Blog ya kijanja kwa ajili ya watu wajanja

Blog ya kijanja kwa ajili ya watu wajanja

Tuesday, August 4, 2015

Kwa kutumia nadharia za Turton (1975) na Barker (1848) kuthibitisha kuwa, hadi kufikia miaka 800 BK hadi 900 BK mijongeo ya wabantu ilikwashafika maeneo ya mito ya juba na tana


Na. Furaha Venance
M.A.KISWAHILI (UDSM)
2015
Ikisiri
Mijongeo ya Wabantu na kutamakani katika upwa wa Afrika Mashariki ni suala ambalo limewashughulisha wataalamu mbalimbali. Ama kwa hakika wataalamu walio wengi wanaelekea kukubaliana kuwa mpaka kufikia miaka 800 BK na 900 BK mijongeo ya Wabantu ilikuwa tayari imekwishafika maeneo ya Mto Juba na Mto Tana. Hivyo basi, katika makala haya tunakusudia kutumia nadharia ya Barker (1848) na nadharia ya Turton (1975) kuafiki kuwa, mpaka kufikia miaka 800BK na 900BK wabantu walishafika na kutamakani maeneo tajwa hapo juu. Ili kufikia lengo hilo, makala haya yamegwanyika katika sehemu tatu sehemu ya kwanza ni utangulizi ambapo kwa kifupi tutaeleza maana ya Wabantu, sehemu ya pili ambapo ndiyo kiini cha makala haya itakuwa na sehemu mbili, sehemu ya kwanza tutaanza kutalii mawazo ya baadhi ya wataalamu yanayodai kuwa mpaka kufikia miaka hiyo Wabantu walishajongea na kutamakani maeneo ya Mto Juba na Mto Tana na sehemu ya pili ya sehemu hii ndipo tutatumia nadharia ya Barker na Turton kuthibitisha ama kuafiki kuwa mpaka kufikia miaka ya 800 na 900BK Wabantu walishafika na kutamakani maeneo ya Mto Juba na Mto Tana. Sehemu ya tatu ambao ndiyo sehemu ya mwisho itakuwa ni hitimisho la makala haya.

1.0            Utangulizi
Katika lugha nyingi za kibantu neno bantu1 lina maana ya watu Mapunda (1980: 26). Neno Bantu kwa mara ya kwanza lilianza kutumiwa na Dkt. Wilhelm Bleek (1827-1875) katika kitabu chake kilichochapishwa mwaka 1862 kilichopewa jina la Comparative Grammar of South African Languages Collins (1968), Massamba (2002). Bleek alitumia neno Bantu kurejea kundi la lugha alizozilinganisha sarufi za lugha husika hususani kwa kuangalia mfumo wa ngeli za majina na vitenzi na kugundua kuwa lugha hizo zinafanana Massamba (2002:36). Mapunda (keshatajwa, 26-27) anaeleza kuwa, wanahistoria wanaelekea kukubaliana kuwa Wabantu ni jamii ya watu ambao huzungumza lugha zenye asili moja. Aidha, Nurse na Spear (1985:37) wanaeleza kuwa Wabantu ni watu walio na nasaba moja ya Proto-Bantu, waliosambaa labda katika milenia ya pili. Watu hawa wanasadikika kutokea katika kitovu kimoja asili yake ni huko Kameruni na Nigeria ya mashariki. Ama kuhusu madai lao kwamba chimbuko la Wabantu ni huko Kameruni na Nigeria bado wataalamu wanatofautiana kuhusiana na chimbuko la Wabantu.

Aidha, Johnson (1919) katika nadharia yake inayojulikana kama nadharia ya Johnson kuhusu chimbuko la Wabantu na mijongeo yao anaeleza kuwa, mtawanyiko wa Wabantu-Azali ulichukua mwelekeo wa mashariki kuelekea maeneo ya kaskazini ya Maziwa ya Albert na Nyanza ambayo yapo kusini magharibi ya Sudan na kaskazini ya Uganda. Kwa mujibu wa maelezo yake, Maziwa ya Albert na Nyanza kwa maana ya Uganda-Albert-Nile ndiyo kitovu cha chimbuko la Wabantu. Kwa upande wake Greenberg (1955) anatofautiana na Johnson anayedai kuwa, chimbuko la Wabantu ni Uganda-Albert-Nile, kwa maoni yake anadai [1]chimbuko la Wabantu ni mpakani mwa Kameruni na Nigeria na baada ya kutoka maeneo hayo wakaanza kushuka kuelekea kusini mwa Jangwa la Sahara Massamba (2002). Tukiyatazama madai haya tutaona kuwa ndiyo yanayoelekea kuungwa mkono na Nurse na Spear katika fasili yao kuhusu Wabantu na chimbuko lao kama tuliyoitazama hapo juu.

Nadharia nyingine inayozungumzia chimbuko na mtawanyiko wa Wabantu ni nadharia ya Malcom Guthrie (1970). Mtaalamu huyo anaonekana kupinga mawazo yote ya watangulizi wake wanaodai kuwa, chimbuko la wabantu ni Uganda-Albert-Nile (Johnson) na chimbuko la Wabantu kuwa ni mpakani mwa Kameruni na Nigeria (Greenberg). Guthrie anadai kuwa Wazungumzaji wa Kibantu wa mwanzo walikuwa eneo lenye pori kusini mwa msitu wa Ikweta kati ya makutano ya Bahari ya Hindi na Bahari ya Atlantiki. Kwa mujibu wa ramani ya sasa eneo hilo linalotajwa yanasemekana kuwa lipo nchini Zambia Massamba (2007:43-44). 

Kwa kuwa lengo letu si kuzijadili nadharia hizi katika makala haya, itoshe kusema kuwa kwa hakika hatuwezi kupinga ama kukubaliana na akina Nurse na Spear ama nadharia hizo kuhusu hasa chimbuko la Wabantu kwani suala bado linahitaji kufanyiwa utafiti wa kina zaidi ingawa wanahistoria wengi wanakubaliana kuwa, chimbuko la Wabantu ni huko Afrika Magharibi  inakadiriwa miaka 2500 hadi miaka 3000 iliyopita, Wabantu walianza kusambaa maeneo mbalimbali kutokea Afrika Magharibi hususani mashariki ya Nigeria na    Kameruni.  Wabantu hao waliingia Afrika Mashariki wakitokea huko Katanga,  Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Mapunda (keshatajwa: 27)

Kwa maana hiyo tunaweza sema kuwa, Wabantu ni jamii ya Waafrika wenye nasaba moja na huzungumza lugha zenye asili moja ambazo kwa kiasi kikubwa zinahusiana, wanapatikana kuanzia Afrika Magharibi, Afrika ya Kati hadi kusini mwa Jangwa la Sahara.
Mtawanyiko wa Wabantu kwa kutumia nadharia inayodai kuwa, chimbuko lao ni Afrika Magharibi hususani maeneo ya Kameruni na Nigeria unaweza kuonekana vizuri katika ramani ifuatayo:


2.0             Kiini cha Makala
2.1  Madai kwamba hadi kufikia miaka 800 BK na 900 BK mijongeo ya Wabantu ilikwishafika maeneo ya mto Juba na Tana kwa mujibu wa wataalamu mbalimbali.

Kama tulivyokwisha dokeza hapo awali. Katika sehemu tutayatalii mawazo ya baadhi ya wataalamu ambayo kwa hakika yaelekeana kukubaliana na hoja hii kuwa mpaka kufikia miaka hiyo mjongeo wa Wabantu ilikwishafika maeneo ya mto Juba na mto Tana.

Tukiitazama ramani ya sasa ya Afrika Mashariki mto Juba unapatika kusini ya Somalia unakaribia mpakani mwa Kenya upande wa kaskazini na Somalia upande wa kusini (Tazama kielelezo na. 2, uk. 7) wakati mto Tana unapatikana katika nchi ya Kenya. Ama kuhusu mjongeo wa Wabantu mpaka kufikia maeneo hayo yanazungumzwa kwa namna tofauti na wataalamu mbalimbali. Mathalani, Christopher Eheret anatueleza kuwa kufikia karne ya 7 yawezekana Wabantu walifika maeneo ya Mto Tana Massamba (2002:80 ). Kwa maelezo haya ya Eheret ina maana kuwa, mpaka kufikia miaka 600 BK ndiyo kipindi ambacho wabantu walikuwa wamefika mto tana. (karne ya 7 = miaka ya 600 BK).

Aidha, Nurse na Spaer (1985) wanaeleza kuwa hadi kufikia miaka ya 500BK Wabantu walikwisha fika pwani ya kaskazini katika eneo ambalo leo hii ni mpakani mwa pwani ya Kenya kaskazini na pwani ya Somalia kusini Massamba (2002:80). Tukiyachunguza madai haya ya Nurse na Spear bila shaka utaona kuwa, yanawiana na yale ya Eheret tuliyoangalia hapo awali, wakati Nurse na Spear wanataja kuwa kati ya mwaka 500 BK. Wabantu walikuwa wameshatamakani katika pwani ya Kenya kaskazini na pwani ya Somalia kusini ingawa hawataji hasa ni eneo gani, Eheret anatueleza kuwa ni karne ya 7 (miaka ya 600 BK) ndiyo Wabantu walikuwa wameshafika eneo la kaskazini mwa Kenya na anatutajia eneo hilo kuwa ni maeneo ya Mto Tana.

Kwa upande wake, Gonzales (2008) anaeleza kuwa, kwa kutumia ushahidi wa kiisimu kufikia karne 4 BK ( sawa na miaka ya 300 BK) Wabantu walishatamakani katika eneo la pwani ya Afrika Mashariki. Aidha, Jenkins2 anabainisha kuwa Wabantu wa Afrika Mashariki na Somalia inaelekea walihamia maeneo hayo wakitokea Afrika ya kati, anaendelea kueleza kuwa wanahistoria wanakubaliana kuwa Wabantu hao walitamakani eneo la kusini mwa Somalia pengine miaka ya 200 BK. Pamoja na kwamba wataalamu hawa wanatofautiana katika miaka wanayotaja Wabantu kutamakani eneo la upwa wa Afrika Mashariki kimsingi hawa wote wanathibitisha kuwa mpaka kufikia mwaka 800BK na 900BK mjongeo wa Wabantu ulikuwa umeshafika maeneo hayo ya Mto Juba na Mto Tana.

Hata hivyo, kuna madai mengine yanayodai kuwa chimbuko la lugha ya Kiswahili (ama waswahili) ambao kwa asili wataalamu mbalimbali kama vile  Wilhem Bleek (1862), Carl Meinhof (1899), C.M. Doke (1935), Malcom Guthrie (1967,1970,1971), Dereck Nurse na Thomas Spear, Shihabudin Chiraghdin na Mathias Mnyampala (1977), Massamba (2002) kwa kuwataja wachache wanakubaliana kuwa, Kiswahili ni moja wapo ya lugha za  Kibantu. Lugha hii inadaiwa kuwa chimbuko lake ni iliyowahi kuwa himaya ya Shungwaya., Mtetezi wa dai hili ni James Der ver Allen (1993) (Tazama Massamba 2007:51-55). Dai hili laelekea pia kuungwa mkono na Mirikau (2013:14) anaeleza kuwa, baadhi ya Waswahili wametoa maoni yao kwa kusisitiza kwamba Kiswahili kilianza kusemwa na Wabantu wa zamani walioishi Shungwaya. Kwa hakika ingawa dai hili linapingwa na wanazuoni wengine kama vile Greenville (1959) na Massamba kwamba Kiswahili kiliinukia eneo moja mahususi (Tazama Massamba 2002: 85), na bado mpaka sasa kuna utata ama kukubaliana au kutokukubaliana miongoni mwa wanazuoni kama himaya hiyo ilipata kuwepo ama la, Mirikau akijiegemeza katika ushahidi wa fasihi simulizi anaeleza kuwa, eneo la Shungwaya ilikuwa kati ya Mto Juba uliopo nchini Somalia na Mto Tana uliopo nchini Kenya.

Massamba (2002:53) akimnukuu Prins anasema kuwa, Shungwaya ilikuwa himaya kuu ikijumuisha Wasomali, Wakikuyu, Wameru, Watharaka, Wakamba, Wataita, Wapare, Wachaga, Washambaa, Wabondei, Wazaramo na Wagara ilichukua eneo lote la Somalia ya sasa, mashariki ya Kenya na baadhi ya maeneo ya kaskazini mwa Tanzania na inakadiliwa kuwa himaya hii ilipata kuwepo hata kabla ya mwaka 800 BK.  Kutokana na maelezo haya na yale ya Mirikau kuwa eneo la Shungwaya lilikuwa kati ya Mto Juba na Mto Tana na madai kuwa, eneo hili lilipata kuwepo hata kabla ya miaka 800 BK kama anavyodai Prins ni wazi kuwa wanatuthibitishia kuwa mjongeo wa Wabantu mpaka kufikia mwaka 800 BK na 900 BK ulikuwa umeshajongea maeneo ya Mto Juba na Mto Tana.

Aidha, Shihabuddin Chiraghdin (1974:57) katika makala yake yenye kichwa cha habari Kiswahili Tokea Ubantu hadi Ki-“standard Swahili.” ingawa haelezi wazi ni mwaka gani, lakini anatuambia kuwa chimbuko la Waswahili (Wabantu) ni huko Ngozini kaskazini ya Kenya pande za visiwa vya Magunyani inayojumuisha Pate, Faza na Lamu na Tikuu na kushukia mpaka mipaka ya Mto Tana. Massamba (2002:84) anaafiki kuwa ,kati ya miaka 400 BK hadi 800 BK upwa wa Mashariki ya Afrika ulikwishakaliwa na Wabantu na Wakushiti yaani Wasomali na Wagalla. Kwa kuwa Chiraghdin anaeleza kuwa Waswahili (Wabantu) walianzia Ngozini na kuenea mpaka mipaka ya Mto Tana ni dhahiri kuwa kwa maelezo yake na tukiyaoainisha na ya Massamba kuwa, kati ya mwaka 400-800BK Wabantu walikwishatamakani upwa wa Afrika Mashariki bila shaka kama tutakubaliana na madai kuwa Wabantu walitokea kusini Somalia na kuteremka mpaka kaskazini ya Kenya, basi watakuwa pia katika kipindi hicho walikuwa wamejongea maeneo ya Juba na kufika huko Ngozini hadi Mto Tana.

Ama kwa hakika, tukiyatalii mawazo ya wanazuoni na wataalamu mbalimbali tuliowaangalia hapo juu tutaona kwamba ingawa wanatofautiana katika miaka na wengine kuonekana kutaja miaka ya kufikirika zaidi, ila kimsingi wote wanaelekea kukubaliana kuwa mpaka kufikia mwaka 800 BK hadi 900 BK Mijongeo ya Wabantu ilikwashafika maeneo ya Mto Juba na Tana. Hivyo basi, katika sehemu inayofuata kwa kutumia nadharia za Turton (1975) na Barker (1848) kuafiki madai haya.

2.2  Nadharia ya Barker (1848) na Nadharia ya Turton (1975)
Katika sehemu hii tutatumia nadharia hizi kutetea ama kuafiki madai kuwa mpaka kufikia mwaka 800 hadi 900BK mijongeo ya Wabantu ilikwishafika na kutamakani maeneo ya Mto Juba na Mto Tana kama ambavyo wataalamu wengine wanavyodai. Tukianza na:

2.2.1  Nadharia ya Barker (1848)
Nadharia hii inaeleza kuwa, kwenye karne ya 10 BK Wasomali ambao wapo katika kundi la Wakushiti wa Mashariki walianza kuteremka kusini wakitokea katika ncha ya Kaskazi ya pembe ya Afrika ambako ndipo inapodaiwa kuwa yalikuwa maskani yao.  Inadaiwa kuwa katika kujongea kwao huko kusini waliwakuta Wagalla ambao walikuwa wakiishi katika maeneo ya kaskazini na kati ya Somalia ya sasa na kuwafukuza. Nadharia inaendelea kueleza kuwa, Wagalla nao wakateremka kusini na wakawakuta Wabantu ambao walikuwa wametamakani katika eneo la Webi Shebelle. Wagalla wakaanza kupambana na kuwashinda Wabantu wa taifa la Shungwaya ambao wakawasukuma kusini ya Mto Juba hadi wakafika chini ya Mito Tana na Sabaki Massamba (2002:81)

Ama kwa hakika, tukiichunguza nadharia hii, tunaona kwamba kuna mambo ya msingi matatu yanayotufanya kuafikia kuwa mijongeo ya Wabantu mpaka kufikia mwaka 800 BK hadi 900 BK ilikwishafika na kutamakani maeneo ya Mto Juba na Mto Tana. Jambo la kwanza ni kuwa nadharia inataja kuwa,   kwenye karne ya 10 BK ndipo Wasomali walipoanza kujongea kusini na kupambana na Wagalla. Wagalla nao wakazidi kushuka kusini wakakutana na Wabantu ambao nao walisukumwa kusini ya Mto Juba hadi chini ya Mto Tana na Mto Sabaki. Kimsingi hapa karne ya 10 inayotajwa hapa ni sawa na miaka 900 BK. Kwa maana hiyo basi ni dhahiri kuwa kwa nadharia hii na kwa kutumia sababu hii tunaweza kuafiki kuwa mpaka mwaka 900 BK Wabantu walikuwa wameshafika maeneo ya Mto Juba na mto Tana kwa kusukumwa na Wagalla wakitokea eneo la Webi Shebelle. Ingawa pia dai kwamba Wabantu walifika huko kutokana na kusukumwa na Wagalla ama kwa kushughuli nyingine ni dai ambalo linatakiwa kutazamwa zaidi kwa jicho la kitafiti kwa maana kuwa ni dai ambalo linaweza kusailika kutokana na nadharia hii na ile ya Turton tutakayoenda kuitazama hivi punde kuwa na utata unaosababisha kujiuliza maswali ni nani hasa alipambana na Wabantu kati ya Wagalla au Wasomali? Maana nadharia itakayofuata inaeleza tofauti.

Aidha, jambo la pili tunalolipata katika nadharia hii yanayotusukuma kuafika dai hili ni hoja inayodai kuwa, Wabantu hao waliosukumwa na Wagalla maskani yao ilikuwa Webi Shebelle. Tukiangalia ramani ya sasa ya Afrika Mashariki, eneo la Webi Shebelle linapatikana kusini ya Somalia, yaelekea basi kama madai haya ni ya kweli, inawezekana Wabantu hao walikuwa wakiishi pembezoni ama katikati ya Mto Shebelle na Mto Juba. Mto Shebelle unatokea katika nyanda za juu ya Ethiopia unashuka mpaka maeneo ya pwani ya Somalia na kukutana na Mto Juba na kuingia bahari ya Hindi. Kama ni hivyo basi kuna uwezekano mkubwa kuwa Wabantu pengine walikuwa wameshajongea mpaka eneo la Mto Juba katika karne hiyo ya 10 BK (sawa na miaka ya 900 BK) pengine hata kabla ya kusukumwa na Wagalla.

Jambo la tatu nadharia hii inatueleza kuwa, Wabantu walioshambuliwa na kushindwa na Wagalla ni Wabantu wa Shungwaya pia yanatufanya tuafiki kuwa nadharia hii pia inakubaliana na dai kuwa Wabantu walijongea mpaka maeneo ya Mto Juba na Tana katika mwaka 800 BK hadi 900 BK kutokana na eneo la kijiografia linalotajwa kuwa himaya hiyo ilipata kuwepo. Aidha, Mirikau (keshatajwa) anaeleza eneo la  Shungwaya lilikuwa kati ya Mto Juba na Mto Tana.  Eneo hili linatajwa kuwa lilipata kuwepo hata kabla ya mwaka 800 BK kama anavyodai Prins (keshatajwa) ni wazi kuwa nadharia hii ya Barker inatufanya pia kuafiki kuwa mijongeo ya Wabantu mpaka kufikia mwaka 800 BK na 900 BK ilikuwa imeshajongea na kutamakani maeneo ya Mto Juba na Mto Tana kama wanavyodai wataalamu wengine.

2.2.2 Nadharia ya Turton
Tumeangalia nadharia ya Barker (1848), tumeona kuwa, nadharia inaleza kuwa Wasomali walipambana na Wagalla. Wagalla wakazidi kuteremka chini (kusini) wakakutana na Wabantu wakaanza kupambana nao, Wabantu wakaelemewa nao wakasukuMwa hadi kusini maeneo ya Mto Tana. Je, nadharia ya Turton (1975:19) inasemaje?

Turton (keshatajwa) katika makala yake aliyoipa jina la Bantu, Galla and Somali Migrations in the Horn of Africa: A Reassessment of the Juba/Tana Area inayopatika katika Jarida la African History anaeleza kuwa, Wasomali Wahawiya na Wa-kabla ya Wahawiya walitokeo maeneo ya karibu na Merka na kuanza kusambaa kuelekea magharibi na kusini na kulikalia karibu eneo lote la kati ya Mto Juba na Mto Tana mapema kabisa kabla hata Wagalla hawajawasili eneo la pwani. Anaendelea kufafanua kwamba, katika hatua hii ya Wasomali wale wa kundi la Wa-kabla ya Wahawiya kujitanua na kuzidi kusambaa kwa kuelekea kusini waliwakuta Wabantu na kuanza kupambana nao kwa ajili ya kugombea maeneo ya malisho. Wasomali (Wa-kabla ya Wahawiya) wakawasukuma Wabantu kurudi nyuma hadi Mto Tana.

Aidha, Turton anaendelea kutueleza kuwa, baadaye kabisa inakadiliwa pengine kwenye karne ya 16 BK (sawa na miaka ya 1500) Wagalla wenyewe walijongea kuelekea pwani wakifuata uelekeo wa Mto Tana ambako huko waliwakuta watu wa Mijikenda na kuwafukuza (Kumbuka Barker anatueleza kuwa Wagalla walishambuliwa na Wasomali). Watu hao wa Mijikenda kulazimika kuelekea kusini hadi kufikia Mto Sabaki kisha Wagalla wakapamba na kuwaondoa Wasomali katika eneo la Juba na Tana na kuwalazimisha zaidi Wasomali kurudi kaskazini. Aidha, tunaelezwa kuwa, katika karne ya 18 BK (sawa na miaka 1700 BK) Wasomali wakaanza tena kusonga chini na kufikia miaka 1860 Wagalla wakawa wamenyang’anywa eneo lote kati ya Mto Juba na Mto Tana walilolikalia zaidi ya miaka 100. Kwa mujibu wa Turton Wabantu hawakwenda sana kaskazini mwa pembe ya Afrika.

Kwa hakika tukiziangalia nadharia hizi mbili kuhusu mijongeo ya Wabantu katika upwa wa Afrika Mashariki ni wazi kuwa kuna mambo ambayo wataalamu wa nadharia hizi wanapingana. Mathalani, wakati Barker anatueleza kuwa, Wasomali waliwashambulia Wagalla na Wagalla wakawashumbulia Wabantu kwa upande wake Turton anapingana na Barker, yeye anatueleza kuwa Wasomali tena wale Wa-kabla ya Wahawiya ndiyo waliopambana na Wabantu na wala si Wagalla kama anavyodai Barker.

Tofauti nyingine inayojitokeza ni kuwa, wakati Barker anatueleza kuwa Wagalla waliwasukuma Wabantu kusini ya Mto Juba hadi wakafika chini ya mito ya Tana na Sabaki, Turton inaelekea hakubaliani na hili, kwa upande wake anadai kuwa katika mapambano kati ya Wasomali na Wabantu, Wabantu hawakwenda zaidi kaskazini mwa Pembe ya Afrika na kutokana na hoja hii Massamba (2002:82) anaona kuwa nadharia hii hailekei kueleza kwamba Wabantu walivuka Mto Juba kwenda kaskazini zaidi. Dai ambalo kwa hakika ni kweli, hakuna tunakoelezwa katika nadharia hii kuwa Wabantu walifika Mto Juba. Ingawa hatuelezwi hilo ila wote wanakubaliana kwamba mpaka miaka hiyo mjongeo ulishafika na kutamakani mto Tana. Lakini tukichunguza vizuri ramani ya Afrika Mashariki hususani Somalia na Kenya na kama tunakubaliana kuwa himaya Shungwaya kuu ilichukua eneo la Somalia, Kenya na Kaskazini ya Tanzania basi kuna uwezekani mkubwa Wabantu walishafika hadi Mto Juba.

Ama kwa hakika ingawa nadharia hizi zinapingana katika maeneo tuliyoyataja hapo juu, tukizichunguza kwa makini nadharia hizi zote zinaelekea kukubaliana kuwa mpaka kufikia mwaka 800 BK hadi 900 BK Wabantu walikwishajongea maeneo ya Mto Juba na Mto Tana. Hili linathibitishwa na maelezo ya wataalamu wote hawa wawili, ingawa Barker anataja Wabantu walikuwa wamesukumwa kusini ya Mto Juba hadi wakafika chini ya mito Tana na Sabaki, Turton yeye anatueleza kuwa Wasomali waliwalazimisha Wabantu kurudi hadi mto Tana. Kwa maelezo haya ya Turton ni kuwa Wabantu walirudi Mto Tana inaelekea Wabantu walishaanza kuweka maskani maeneo ya Mto Tana na walikuwa wanaelekea Kaskazini ambako ni Somalia kabla ya kukutana na Wasomali.  ingawa haelezi wazi kama walifika Mto Juba ila kimsingi wote wanakubaliana kati ya miaka hiyo Wabantu walikuwa washatamakani maeneo ya Mto Tana.

Si hivyo tu, nadharia hizi pia zaelekea kukubaliana kuwa, Wabantu ndiyo watu wa mwanzo kabisa kufika na kutamakani maeneo hayo kuliko Wasomali ama Wagalla na hii inatokana na ukweli kwamba, tunapoelezwa kuwa, Wagalla waliposhuka chini zaidi waliwakuta Wabantu katika taifa la Shungwa ambalo kama tulivyoelezwa na Mirikau (keshatajwa, uk.14) kuwa eneo la Shungwaya lilikuwa kati ya Mto Juba nchini Somalia na Mto Tana nchini Kenya, ingawa Prins (keshatajwa) anaongezea kuwa eneo la Shungwaya ilichukua eneo lote la Somalia, Kenya na baadhi ya sehemu za kaskazini ya Tanzania.

2       Hitimisho

Kwa hakika, pamoja na kwamba madai ya wataalamu wengi wanakubaliana kuwa hadi kufikia miaka 800BK hadi 900BK mijongeo ya Wabantu na kutamakani kwa Wabantu katika upya wa Afrika Mashariki hususani katika maeneo ya Mto Juba na Mto Tana ilikwishakuwa tayari kuna uwezekano mkubwa pengine Wabantu walishajongea maeneo hayo mapema zaidi kuliko miaka hiyo inayotajwa, tafiti za kiakolojia ingawa zingine hazitaji wazi ni watu wa jamii gani, zinathibitisha kuwa eneo la upwa wa Afrika Mashariki zilianza kukaliwa na watu kuanzia karne ya 3BK. Mathalani Chittick (1975:37) anasema katika maeneo ya unguja Ukuu huko Zanzibar na Manda katika mwambao wa Kenya kulipatikana vifinyange vya zamani sana kati ya vifaa hivyo vimekadiliwa kuwa vilikuwa vya kati ya karne ya tatu hadi karne ya 14 BK Massamba (2002:190). Aidha, Massamba anatudokeza utafiti mwingine wa kiakolojia majengo yaliyochimbuliwa Manda, inakadiliwa kuwa mji huo ulijengwa karne tatu na karne ya tisa, na mji wa Kilwa ulijengwa kati ya nne na karne kumi au karne ya tano na karne ya kumi na moja ama karne ya sita na karne ya kumi na mbili. Kutokana na ugunduzi wa kiakiolojia uliofanywa na Wanakiolojia mbalimbali, Massamba anahitimisha kwa kusema kuwa wenyeji wa asili walioanzisha makazi katika maeneo ya pwani walikuwa ni Wabantu.

Aidha, hata huu ushahidi wa kiakiolojia nao hauwezi kuwa ushahidi wa moja moja kuhitimisha kwa kusema kuwa Wabantu walianza kulikalia eneo la Afrika Mashariki kuanzia karne ya tatu kwa kutegemea kugunduliwa kwa majengo au vyombo/vifaa vya kale kwani vifaa ama amajengo hayo kwa hakika yalijengwa na wageni ambao walikuwa na teknolojia bora zaidi iliyowawezesha kujenga majengo yanayoweza kudumu muda mrefu tofauti na Wabantu ambao kutokana na teknolojia duni iliyokuwa ikitumika katika ujenzi wa nyumba za kibantu isingewezekana majengo hayo kudumu kwa miaka mingi kama yalivyobainika majengo ya wageni. Lakini tatizo lingine tunadokezwa na Massamba (2002:utangulizi) ni kuwa vyanzo vingi vya kihistoria na vya kiakiolojia vilivyopo vinaanzia karne ya kumi na kuendelea. Kutokana na hali hii tunashindwa kupata data zaidi za nyuma ya hapo na hii ni kwa sababu Wabantu hawakuwa na utamaduni wa kuandika au taaluma hiyo ilikuwa bado kuvumbuliwa. Ushahidi unaotumika wakati mwingine unatokana na masimulizi jambo ambalo linatufanya kupata ugumu hasa kujua, Wabantu walianza kuishi lini Pwani ya Afrika Mashariki. Hivyo suala la wabantu walianza lini hasa kujongea na kutamakani maeneo ya upwa wa Afrika Mashariki ni jambo ambalo bado linasawilika. Hivyo basi utafiti zaidi unahitajika kufanyika ili kupata taarifa sahihi kuhusiana na mijongeo ya Wabantu katika upwa wa Afrika Mashariki.

MAREJEO
Chiraghdin, S. (1974) “Kiswahili Tokea Ubantu hadi Ki-Standard Swahili.” Katika Mulika.
                  Na. 6 (1974) uk. 57-60.

Charaghdin, S. Na Mnyampala, M. (1977) Historia ya Kiswahili. Nairobi. University Press.

Collins, R.O. (1968) Problem in African History.
Gonzales,R.M (2008) Society, Religion and History: From Hunter land to Motherland, The Northeast-
                  Central Culture Zone. Columbia University Press. Iimepakuliwa kutoka
                   www.guternberg- e.org/gonzales tarehe 05/06/2015.

Jenkins, O.B (HM) Race and Ethnicity in The Horn of Africa. Imepakuliwa kutoka
                     www.orvillejenkins.com/people/race and ethnicity.html

Mapunda, H. (1980) Historia ya Mapambano ya Mtanzania. Dar es Salaam. TPH.

Massamba, D.P.B. (2002) Historia ya Kiswahili: 50 BK hadi 1500 BK. Nairobi.
                      The Jomo Kenyatta Foundation.

Massamba, D.P.B. (2007) Kiswahili Origins and The Bantu Divergence-Convergence Theory.
                      Dar es Salaam. TUKI.

Mrikau, S.a. (2013) Msururu wa PTE Kiswahili. Nairobi. East African Educational Publishers ltd.
Nurse, D. Na Spear, T. (1985) The Swahili: Reconstructing the History and Language of an African
                        Society, 800 – 1500. University of Pennsylavania Press.

Turton, E.R. (1975) “Bantu, Galla and Somali Migrations in The Horn of Africa: A Reassessment of the
                        Juba/Tana Area.” Katika Journal of African History. Vol.16. no. 4 (1975) uk.519-537.           
                         Cambridge University Press. Imepakuliwa kutoka     
                        www.jstor.org/stable/1804495?seq=/#page_tab_contents tarahe 05/06/2015


No comments:

Post a Comment