Blog ya kijanja kwa ajili ya watu wajanja

Blog ya kijanja kwa ajili ya watu wajanja

Friday, August 7, 2015

MSANII MWINGINE AWAPONDA WASANII WENZAKE AANDIKA BARUA NZITO KWAO. KISA DINNER YA JANA USIKU



Barua ya Msanii Marufuku!
YAH. MAISHA YA WAPENZI WA WASANII MAARUFU NA WASANII MARUFUKU.

Wapendwa wanasiasa na yeyote atakaye husika, rejea kichwa cha Barua hii hapo juu. 
'Ashakum si Matusi'

Mimi Vitali Maembe 'Mswahili' Mmoja wa wasanii Marufuku wa Tanzania! Nazungumza nikiwa Upande wa ukweli, Bado sijaolewa na Chama chochote cha siasa na hakuna Chama kinachonijua 'kwa upande huo mimi bado Bikra' na ninajivunia hilo. Sitagombea, sigombei na sijawahi kumpigia mtu wala Chama chochote debe, labda nitafanya hivyo kukiwa na chama chenye misingi ya Uafrika wa kweli au katiba ikiruhusu mgombea Binafsi. Ila nitapiga kura kwa kuwa ni Haki na wajibu wangu na nitaamua kwa haki kwaajili ya ubora wa Taifa langu.
Ndugu!

Nimepata taarifa kupitia vyombo vya habari kuwa kulikuwa na Hafla fupi ya kumuaga Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na kumpongeza mh John Magufuli ambaye anagombea Urais 2015, Hafla iliyoandaliwa na Umoja wa Wasanii watanzania na kauli mbali mbali zimetolewa kwa wasanii na kwaniaba ya wasanii.

Napenda kwanza kabla sijasema lililonigusa nifafanue kuwa Kuna tofauti kati ya Umoja wa Vijana na Umoja wa vijana wa CCM, Kuna tofauti kati ya Umoja wa wanawake na Umoja wa wanawake wa CCM. Na kila umoja ni halali kwa namna ulivyoundwa na ulivyohalalishwa. 

Sasa nyinyi ndugu zangu watu wa habari mnaporipoti msikurupuke semeni kwanguvu, msinong'one wafafanulieni watu kama ni Umoja wa wasanii wa CCM au wa watanzania? Umoja wa wasanii wa Tanzania umeanza lini na ameuanzisha nani mbona nyinyi wanahabari hamkuwahi kututaarifu hilo? au umoja wa wasanii Maswahiba wa Kikwete? 
Hayo nimeyamaliza nishawasamehe, mnajua mlitendalo lakini hamko juu ya kazi yenu na uhuru pia hamna. siyo kosa lenu.

Naanza sasa!
Kwanza ningependa kuifahamisha Dunia kuwa Serikari ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Maafisa wake wakiongozwa na Rais wetu J. M. Kikwete haijawahi kunisaidia na kwa roho zao Mbaya sizani kama watakuja kunisaidia katika kazi yangu wala katika malezi ya wanangu. 

Maafisa wa Serikali ya Mkapa na Kikwete wamekuwa kikwazo katika kazi yangu ya sanaa tangu naanza kusoma mpaka kazi, wamewanyanyasa na kuwadhurumu wasanii na wanachi wa Tanzania wasiojua lolote Masikini wa Mungu, haya nayasema mtandaoni, nayasema kwenye nyimbo zangu na hata kesho nikiwa hai naweza kuyasema kwa sauti kubwa nikiwa juu ya Paa na sio uvunguni mwa kitanda.

Wasanii Maarufu na Wasanii Marufuku!
Kwa ushauri tu, Nd. Magufuli au Mtu yeyote utakaye kuwa Rais, usijitoe Akili! Unafahamu kuwa Kikwete anaondoka Madrakani huku Nchi haina Sera ya Utamaduni, Chuo cha sanaa Bagamoyo, Baraza la sanaa na COSOTA vimeoza, Kazi za wasanii zinauzwa ovyo na wasanii wanadhalilika mitaani kuhusu haki miliki. Wasanii hawana faida na kazi zao wanakuwa walevi wa pombe na dawa za kulevya. 

Nyinyi mnaojiita Chama tawala, Utamaduni unadhlilishwa mikononi mwenu, jikazeni katika upande huu tuone kweli kama mnatawala, na nyinyi 'vyama tawaliwa' mnaojiita wapinzani mjikaze msije mkachukua nchi iliyoposwa. Utamaduni wa nchi kubwa kama hii unavuliwa nguo mnaangalia, unachezewa matiti Makaka wakubwa mnachekacheka tu! 
Wako 
Msanii Marufuku!



No comments:

Post a Comment