WAZIRI wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, amesema Tanzania
itatoa talaka kwa nchi za Rwanda, Kenya na Uganda ambazo zimeamua kuanzisha
Jumuiya ya hiari nje ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Sitta alisema kutokana na nchi hizo kuonekana kuitenga Tanzania na Burundi
ambazo ni wanachama wa jumuiya hiyo, wameshaanza mazungumzo ya kushirikiana
kiuchumi, kisiasa na nchi za Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Congo
(DRC).
Kauli hiyo ya Sitta inatokana na mikutano ya mara kwa mara inayofanywa na
marais Uhuru Kenyata wa Kenya, Paul Kagame (Rwanda) na Yoweri Museveni (Uganda)
kuzungumzia masuala mbalimbali ya kushirikiana nje ya Jumuiya ya Afrika
Mashariki.
Waziri Sitta alibainisha msimamo wa Tanzania kutengwa na nchi hizo tatu jana
bungeni, alipokuwa akijibu maswali ya wabunge mbalimbali waliokuwa wakitaka
kujua kauli ya serikali juu ya vikao vinavyofanywa na marais hao watatu.
Mbunge wa Viti Maalumu Rukia Ahmed (CCM), aliitaka serikali ipeleke pendekezo
bungeni la kujitoa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki kabla haijapewa talaka
kutoka kwa Rwanda, Uganda na Kenya ambazo zimekuwa zikifanya mikutano
inayojadili masuala ya jumuiya bila kuihusisha serikali ya Tanzania.
Akijibu hoja hiyo Sitta, alisema ni mapema kwa Tanzania kupeleka bungeni hoja
ya kujitoa katika jumuiya hiyo kwa kuwa kinachofanywa na nchi hizo
kimeshafikishwa kwa Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa nchi wanachama ambaye
atakitolea ufafanuzi katika kikao kitakachofanyika wiki mbili zijazo.
Sitta alifafanua kauli ya Waziri mwenzake wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, Bernard Membe, hivi karibuni ya kwamba Tanzania inasubiri talaka
akisema yenyewe ndiyo yenye uwezo wa kutoa talaka kwa jumuiya hiyo kwa kuwa
inamiliki asilimia 52 ya eneo lote huku nchi zilizobakia zikigawana asilimia 48
iliyobakia.
“Hawa wenzetu wanafanya utoto wa kutuzunguka, sisi tunatumia hekima za mzee
Mwinyi aliyesema ‘mwongo, mwongoze’. Kama wao wana hila zozote juu yetu, siku si
nyingi tutazibaini, kama ni ndoa kwenye jumuiya basi sisi ndio tutakuwa
tumeoa…hivyo tutatoa talaka wakati wowote,” alisema.
Naye Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango Malecela (CCM), aliitaka serikali
isiendelee na hatua zozote kwenye jumuiya hiyo ambayo inaonekana kuelekea
kuvunjika.
Akijibu swali hilo, Sitta alisema serikali haijakaa kimya bali imeamua
kutoshiriki vikao vyote ambavyo nchi za Kenya, Rwanda na Uganda zitakuwa
zimeshayazungumzia masuala husika na kuamua kuwa na msimamo wa pamoja nje ya
jumuiya.
Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed (CUF), alihoji serikali inangoja utafiti
gani juu ya kutengwa kwao kiuchumi na nchi hizo tatu wakati Kenya wameshaingia
makubaliano ya kibiashara na Ethiopia na Sudan.
Katika jibu lake, Sitta alisema Tanzania imeshafanya mazungumzo na nchi za
DRC na Burundi kushirikiana katika nyanja mbalimbali.
Alisema kuwa DRC ndiyo yenye manufaa makubwa kiuchumi kwa Tanzania kuliko
Rwanda, Uganda, Kenya na Burundi kwa sababu mizigo mingi hutegemea bandari ya
Dar es Salaam.
“Burundi nao wanatengwa kama tunavyofanyiwa sisi, lakini tumeamua
kushirikiana kikamilifu na DRC pamoja na Burundi ambao tuna imani wana manufaa
makubwa kwetu,” alisema.
Hivi karibuni Tanzania iliingia kwenye mgogoro na Rwanda baada ya Rais Jakaya
Kikwete kutoa ushauri kwa Rais wa Rwanda, Kagame kuketi chini na waasi wa nchi
hiyo ili kuzungumzia masuala ya amani kwa nchi yao.
Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment