliyoandaliwa na Watanzania wote,” alisema.

Alisema madai ya umoja huo ni kuwapo kwa mchakato wa Katiba shirikishi, utakaoheshimu matakwa ya Watanzania wote wa Bara na Visiwani ili kuweza kupata Katiba iliyotengenezwa na wananchi wenyewe.
Hata hivyo, pamoja na umoja huo kuyasitisha maandamano hayo, tayari Jeshi la Polisi kupitia Kamanda wa Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alishayapiga marufuku, kwa madai kuwa yatasababisha usumbufu kwa wasafiri wengine na kupendekeza wafuasi wa vyama hivyo wakutane katika viwanja vya Jangwani bila maandamano.

No comments:

Post a Comment