SIKIA hii. Mrisho Ngassa alichukua pesa ya Simba kimya kimya, akavinjari mitaani na kupiga dili zake, siku zikasonga, maisha yakaenda ikafika siku akasaini mkataba mwingine na Yanga.
Hata hivyo, Shirikisho linalosimamia soka nchini (TFF) limemwamuru azirudishe fedha hizo alizochukua Simba pamoja na faini juu. Ngassa hakuwa na kinyongo, Ijumaa jioni iliyopita akiwa na begi lake akatinga ofisi za TFF kwenye Uwanja wa Karume, Dar es Salaam na kulipa kwa kutumia hundi ya Sh45 milioni.
Ngassa, ambaye amecheza mechi yake ya kwanza ya Yanga Jumamosi iliyopita dhidi ya Ruvu Shooting sasa ameibuka na kuwaomba mashabiki wa Yanga wenye nia njema wamchangie kuziba pengo alilonalo mfukoni kwa vile adhabu aliyopewa imemgharimu sana. Unajua Sh45 milioni si mchezo!
Mchezaji huyo ambaye amemaliza adhabu yake ya kutokucheza mechi sita ametamka maneno haya kwa huruma: “Nawaomba watu ambao wana nia ya dhati kunichangia niweze kurudisha fedha zangu kwenye namba yangu ya simu au akaunti yangu ya CRDB ambayo ni 01J2095037800.’’
Ngassa alidai kwamba fedha hizo alizilipa mwenyewe kutoka mfukoni kwake na sasa amebaki katika wakati mgumu ndiyo maana anaomba wasamaria wema kutoka Yanga kujipigapiga na kumchangia kitu kidogo kwenye akaunti yake hiyo na kwenye simu yake.
Katika hatua nyingine, mchezaji wa zamani wa Simba, Yusuph Macho ‘Musso’ alisema hakuna mchezaji mwenye rekodi ya kucheza misimu mingi kwenye ligi pasipo kuchuja kama Ngassa hatua ambayo amesema ni mchezaji bora wa Afrika Mashariki kwa sasa.
“Ni mchezaji ambaye ananishangaza kwa kasi yake uwanjani, amecheza ligi kwa misimu mingi lakini hajawahi kuchuja wala kasi yake kupungua kuanzia kwenye timu yake mpaka Taifa Stars, ni winga pekee kwa sasa Afrika Mashariki,” alisema Musso alipozungumza na Mwanaspoti mjini Dodoma.
No comments:
Post a Comment