Blog ya kijanja kwa ajili ya watu wajanja

Blog ya kijanja kwa ajili ya watu wajanja

Saturday, October 5, 2013

LISSU AMJIBU KIKWETE, KUKAA MEZA MOJA WAPINZANI WAZIDI KUMBANA

NILIKUWA MBALI KIDOGO NASIKIA VIJANA MNANIITA SANA HAPA NA KUZUSHA MENGI.
KAMA KUNA KIJANA ANAFATILIA SIASA NA HAJAMUELEWA RAIS KIKWETE
HOJA KWA HOJA
AKAPATA  AKILI YA KUJUA UDHAIFU WA HOJA ZA  WALE JAMAA

BASI KIJANA HUYO NI MAJANGA.

maneno mengi ya nini???? soma hotuba Yake neno kwa neno.

mmekaa pazuri,mwaicheza vizuri midundo ya ngoma ya kimapinduzi.
MBONA 2015 MBALI, ALAFU CD ZIPO 10000,ATA MOJA HAIJESHA

TIME WILL TELL.

 Mchakato wa Katiba Mpya
Ndugu Wananchi;
          Kama mtakavyokumbuka, Bunge lilitunga Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Novemba, 2011.  Sheria hii imeweka mchakato mzima wa kupata Katiba hiyo na kuunda taasisi zake.  Mwezi Mei, 2012, Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliundwa na imekamilisha hatua tatu muhimu katika mchakato huo.  Hatua hizo ni kupokea maoni ya wananchi, kutayarisha rasimu ya kwanza ya Katiba Mpya na kupokea maoni ya Mabaraza ya Katiba ya Wilaya na ya taasisi.  Hivi sasa Tume inaandaa mapendekezo ya Rasimu ya Pili ya Katiba itakayopelekwa kwenye Bunge Maalum.  Baada ya tafakuri zake, Bunge Maalum litatoa rasimu ya mwisho ya Katiba ambayo itapelekwa kwa wananchi kwa ajili ya uamuzi wa mwisho kupitia kura ya maoni.  Baada ya hatua hiyo, ndipo tutakapokuwa tumepata Katiba Mpya.
Ndugu Wananchi;
Baada ya Bunge la Novemba, 2011 kupitisha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, kulikuwepo na madai ya kutaka sheria hiyo iboreshwe kutoka vyama vyote vya siasa vikiwemo vyama vya upinzani na Chama tawala.  Majadiliano yalifanyika baina ya Serikali na vyama hivyo pamoja na shirikisho la asasi za kiraia.  Makubaliano yalifikiwa kuwa marekebisho yafanyike kwa awamu.  Awamu ya kwanza ihusishe Tume ya Mabadiliko ya Katiba kisha hapo yafanyike marekebisho yanayohusu Bunge Maalum na mwisho Kura ya Maoni.
Kama ilivyokuwa kwa mabadiliko yaliyohusu Tume ya Mabadiliko ya Katiba, safari hii nayo vyama vya siasa vilitoa mapendekezo yao.  Yalifanyika mazungumzo kati yao na Serikali na maelewano kufikiwa kuhusu maeneo ya kufanyiwa marekebisho. Serikali ilitayarisha rasimu ya Muswada na kuuwasilisha kwa wenzetu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Ndugu Wananchi;
 Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ilitoa mapendekezo yake na ushauri kwenye maeneo mawili. Kwanza kwamba uteuzi wa wajumbe wa Bunge Maalum ufanywe na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushauriana na kuafikiana na Rais wa Zanzibar.  Pili walishauri kwamba kama Bunge Maalum litashindwa kufikia maamuzi ndani ya siku 70 zilizopendekezwa, liweze kuongezwa muda hadi kufikia siku 90.  Maeneo mengine ya Muswada waliafikiana nayo.
Ndugu Wananchi;
          Kwa kuzingatia utaratibu wa kutunga Sheria, Serikali ilifikisha Muswada kwa Spika wa Bunge ambaye nae aliuwasilisha kwenye Kamati ya Kudumu ya Katiba, Sheria na Utawala.  Kama ilivyo ada, Kamati hiyo ilifanya vikao na wadau na kupokea maoni yao kuhusu Muswada.  Nimeambiwa kulikuwa na mjadala wa kina na mapendekezo mazuri yalitolewa na wadau.  Kisha hapo Wajumbe wa Kamati walikaa wenyewe kujadili Muswada walikuwepo pia Wabunge ambao si Wajumbe wa Kamati walioshiriki kwa vile Kanuni zinaruhusu.  Nimeambiwa pia kwamba mjadala ulikuwa mpana na wa kina zaidi.  Mapendekezo kadhaa yalitolewa na Wajumbe kuhusu vifungu mbalimbali vya Muswada.
Ndugu Wananchi; 
Nimefahamishwa kuwa Wabunge wa vyama vyote walichangia na kwamba baadhi ya nyakati mambo yalipokuwa ugumu mawazo mazuri ya baadhi ya Wabunge wa upinzani yalisaidia kupata ufumbuzi.  Nimeambiwa pia kwamba Wajumbe wa Kamati na upande wa Serikali walikubaliana kwa maeneo mengi isipokuwa machache ambayo walikubaliana kwa pamoja wayapeleke Bungeni ili Wabunge nao wayajadili na kuyapatia ufumbuzi. 
Ndugu Wananchi;
          Baada ya Kamati kumaliza kazi yake, Waziri wa Katiba na Sheria, Mheshimiwa Mathias Chikawe aliwasilisha Muswada Bungeni.  Akafuatiwa na Mheshimiwa Gosbert Blandes kwa niaba ya Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala, kutoa maoni ya Kamati. Baadaye Msemaji wa Kambi ya Upinzani, Mheshimiwa Tundu Lissu  alitoa maoni yake. 
Ndugu Zangu;
Baada ya watu hao watatu kutoa maoni yao ilitarajiwa kuwa Wabunge wangeanza kujadili Muswada.  Naambiwa mambo hayakuwa hivyo.  Badala yake kukazuka malumbano baina ya Spika na baadhi ya Wabunge wa Upinzani wakitaka Muswada usijadiliwe.  Ilifikia wakati hoja hiyo ikabidi iamuliwe kwa kura ambapo ilishindwa.  Katika hali isiyotarajiwa, Wabunge wote wa upinzani wakatoka nje ya Bunge isipokuwa wawili.  Kitendo hicho kimewanyima Wabunge wengi wa upinzani fursa ya kutetea hoja zao walizozitoa kupitia hotuba ya Msemaji wa Kambi ya Upinzani.  Pia wamejinyima nafasi ya kusema mambo mengine wakati wa mjadala na Kamati ya Bunge zima.
Wabunge waliokuwepo waliendelea kuujadili Muswada na kutoa hoja na mapendekezo ya kuuboresha.  Walifanya hivyo wakati wa mjadala na wakati wa kupitia kifungu kwa kifungu.  Baadhi ya hoja na mapendekezo yalikubaliwa na mengine yalikataliwa.  Miongoni mwa yaliyokubaliwa na Wabunge, kwa mfano, ni kuhusu elimu ya mtu atakayekuwa Mwenyekiti wa Bunge Maalum na lile la ukomo wa uhai wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Ndugu Wananchi;
Kwa maoni yangu madai ya Kambi ya Upinzani yanazungumzika na hata baadhi yangeweza kukubalika kama Wabunge wake wangekuwepo Bungeni na kushiriki mchakato wote wa kujadili na kupitisha Miswada Bungeni.  Bahati mbaya hawakuwepo, hivyo hapakuwepo na mtu wa kusema mawazo yao.  Baada ya kupoteza fursa yao halali, kutaka kupata ufumbuzi nje ya Bunge ni jambo lisilowezekana.  Haya ni masuala yanayohusu Bunge ambayo hujadiliwa na kuamuliwa Bungeni na si vinginevyo.  Kuandamana nchi nzima au kuchukua hatua za kutotii sheria kama Mwenyekiti wa CHADEMA, Mheshimiwa Freeman Mbowe anavyotaka, hakutaleta mabadiliko wanayoyataka katika sheria hii. Naamini na wao wanautambua ukweli huo. 
Ndugu Wananchi;
Kuna msemo wa wahenga kuwa “historia hujirudia”.  Naomba hekima ziwaongoze viongozi wa CHADEMA, CUF na NCCR-Mageuzi na zituongoze sote kutumia utaratibu tulioutumia mwaka 2012.  Kulipotokea mazingira kama haya pande zote zilikaa pamoja na kuzungumzia hoja moja baada ya nyingine na kukubaliana nini kifanyike na kifanyike vipi.  Baada ya kuridhiana hatua zipasazo za kisheria na kanuni zilichukuliwa na kumaliza mzozo.
Ndugu Wananchi;
Kufanya kinyume cha hayo hakutaleta ufumbuzi wa mzozo huu.  Tutaliingiza taifa kwenye matatizo yasiyokuwa ya lazima.  Tukikataa kufanya hayo Watanzania wanayo kila sababu ya kuhoji dhamira zetu na kutilia shaka nia zetu.  Watakuwa na haki ya kuuliza nia ni hii yetu sote ya kupata Katiba Mpya kwa kutumia njia za kikatiba na kisheria au tuna dhamira nyingine iliyojificha? 
Kama dhamira yetu ni kutaka kupata Katiba mpya kwa mujibu wa Katiba na Sheria, ushauri wangu na rai kwa ndugu zetu wa CHADEMA, CUF na NCCR-Maguezi ni kuwa waachane na mipango ya maandamano na kufanya ghasia.  Badala yake watumie njia halali zinazotambulika kikatiba na kisheria kujenga hoja za kufanya marekebisho wanayoyaona wao yanafaa kuboresha Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.  Tukifanya hivyo tutakuwa tunajenga badala ya kubomoa.  Tutaliponya taifa.  Sisi katika Serikali tuko tayari.
Ndugu Wananchi;
Napenda pia kuzisemea baadhi ya hoja zilizotolewa na Kambi ya Upinzani.   Kwanza kabisa nasema kuwa nimesikitishwa sana na madai na tuhuma za uongo eti katika uteuzi wa Tume ya Katiba sikuheshimu mapendekezo ya TEC, CCT na walemavu.    
Ndugu Zangu, Watanzania Wenzangu;
Siyo tu kauli hiyo ya Mheshimiwa Tundu Lissu ni uzushi na uongo mtupu bali pia ni ya unafiki, fitina na uzandiki wa hali ya juu.  Nasema hivyo kwa sababu, sipendi kuamini kuwa Mheshimiwa Mbunge amesema yale kwa kutokufahamu ukweli au kwa bahati mbaya.  Amesema yale kwa makusudi mazima ya kupotosha ukweli ili pengine isaidie kujenga hoja yake ya kutaka Rais asiteue wale Wajumbe 166 wa Bunge Maalum.  
Napenda ieleweke kuwa siishabikii kazi hiyo, lakini kwa kutimiza wajibu na maslahi ya taifa nikiagizwa na Sheria za nchi nitafanya.  Nasema hivyo kwa sababu nafahamu ni kazi ngumu.  Kama kazi ya uteuzi wa Wajumbe 30 wa Tume haikuwa rahisi hata kidogo, hii ya uteuzi wa watu 166 itakuwa ngumu zaidi.  Ile ya Tume ilikuwa ngumu kwa namna mbili.  Kwanza, kwamba taasisi zilizoomba na waombaji walikuwa wengi mno kuliko nafasi za kujaza yaani 15 Zanzibar na 15 Bara.  Zanzibar ziliomba taasisi zaidi ya 60 na waombaji walikuwa zaidi ya 200 wakati Bara kulikuwa na taasisi zaidi ya 170 zikiwa na waombaji zaidi ya 500.  Kupata watu 30 kutoka orodha kubwa kiasi hicho si mtihani mdogo.  Pili kwamba tulitakiwa kuunda Tume inayoasili sura ya taifa, yaani watu wa nchi yetu kwa maeneo, vyama vya siasa, dini, wanawake, vijana, walemavu, wafanyakazi, wasomi, Wabunge, Wawakilishi, wanasheria, wafanyabiashara, wakulima, asasi za kiraia n.k.
Ndugu Wananchi;
Pamoja na changamoto hizo, lakini tulifanikiwa kuunda Tume iliyopokelewa vizuri na jamii na kufanya watu wengi hata wale ambao hawakuteuliwa wahisi kuwakilishwa.  Tulifanyaje? Kwanza kabisa tulihakikisha kuwa tunapata wawakilishi wa vyama vya siasa vyenye wawakilishi Bungeni na kwenye Baraza la Wawakilishi na tunapata wawakilishi wa mashirika ya dini zetu kubwa yaani, TEC, CCT na BAKWATA.    Ndiyo maana nikasema kuwa kwa Mheshimiwa Tundu Lisu kudai kuwa mapendekezo ya TEC na CCT hayakuheshimiwa ni uongo wa mchana usiokuwa na kichwa wala miguu.
Baada ya hapo ndipo tukaangalia waombaji wa makundi na taasisi nyingine.   Tulijitahidi sana kupata watu ambao wanawakilisha kundi zaidi ya moja.  Tulifikiria hivyo kwa sababu ni ukweli ulio wazi kuwa si kila taasisi iliyoomba itapata mwakilishi kwani hata tungependa iwe hivyo nafasi hazikuwepo.  Kwa kutumia utaratibu huu makundi mengi yamepata uwakilishi kutokana na watu waliopendekezwa na makundi mengi.  Tumefanya kazi kubwa sana ya kuwianisha mambo na makundi ya maslahi mbalimbali nchini. 
          Ndiyo maana naiona mantiki ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akishirikiana na Rais wa Zanzibar wa kuwateua Wajumbe wa Bunge Maalum.  Dhana kuwa kila kikundi kiteue chenyewe watu ingefaa sana kama kungekuwepo na nafasi za kutosha kila kundi nchini.  Hilo haliwezekani, labda tuwe na Bunge Maalum lisilokuwa na ukomo wa wajumbe.
Ndugu Wananchi;
Mimi na Rais wa Zanzibar tumekuwa tunajiuliza baada ya kazi ngumu na nzuri tuliyoifanya na iliyopongezwa na wengi ya kuteua Tume ya Mabadiliko ya Katiba nini kilichoharibika sasa hata tuonekane hatuaminiki kuteua hawa 166?  Kama ni kwa sababu za Mheshimiwa Tundu Lissu, nimeshasema hazina ukweli wowote.  Ninapojiuliza kwa nini aseme uongo nashindwa kupata jibu linaloingia akilini.  Wakati mwingine nafikiria kuwa ni hiana.  Lakini nadhani ni hila za kisiasa zenye nia ya kutaka kupata watu wa kutetea maslahi ya chama chake.  Kama hiyo ndiyo shabaha basi amekosea sana. 
Ndugu Zangu, Watanzania Wenzangu;
Hatutengenezi Katiba ya Chama fulani bali Katiba ya nchi, Katiba ya watu wa vyama vyote na wasiokuwa na vyama ambao ndiyo wengi kuliko wote.  Lazima tuongozwe na ukweli huo na tuwe na msimamo huo wakati wote.  Lazima tukumbuke kuwa si watu wote wanaostahili au kuwa na sifa ambao wataomba na kupata nafasi ya kuwa Wajumbe, hivyo wale wachache watakao bahatika lazima wawasemee wote.  Wanatakiwa kusikiliza na kuwakilisha mawazo ya wote hata wale wasiokuwa wa Chama chao au kundi lao. 
Ndugu Wananchi;
Bahati nzuri hii ndiyo sifa kubwa iliyooneshwa na Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.  Wamewasimamia na kuwasemea watu wote bila ya kubagua.  Natambua kuwepo kwa baadhi ya watu ambao hawafurahii msimamo huo na matokeo ya kazi yao.  Watu hao kuwalaumu Wajumbe wa Tume kwa ajili hiyo ni kuwaonea na kutowatendea haki.  Tunataka watakaokuwa Wajumbe wa Bunge Maalum nao waige mfano huu mzuri.  Wajali maslahi mapana ya taifa letu na watu wake badala ya kujali yale ya taasisi zao au makundi yao.
Zanzibar Kutokushirikishwa
Ndugu Wanachi;
Nimeambiwa pia kuliwepo madai ya Zanzibar kutokushirikishwa ipasavyo.  Nimeeleza kwa kiasi gani Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeshirikishwa na kutoa maoni yake yaliyojumuishwa katika Muswada.  Hivyo basi napata tabu kuyaelewa madai kwamba Serikali ya Mapinduzi Zanzibar haikushirikishwa msingi wake nini!  Labda kuna kitu sikuambiwa! 
Nimeulizia kuhusu hoja ya Kamati kutokufanya vikao Zanzibar kusikiliza maoni ya wadau wa Zanzibar.  Nimeambiwa kuwa Kanuni za Bunge hazina sharti hilo hivyo Kamati haistahili kulaumiwa.  Kama hivyo, nashauri kuwa suala hili lirudishwe Bungeni ili Wabunge walizungumze na kulifanyia uamuzi muafaka. Vinginevyo watu wataendelea kulauminiana isivyostahili.  Hivyo basi, kuligeuza jambo hili kuwa ni suala la kukataa Muswada au kususia vikao vya Bunge au kufanya maandamano sidhani kama ni sawa. 
Ndugu Wananchi;
Nimeambiwa pia kuwa kulikuwa na hoja ya kutaka idadi ya Wajumbe wa kutoka Tanzania Bara na Zanzibar iwe sawa kama ilivyo kwenye Tume ya Mabadiliko ya Katiba.  Sababu ya idadi ya Wajumbe wa Tume kuwa sawa inatokana na utaratibu wao wa kufikia uamuzi.  Ni kwa maelewano ya wote (consensus) na siyo kwa kupiga kura.  Ndiyo maana idadi imewekwa sawa ili sauti za pande zote zisikike sawia.  Bunge Maalum lina sharti la kufanya uamuzi kwa theluthi mbili ya kura za kila upande kukubali.  Bila ya hivyo hakuna uamuzi.
 Hivyo basi, katika Bunge Maalum nguvu si uwingi wa kura ambazo upande fulani unaweza kupata bali ni ulinganifu sawa wa kura za kila upande peke yake.  Huu ndiyo msingi unaotumika katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hivi sasa kwa lengo la kulinda maslahi ya Zanzibar.  Zanzibar ina Majimbo 50 ya uchaguzi na Tanzania Bara ina Majimbo 189, hivyo ukiamua kwa wingi kila wakati Wazanzibari watashindwa.  Lakini, hapajakuwepo madai ya Zanzibar nao kutaka kuwa na idadi sawa ya majimbo kama Bara au kupunguza majimbo ya Bara yawe sawa na ya Zanzibar kwa sababu wingi si hoja. Msingi unaotumika ni kutoa nguvu sawa za uamuzi kwa kila upande wa Muungano wakati wa kuamua masuala ya Katiba.  Hakuna mdogo wala mkubwa, wote wako sawa.  Hakuna mdogo kumezwa na mkubwa.  Ndiyo msingi unaopendekezwa kutumika kwenye Bunge Maalum hivyo hakuna kitakachoharibika kwa idadi ya Wajumbe kutokukulingana.  Nadhani inafaa ibaki ilivyo.  Lakini kama Wabunge wataamua waongeze idadi itakuwa kwa sababu nyingine siyo hii ya mfano wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Ndugu Wananchi;
          Katika orodha ya madai ya ndugu zetu wa upinzani lipo suala la uhai wa Tume ya Katiba.  Wanataka usiishe wanapokabidhi rasimu ya pili kwa Bunge Maalum bali waendelee kuwepo mpaka mwisho wa mchakato.  Nimeulizia ilikuwaje?  Nimeelezwa kuwa jambo hili halitokani na mapendekezo ya Serikali wala ya Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala.  Limetokana na pendekezo la Mbunge katika Bunge wakati wa kupitia vifungu na kuungwa mkono na Wabunge wengi.  Kwa hiyo kuilaumu Serikali si haki.  Serikali inaweza kuwa mshirika katika hoja hii.
          Nami naiona hoja ya Wajumbe wa Tume kuwa na wajibu wakati wa Bunge Maalum hasa wa kusaidia kufafanua mapendekezo ya Tume.  Je ushiriki huo uwe vipi? Je ni Wajumbe wote au baadhi yao ni jambo linaloweza kujadiliwa.
Ndugu Wananchi;
Naomba nimalizie kwa kuwasihi viongozi wa CHADEMA, CUF na NCCR-Mageuzi kuongozwa na hekima iliyotumika wakati tulipokuwa na tatizo linalofana na hili kuhusu Sheria ya Mabadiliko ya Katiba. Mimi naamini kama iliwezekana kufanikisha mambo wakati ule inaweza kufanya hivyo hata safari hii. Itatufikisha pale tunapopataka salama salimini bila maandamano, kushupaliana au uvunjifu wa amani.  Kupanga ni kuchagua, naomba sote, mmoja mmoja na kwa umoja wetu tuchague njia ya mazungumzo na maelewano kwani itaihakikishia nchi yetu amani, usalama na utulivu. Tukifanya hivyo historia itatuhukumu kwa wema
ASANTENI KWA KUNISIKILIZA
MUNGU IBARIKI TANZANIASIKU moja baada ya Rais Jakaya Kikwete kuvisihi vyama vya CHADEMA, CUF na NCCR-Mageuzi kusitisha maandamano yao na kurejea meza ya mazungumzo ili kupata muafaka wa muswada wa sheria ya kubadili sheria ya mabadiliko ya katiba, vyama hivyo vimetoa masharti mazito ya kukutana naye.
 
 
Hatua hiyo inakuja wakati vyama hivyo vikiendelea kushikilia msimamo wao wa kuitisha maandamano ya nchi nzima kupinga muswada huo, wanaodai kuwa unalenga kuipa CCM nafasi ya kuhodhi mchakato wa katiba mpya.
 
 
Wakati vyama hivyo vikiwa vimefanya mikutano ya ndani na makundi mbalimbali, na kisha mikutano miwili ya hadhara Dar es Salaam na Zanzibar, CCM nayo inakazana kumshinikiza rais asaini muswada huo kama ulivyopitishwa na Bunge.
 
 
Tanzania Daima Jumapili limedokezwa kuwepo mvutano mkali ndani ya CCM, ambako makundi ya vigogo wanaotajwa kugombea urais mwaka 2015, wanampinga Rais Kikwete kwa jinsi anavyoendesha mchakato huo, wakidai anawabeba wapinzani.
 
 
Licha ya wadadisi wa masuala ya kisiasa kumtabiria Rais Kikwete kuwa anaweza kujiandikia historia nzuri endapo mchakato huo ukifanikiwa kwa kuzingatia matakwa ya wananchi, CCM inamtazama mwenyekiti huyo kama anataka kuwakomoa wenzake.
 
 
“Kuna msuguano mkali ndani ya CCM, Rais Kikwete ana nia njema na mchakato huu ili ukamilike kwa amani, lakini wenzake ndani ya chama wanadhani anataka kuwanufaisha wapinzani kwani hatakuwa na chochote cha kupoteza,” alisema kigogo mmoja wa CCM.
 
 
Ni katika nia njema hiyo Rais Kikwete katika hotuba yake ya mwisho wa mwezi, aliwasihi viongozi wa vyama vitatu vya upinzani kutoandamana, badala yake wakae na kutafuta njia mbadala ya kisheria kuboresha muswada huo, na kwamba serikali iko tayari kuwasikiliza.
 
 
Hata hivyo, wito wa Rais Kikwete umepokelewa kwa taswira tofauti na vyama hivyo, vikisema kuwa yeye ndiye anapaswa kuwaandikia barua kuwaomba akutane nao kwa mazungumzo Ikulu, kwani wao hawajawahi kuomba kukutana naye.
 
 
Badala yake, vyama hivyo vilisisitiza kuwa viliomba kukutana na wadau mbalimbali na wananchi kumshinikiza asisaini muswada, na kwamba msimamo wao uko pale pale.
 
 
Katika msimamo huo, vyama hivyo vimesema maandamano yaliyotangazwa kufanyika Oktoba 10 nchi nzima yako pale pale, na kamati ya maandalizi inaendelea kufanya taratibu zote.
 
 
Wakizungumza jana jijini Dar es Salaam, wawakilishi wa vyama hivyo, John Mnyika (CHADEMA), Faustine Sungura (NCCR-Mageuzi) na Abdul Kambaya (CUF), walisema kuwa kamati ya maandalizi ya maandamano inaendelea kwa kuwa Rais Kikwete katika hotuba yake hakugusia suala lolote kama atasaini muswada huo au la.
 
 
“Rais amezungumzia hoja za upinzani za kuvunjwa kwa Tume ya Jaji Joseph Warioba kabla ya kumaliza muda wake, kwa hili tunampongeza, amekuwa wazi. Lakini afahamu kuwa hiyo si hoja kuu iliyosababisha tuandae maandamano kushinikiza asisaini huo muswada.
 
 
“Mambo mengine mazito yapo, kuhusu muundo wa Bunge la Katiba na idadi ya wajumbe kwa uwiano sawa wa Zanzibar na Tanganyika na kuhusu maoni ya wadau kuachwa,” alisema Mnyika.
 
 
Alisema kuwa maoni ya wadau yamepuuzwa, uchakachuaji umefanyika, taasisi zilipeleka majina, lakini Rais Kikwete anasema kuwa alizingatia hilo, kwamba wanamwomba aseme kwanini hakuchukua jina kati ya yale yaliyopendekezwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Shirikisho la Vyama vya Wenye Ulemavu (Shiwavyata) na CCT.
 
 
Alisema kuwa hao walijitokeza kwenye kamati wala hawakusema kwa siri, hivyo Rais Kikwete awaambie mawaziri wake wamwambie ukweli.
 
 
Alihoji kuwa Rais Kikwete katika hotuba yake ametumia neno ‘nimeambiwa’ kwa kiasi kikubwa, kwamba ingefaa mawaziri wake hasa Waziri wa Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi; Waziri wa Sheria na Katiba, Mathias Chikawe; Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mahusiano na Uratibu, Stephen Wassira na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sophia Simba wamwambie ukweli.
 
 
“Huyu huyu rais ndie aliwaambia wafanyakazi wakati wa mgomo wao kuwa akili za kuambiwa na viongozi wao wachanganye na za kwao, kwanini katika mambo aliyoambiwa na wasaidizi wake hakujiridhisha kwanza?” alihoji.
 
 
Hivi karibuni, Waziri Wassira aliwakejeli wapinzani kuwa wasitarajie tena kukaribishwa Ikulu, kutokana na msimamo wao wa kususia mjadala wa muswada wa marekebisho ya sheria ya mabadiliko ya katiba wa mwaka 2013.
 
 
Alisema kuwa maandamano yaliyokuwa yanaandaliwa kumshinikiza rais asisaini muswada huo, hayana maana kwani rais hana sababu za kutousaini.
 
 
Licha ya Wassira kudai milango ya wapinzani kuzungumza na rais katika suala hilo imefungwa, Rais Kikwete amewasihi wapinzani wakae na serikali wajadili kasoro zilizopo kwenye muswada kama walivyofanya mwaka 2011 wakati mchakato unaanza hatua ya kwanza.
 
 
Hata Waziri Chikawe naye alimtisha rais hivi karibuni kuwa iwapo ataliafiki suala hilo la wapinzani na makundi mengine, na kuacha kutia saini muswada huo, atakuwa ametengeneza mgogoro na mhimili wa Bunge kutokana na chombo hicho kukamilisha kazi yake.
 
 
Lakini rais amewapuuza mawaziri wake hao na kutumia busara akisema kuhusu hoja ya Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria kutokufanya vikao Zanzibar kusikiliza maoni ya wadau, saula hilo lilianzia bungeni hivyo linaweza kurudishwa huko lijadiliwe tena.
 
 
Kuhusu rais kumwandama Msemaji wa Kambi ya Upinzani, Tundu Lissu kuwa alisema uongo bungeni, Mnyika alisema hakufanya vema kumshambulia mbunge huyo kwani hayo hayakuwa mawazo yake binafsi bali maoni ya kambi ya upinzani.
 
 
“Inakuwa sio vizuri mbunge aliyetoa mawazo bungeni kwa mujibu wa katiba na kanuni za Bunge kushambuliwa kwa maneno makali na rais wakati alikuwa anatoa mawazo ya kambi wala si yake,” alisema Mnyika.
 
Lissu ajibu
 
Akizungumza na gazeti hili, Lissu amehoji hotuba ya Rais Kikwete iliyojaa neno “nimeambiwa” akisema ana uhakika gani wale waliomwambia kama hawakumdanganya?
“Maneno yaliyotajwa na rais kuhusu uteuzi wa wajumbe toka Shirikisho la Vyama vya Wenye Ulemavu, TEC na CCT yalizungumzwa kwenye kamati sio maneno yangu. Kikwete hakuwepo kwenye kamati, mimi nilikuwepo. Sasa mawaziri wake na wabunge wake wa CCM wamwambie ukweli, waache kumdanganya.
 
 
“Kikwete amesema mimi ni muongo, mnafiki, lakini hoja ambazo tulizipinga mfano ya ushiriki wa wadau wa Zanzibar, hata Waziri wa Sheria na Katiba wa Zanzibar, Abubakari Khamisi naye ameniunga mkono. Je, na huyu ni mzushi, muongo na mfitini?” alihoji.
 
 
Aliongeza kuwa hoja ambayo rais anakimbilia kwamba alimzuia asiteue wajumbe 166, ilikuja bungeni mwaka 2011, wakaipinga, ikaondolewa. Lakini mwaka huu wameirejesha tena.


Via: Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment