Mahakama ya kimataifa ya ICC, imetoa kibali cha kukamatwa kwa
raia Mkenya ambaye anatuhumiwa kwa kujaribu kuwahonga mashahidi ili wajiondoe
kwenye kesi dhidi ya Naibu Rais wa Kenya William Ruto.
Viongozi wa mashtaka walisema kuwa mshukiwa huyo Walter Osapiri Barasa [Pichani]
ameshtakiwa kwa makosa matatu ikiwemo kutumia njia za ufisadi kumshawishi
shahidi mmoja na mkewe kwa kumlipa shilingi milioni 1.4 au dola 16,200, ili
wajiondoe kama mashahidi katika kesi hiyo.
Aidha mahakama inasema kuwa ni juu ya Kenya sasa kumkamata Barasa.
Kiongozi wa mashtaka Fatou Bensouda amesema kuwa ana ushahidi wa kutosha
kuonyesha njama ya Barasa kutaka kuwahonga mashahidi ili wajiondoe katika kesi
dhidi ya Ruto.
Bensouda amesema kuwa kuna mtandao wa watu wanaofanya kila wawezalo ili
kuporomosha kesi dhidi ya Ruto.
Lakini Barasa ameambia BBC kuwa yuko tayari kujitetea mbele ya mahakama hiyo
na kuonyesha kuwa hana hatia.
Naibu Rais Ruto na Rais Kenyatta wameshtakiwa kwa kupanga na kuongoza ghasia
za baada ya uchaguzi wa mwaka 2007 ambapo watu 1,200 walifariki.
Muda kuongezwa
Mahakama ya kimataifa ya ICC italazimika kuwa na vikao virefu zaidi vya
kusikiliza kesi dhidi ya Naibu rais wa Kenya William Ruto, kwa sababu ya muda
uliopotea kutokana na Ruto kurejea Kenya kwa dharura.
Jaji anayeongoza kesi hiyo Chile Eboe-Osuji pia alisema kuwa mahakama
itadurusu uwezekano wa kusikiliza kesi hiyo Jumatano siku ambayo wangepumzika
ili kuruhusu kesi nyengine kusikilizwa ndani ya chumba hicho.
"kama tunavyojua sote tumepoteza muda katika kesi hii kwa sababu ya matukio
ambayo hayangeweza kuepukika. Lazima tuweze kupata muda huo'', alisema jaji
huyo.
Kesi dhidi ya Ruto iliakhirishwa Septemba 23 kutokana na shambulizi la
kigaidi nchini Kenya ambalo liliwau watu zaidi ya sitini.
Hata hivyo jaji huyo alisisitiza kuwa kesi hiyo itaakhirishwa kwa muda ili
kutoa nafasi kwa kuanza kusikilizwa kwa kesi dhidi ya Rais Uhuru Kenyatta
Novemba tarehe 12 ambaye ni mshitakiwa mwenza wa William Ruto.
Kesi dhidi ya Ruto na mwenzake Joshua Sang, iliakhirishwa tarehe 23 Septemba,
wakati mahakama ilipomruhusu Ruto kurejea Nairobi kushughulikia shambulizi la
kigaidi la Westgate na athari zake.
BBC Swahili
No comments:
Post a Comment