Serikali ya Tanzania imesema inatafakari ushiriki wake ndani ya
Jumuiya ya Afrika Mashariki na inaweza kujitoa ndani ya Jumuiya hiyo iwapo
itaendelea kutengwa katika baadhi ya vikao.
Aidha imesema Tanzania haitambui vikao vinavyofanywa na nchi tatu zilizopo
ndani ya Jumuiya hiyo ambazo zimekuwa zikizitenga Tanzania na Burundi.
Waziri anayehusika na masuala ya Afrika Mashariki wa Tanzania Samwel Sitta
ameliambia Bunge la Tanzania kuwa makubaliano ya vikao hivyo vinavyofanywa na
nchi za Kenya, Rwanda na Uganda yatatekelezwa na nchi hizo zinazofanya vikao
hivyo kwa sababu vinafanyika nje ya utaratibu wa mkataba wa jumuiya hiyo.
Katika mikutano iliyofanyika hivi karibuni Tanzania na Burundi hazikualikwa
kwenye vikao hivyo.
Kwa mujibu wa Waziri Sitta mikutano ya wakuu wa nchi za Rwanda, Kenya na
Uganda ambayo ilianza kwa kuitenga Tanzania ilifanyika Entebbe nchini Uganda
mwezi Juni mwaka huu na kufuatiwa na mkutano wa pili uliofanyika Agosti mwaka
huu huko Mombasa nchini Kenya ambapo nchi hizo tatu bila kuishirikisha Tanzania
walizungumzia uanzishaji wa himaya moja ya forodha.
Mambo mengine waliyozungumza wakuu hao ilikuwa uanzishaji wa visa moja ya
utalii kwa nchi zao na matumizi ya vitambulisho vya uraia ambavyo vitatumika
kama hati za kusafiria miongoni mwa nchi hizo.
Aidha Waziri Sitta amesema ndani ya mikutano hiyo pia walizungumzia kuanzisha
mchakato wa kuanzisha shirikisho la nchi hizo.
Tayari Tanzania imeanza mazungumzo na nchi za Burundi na Jamhuri ya
Kidemokrasi ya Congo kuangalia ni kwa namna gani zitaanzisha ushirikiano nje ya
Jumuiya ya Afrika Mashariki kama zinavyofanya nchi za Rwanda, Uganda na
Kenya.
Via- bbc
No comments:
Post a Comment