Na. Furaha Venance
M.A. KISWAHILI (UDSM)
2015
Ikisiri
Utendi
wa Ras I’Ghuli
kama tunavyoelezwa na Leo Van Kessel (1973,dibaji) kuwa unatokana na kisa
kimoja cha Kiarabu kiitwacho Futuhu
‘lYamani maana yake ni kushindwa au kutiishwa kwa Yemeni. Kisa hicho cha
Kiarabu husimulia jinsi nchi ya Yemeni ilivyoshindwa na kutekwa na majeshi ya
Waislamu. Mwanzoni kisa hiki kiliandikwa katika lugha ya kigeni (Kiarabu).
Hivyo si Waswahili wengi walioweza kukielewa ndipo Mwalimu Mgeni bin Faqihi
aliamua kukibadili kisa hicho kutoka katika usimulizi wa kawaida kuwa utenzi
na kukiandika kwa lugha ya Kiswahili
lakini kwa kutumia hati za Kiarabu ili kiweze kusomwa na watu wengi zaidi. Kwa
kuwa kisa hicho kwa asili kilikuwa kinawahusu Waarabu na Uislamu na kiliandikwa
kwa lugha ya Kiarabu swali la kujiuliza je kutafsiriwa kwa kisa hicho kwa lugha
ya Kiswahili lakini kikiandikwa kwa kutumia hati za Kiarabu na baadaye
kuandikwa kwa haati za Kirumi, je tunaweza kuujumuisha utendi huo kuwa ni
utendi wa Kiafrika au Kiswahili? Hivyo makala haya yanakusudia kuuhakiki utendi
huo kama una sifa za kuitwa utendi wa Kiswahili au la. Hivyo basi kukamilisha
lengo hilo kazi hii imegawanyika katika sehemu kuu nne. Sehemu ya kwanza ni
utangulizi katika sehemu hii tutatoa fasili ya utendi, muhtasari wa kitabu na
usuli wa mwandishi na sehemu ya pili, kwa kuwa kulishawahi kutolewa mawazo kuwa
hakuna utendi wa Kiafrika tutaongozwa na vigezo kama vilivyopendekezwa na
Mulokozi (1999) kuuhakiki utendi huo kama unakidhi vigezo vya kuitwa utendi wa
Kiafrika kabla hatujazama kuutazama utendi huu kama una sifa za kuitwa utendi
wa Kiswahili. Sehemu ya tatu tutajikita kuangalia kama Utendi wa Rasi ‘lGhuli unakidhi vigezo vya kuitwa utendi wa
Kiswahili tukimakinikia vigezo vya kifani na kimuundo. Na sehemu ya mwisho ni
hitimisho.
1.0
Utangulizi
Dhana utendi ni dhana iliyowashughulisha
wataalamu mbalimbali. Mathalani, Chaligha (20013:82) anatueleza kwamba,
mtaalamu Bowra (1930) anatumia fomula kuelezea maana ya utendi kuwa ni U=M+V
(Utendi =Muziki + Vita) akiwa na maana utendi ni tukio la kimuziki unaozungumzia
vita na miungu kwa njia ya ushairi ulioandikwa. Kwa upande wake Mulokozi (2009),
anasema, utendi ni utungo mrefu wa kishairi wenye kusimulia hadithi ya ushujaa
na mashujaa, na utenzi ni utungo wowote mrefu wa kishairi, aghalabu wenye kutoa
mawaidha ya kidini au ya kidunia au kusimulia habari fulani. Aidha, Belcher
(1999: xiv) anasema kuwa, tendi ni masimulizi ya papo kwa papo yanayohusu
masuala ya kihistoria ambayo hutolewa hadharani mbele ya hadhira na yeli
maalumu. Anaendelea kufafanua kuwa, tendi nyingi huambatana na muziki. Aidha Wamitila
(2003:333) anasema kuwa, utendi ni shairi refu la kisimulizi linalozungumzia
kwa mapana na mtindo wa hali ya juu matendo ya mashujaa au shujaa mmoja.
Ama
kwa hakika tukiwaangalia wataalamu wote hawa kimsingi hawatofautiani sana isipokuwa
wengine wamejikita zaidi kutoa fasili zinazoegemea katika utendi simulizi na wengine
wamejikita katika utendi andishi na wapo wengine ambao fasili zao zimejumuisha
aina zote za utendi yaani utendi simulizi na utendi andishi. Mathalani Bowra
anauona utendi kama kazi iliyoandikwa akijikita zaidi katika utendi andishi
wakati Belcher, Molokozi na Wamitila wote wanakubaliana kuwa utendi ni
shairi/nyimbo ndefu za kisimulizi wakijikita katika kigezo cha utendi simulizi.
Kutokana na maelezo ya wataalamu hao kuhusu tendi, tunaweza
kujumuisha mawazo hayo kwa pamoja kwa kusema, utendi ni masimulizi marefu yenye
umbo la kishairi yanayoelezea visa kuhusu mashujaa na matendo yao ya kishujaa,
historia na ustawi wa jamii. Tendi inaweza kuwa katika umbo la usimulizi ama
uandishi mara nyingi utendi ukiwa katika usimulizi uwasilishaji wake huambatana
na muziki.
1.1
Muhtasari wa Utendi wa Rasi ‘lGhuli
Utendi wa Rasi ‘lGhuli unatokana na kisa cha Kiarabu kiitwacho Futuhu ‘lYamani ikiwa na maana kushindwa au kutiishwa kwa Yemeni.
Kisa hicho cha Kiarabu husimulia jinsi nchi ya Yemeni ilivyoshindwa na kutekwa
na majeshi ya Waislamu yakiiongozwa na Mtume Muhamadi[1] mwenyewe, Seyyidna Ali bin
Abi Talibu[2] (kuanzia sasa Seyyidna
Ali) na Seyyidna Umar bin Khatab kunako karne 6. Tafsiri ya utendi huu umepewa
jina la Rasi ‘lGhuli linalotokana na
jina la kebehi la mtawala wa makafiri wa Yemeni ambaye jina lake halisi aliitwa
Mukhariki bin Shahabu. Jina hili la kebehi Ras ‘lGhuli lina maana ya Kichwa cha Nyoka.
Kwa ujumla utendi huu una beti zipatazo 4584. Kuanzia ubeti wa
1-43 ni nyongeza ya mshairi ambapo anaanza kwa kumsifu Mungu na anaeleza sababu
ya kutafsiri kisa hicho kutoka lugha ya Kiarabu hadi Kiswahili. Kisa chenyewe kinanzia
aubeti 44- 4,565 na kuanzia ubeti 4,566 hadi 4,584 ni nyongeza ya mshairi
ambapo anamalizia kwa kuomba dua.
Visa vya utendi huu vimepangwa katika sehemu viii (nane). Utendi unaanza
Muhamadi akielezwa jinsi mtawala wa Yemeni Mukhairiqi bin Shahabu (Rasi ‘lGhuli)
anavyo wadhulumu watu wake. Muhamadi anatokewa na malaika Jiburili na kumtaka
kumtuma mtu kwenda kupeleleza nchi ya Rasi ‘lGhuli.
Malaika Jiburili anamweleza Muhamadi habari za kukamatwa kwa
Zuberi, Sayyidna Umari anatumwa kuipeleleza nchi ya Rasi ‘lGhuli. Mtume anaamua
kupeleka jeshi kupambana na Rasi ‘lGhuli. Rasi ‘lGhuli anaazimia kuishambulia Madina,
mapigano makubwa yanaanza majeshi ya pande zote mbili yanapigana siku kucha
Muhamadi anamuomba Mungu dua, Mungu anaitikia sala yake anawatuma malaika
kusaidia jeshi la Waislamu kupambana na makafiri na anatuma na tufani ya mvua
makafiri wanashindwa na kukimbia wengine wanasilimu. Majeshi ya Waislamu
yanateka miji kadhaa. Rasi l’Ghuli anaomba msaada kwa majeshi mengine. Majeshi
ya Waislamu yanazidiwa nguvu mpaka anapowasili Sayyidna Umar majeshi ya
makafiri yanashindwa na kukimbia.
Vita vinaanza upya Rasi ‘lGhuli anawapa silaha askari wake.
Muhamadi naye anaandaa vikosi viwili vya jeshi moja linaongozwa na Sayyidna Ali
na lingine linaongozwa na Sayyidna Umari. Majeshi ya Rasi ‘lGhuli yanashambuliwa.
Majeshi ya Rasi ‘lGhuli yanalivamia jeshi la Waislamu katakati ya mapambano
Rasi ‘lGhuli anakimbia na kukimbilia mjini anaingia gerezani bila kutarajia
anamkuta Sayyidna Ali. Wanapigana
hatimaye Sayyidna Ali anafanikiwa kumuua kwa kumkata kichwa na kuamuru kichwa
chake kitundikwe katika lango la mji ili kila anayepita akione. Makafiri
wanakimbizwa mpaka milango ya mji wanapoona kichwa cha Rasi ‘lGhuli
wanafadhaika wengine wanasilimu wasiosilimu wanauwawa Mtume Muhamadi anaweka
utawala mpya na kurudi na watu wake Madina baada ya ushindi. Kwa ufupi kisa cha
utenzi huu kiliandikwa katika muktadha wa kuanzishwa na kuenezwa kwa dini ya
Kiislamu huko Saudia Arabia na Yemen.
Tunataarifiwa kuwa, utendi huo hughanwa au kusomwa wakati wa
sherehe kama vile matanga, harusi, n.k. na mghani maarufu wa utendi huo
tunaambiwa kuwa alikuwa ni Mwalimu Sefu bin Hamidi wa Bagamoyo Leo Van Kessel
(keshatajwa, dibaji).
1.2 Usuli kuhusu
mwandishi wa Utenzi wa Ras ‘lGhuli
Kwa mujibu wa Mhariri wa utenzi huu,
Bwana Leo Van Kessel anatueleza
kuwa, Mgeni bin Faqihi alikuwa ni Mtumbatu kutoka Unguja aliyehamia Bagamoyo.[3]
Inasemekana kuwa alizaliwa mwanzoni mwa karne ya 19. Huko Bagamoyo alikuwa
akifundisha dini ya Kiislamu katika vyuo vya Kiislamu. Alitumia muda wa miaka
mitano kukamilisha utendi huu kwani inasemekana alianza kuandika utendi huu
mwanzoni mwa miaka ya 1850 na kuukamilisha mwaka 1855. Ni miongoni mwa washairi na watunzi wazuri wa kazi za fasihi
kutoka Zanzibar waliopata kuwepo. ama kuhusu tarehe ya kufariki kwake bado mpaka
sasa haijuikani.
Aidha
kwa kuwa, kazi hiyo inaitwa Utenzi wa Ras
‘lGhuli na kwa kuwa unatokana na kisa cha kiarabu na unazungumzia habari za
Waarabu na dini ya Kiislamu. Je huu ni utendi? Kumbuka si kila utenzi unaweza
kuwa utendi. Hivyo ili kutegua kitendawili hiki itatulazimu kwanza kuondoa
utata huo kwa kuangalia sifa za utendi wa Kiafrika ili kuuona utenzi huu kama
unakidhi sifa hizo na tunaweza kuuweka katika kundi la tendi, ndipo sasa
tuingie katika msingi wa hoja yetu, ya kuthibitisha kama utenzi huu una sifa za
utendi wa Kiswahili ama la.
2.0
Sifa
za utendi wa Kiafrika
Ama kuhusu sifa za utendi, wataalamu
mbalimbali wameainisha vigezo au sifa za utendi wa kiafrika. Miongoni mwa
wataalamu hao ni, Finnegan (1970) Okpewho (1979), Johnson (1986), Mbele (1986), Belcher (1999), Mulokozi (1999),
kwa kuwataja wachache. Aidha Utendi wa
Rasi ‘lGhuli ni utendi unaonekana kuzingatia vigezo vya utendi kama
vilivyopendekezwa na Mulokozi (1999:11) baada ya kufanya majumuisho ya mawazo ya watafiti mbalimbali na
kupata vigezo vipya vya utendi wa kiafrika ambavyo ni: (a) Utendi kuwa na sifa
ya usimulizi yaani huwa na umbo la kihadithi, (b) Ni nudhumu yaani hutolewa
kishairi na huwasilishwa kwa kughanwa hususani pamoja na ala ya muziki, (c) Huhusu
matukio au masuala muhimu ya kihistoria na/au kijamii, (d) Huelezea habari za
ushujaa na mashujaa, (e) Matini yake kwa kawaida hutungwa papo kwa papo na (f) Utendi
hutawaliwa na muktadha wa utunzi na uwasilishaji wake kwa jamii.
Ama
kwa hakika, ingawa vigezo hivi vinavyotajwa na Mulokozi (keshatajwa) kujikita
zaidi katika utendi simulizi, na tukiuchunguza Utendi wa Ras ‘iGhuli tutaona kuwa unakidhi vigezo hivyo. Hebu
tuanze kuangalia vigezo hivyo jinsi vinavyojitokeza katika utendi huo. Tukianza
na:
Kigezo
cha masimulizi yaani utendi kuwa katika umbo la kihadithi. Utendi wa Ras ‘lGhuli ni miongoni mwa tendi ambazo zinakidhi kigezo
hiki cha usimulizi. Leo van Kessel (keshatajwa, viii) anatubainishia hili
anapotuambia kuwa, mshairi ni msimulizi bingwa. Anatuhadithia wingi wa mambo ya
kusisimua yaliyojiri wakati wa vita. Ukiisoma utendi huu utagundua kuwa ni
masimulizi yaliyo katika umbo la kihadithi
yanaeleza habari za kuinukia kwa dini ya Kiislamu na mapambano ya vita
yaliyoongozwa na Seyyidna Ali bin Abi Talib, Seyyidna Umar bin Khatab na Mtume
Muhamadi kunako karne ya sita na ushindi walioupata katika vita hivyo
kuwashinda makafiri na Mtume Muhamadi kusimika utawala mpya na kurejea Madina
ambako walipokelewa kwa furaha. Rejea ubeti wa 4560-4563. Ama kwa hakika
tukichunguza beti hizi utaona kuwa utendi huu umekaa kisimulizi msimulizi
anatusimulia hadithi ya kuinukia kwa dini ya Kiislamu na vita vya mapambano
kati ya majeshi ya Waislam na makafiri na ushindi wa majeshi ya Muhamadi na
namna walivyorejea Madina na kupokelewa.
Sifa nyingine ambayo inajitokeza katika
utendi huu ni kuwa na sifa ya nudhumu. Wamitila (keshatajwa, 171) anaeleza
nudhumu ni tungo za kifasihi zenye matumizi ya lugha yanayozifanya tungo hizo
kubaguliwa au kubainika kama zisizo za kinathari. Anaendelea kufafanua kuwa
tungo hizo hutumia mapigo kwa utaratibu maalumu aghalabu neno hili hutumiwa kwa
maana ya tungo za kishairi. Kwa maelezo haya yanatupa maana kuwa utendi
unatakiwa kuandikwa au kutolewa kishairi na kuwasilishwa kwa kughanwa. Utendi
huo una sifa ya kishairi na vipengele vifuatavyo ndivyo vinavyoufanya utendi
huu kuwa na sifa ya kishairi:
(a) Utendi
umeundwa na beti, Wamitila (keshatajwa, 243) anasema ubeti ni kifungu cha
mshororo mmoja mmoja au mishororo kadha katika shairi na ambacho
kinajitosheleza. Utendi wa Rasi ‘iGhuli umeundwa na beti 4584 na kila ubeti
umeundwa na vipende vinne vya mistari ambavyo vinajitosheleza na hivyo kubeba
sifa ya ushairi.
(b) Kila
ubeti umeundwa na vina na mizani 8 kwa kila kipande cha mstari. Abedi (1953:
15) anasema tenzi nyingi zaidi huwa zenye mistari minne na mizani nane kama
inavyojitokeza katika Utendi wa Rasi
‘iGhuli. (rejea beti za utenzi huo). Tukitazama beti hizo tunaona kuwa, kila
kipande kimeundwa na mizani nane (8) na kuhusu vina kila ubeti umebeba vina
vyake huku kukiwa na kina bahari cha ri
kinachojitokeza katika beti zote. Sifa zote hizo zinaufanya utendi huo kuwa na
sifa ya kishairi. Ikumbukwe kuwa tendi nyingi za Kiswahili huundwa na beti
ambazo kila ubeti huundwa na mistari minne ingawa pia zipo tendi zenye kutumia
mistari zaidi ya mine katika beti, mfano mzuri ni Utenzi wa Vita vya Kagera msimulizi amechanganya mistari zaidi ya
minne. Tendi nyingine za Kiswahili zinazotumia mistari mine kwa kila beti ni
kama vile Utendi wa Fumo Liyongo,
Al-inkishafi, Mwanakupona kwa kutaja chache.
Aidha sifa nyingine kama ilivotajwa na
Mulokozi ni utendi kuelezea matukio au masuala muhimu ya kihistoria au kijamii.
Utendi wa Rasi ‘iGhuli una sifa hii kwani unahusu masuala ya kihistoria
hususani historia ya kuanzishwa kwa Uislamu huko Saudi Arabia na Yemen katika
karne ya saba.
Kigezo
kingine kinachojitokeza katika Utendi wa
Rasi ‘lGhuli ni utendi kuelezea habari za ushujaa na mashujaa.[4]
Mashujaa wanaozungumziwa katika utendi huu ni Mtume Muhammad na masahaba wake
kama vile Seyyidna Ali bin Abdala Talib na Seyyidna Umar bin Khatab. Mathalani
msimulizi anatueleza jinsi shujaa Ali alivyofanikiwa kumuua Rasi ‘iGhuli
anatueleza kuwa Rasi ‘iGhuli baada ya kuona mapigano yamepamba moto anaamua
kukimbilia mjini na kuingia na kumkuta Ali wanapigana hatimaye Ali anaibuka
shujaa kwa kumkata kichwa Rasi ‘iGhuli na kichwa chake kutundikwa juu ya lango
la mji. Rejea kuanzia ubeti wa 4528-4532.
Aidha
utendi huu unakidhi hata vigezo vya utendi vilivyotolewa na Ruth Finnegan
(1970:108-109) hususani kigezo cha urefu na uunganifu ambavyo havijitokezi
katika vigezo vilivyoainishwa na Mulokozi. Mathalani kwa upande wa Urefu shairi
hili linakidhi kigezo hiki. Leo van Kessel (keshatajwa, viii) anatueleza kuwa Utendi wa Rasi ‘lGhuli ndio utenzi mrefu
kuliko zote zilizopata kuchapishwa katika lugha yoyote ile ya Kiafrika. Utendi
huo una beti 4584.
3.0
Sifa
pambanuzi za kifani za utendi andishi wa Kiswahili zinavyojitokeza katika Utenzi wa
Rasi ‘lGhuli
Tunapozungumzia utendi wa Kiswahili tunatakiwa
kuhusisha na dhana nzima ya fasihi ya Kiswahili. Tunaarifiwa kuwa mwanzo mwa
miaka ya 1970 hadi 1990 dhana ya fasihi ya Kiswahili ilizua mjadala mkubwa
miongoni mwa wanataaluma wa fasihi. Wapo waliokuwa wanaona kuwa kuna fasihi ya
Kiswahili na upo upande mwingine uliona kuwa hakuna fasihi ya Kiswahili. kwa
kuwa si lengo la makala haya kujikita katika mjadala huo. Itoshe kusema kuwa,
wataalamu hao walikubaliana kwamba, fasihi ya Kiswahili ni ile inayotumia lugha
ya Kiswahili na hata iliyotafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili, Sengo (1987),
Mazigwa (1991). Aidha Synambo na Mazrui (1990) wanasema kuwa fasihi ya
Kiswahili ni ile iliyoandikwa kwa Kiswahili tu na iwapo inazungumzia utamaduni
wa Kiswahili au utamaduni mwingine. Hivyo basi, kwa mawazo hayo tunaweza kusema
kuwa utendi wa Kiswahili ni utendi ulioandikwa au kusimuliwa kwa lugha ya
Kiswahili na unaozingatia fani na maudhui (utamaduni) ya Waswahili wenyewe au
jamii nyingine maadamu umeandikwa kwa lugha ya Kiswahili.
Ama
kwa hakika, utendi andishi wa Kiswahili una sifa zake pambanuzi za kifani
ambazo huweza kutumika kuzitofautisha na tendi nyingine zisizo za Kiswahili. Wamitila
(keshatajwa, 41) anaeleza fani kuwa ni dhana inayotumiwa kuelezea muundo au
mpangilio wa kazi fulani ya kifasihi au hata sehemu zake. Anaendelea kufafanua
kuwa fani huelezea mbinu na mtindo wa kuyawasilisha yaliyomo au maudhui. Njogu
na Chimerah (2008:312) wanasema, fani ni usanifu wa kazi ya fasihi. Wanaendelea
kufafanua kwamba, fani ni vipengele mbalimbali vya sanaa na jinsi kazi hiyo
inavyojengwa ili kupata maana yake. Hivyo basi katika utendi tunapoangalia fani
tunaangalia tunaangalia vipengele mbalimbali vya sanaa ya utendi wa Kiswahili
ama mbinu au mtindo anaoutumia msimulizi kuwasilisha mawazo yake kwa hadhira.
Ama kwa hakika Utenzi wa Rasi ‘lGhuli unakidhi sifa za kuitwa utendi wa Kiswahili
kutokana na kubeba sifa pambanuzi za kifani za utendi wa Kiswahili. Utendi wa
Kiswahili una sifa pambanuzi zifuatazo za kifani ambazo kwa hakika zinajitokeza
katika Utendi wa Rasi ‘lGhuli:
Kwanza ni matumizi ya fomula. Wamitila
(2003:49) anasema fomula ni istilahi inayotumiwa kuelezea kiunzi cha msuko au
sifa fulani ambazo hutumiwa katika uundaji wa kazi za kifasihi. Anaendelea
kufafanua kuwa usimulizi na utambaji wa hadithi katika fasihi simulizi
hutangulizwa na kianzio cha fomula. Katika tendi za Kiswahili kuna mwanzo wa
kifomula ambapo msimulizi huanza na kuomba dua na kumsifu Mungu na Mtume. Fomula
hii inajitokeza katika Utendi wa Rasi
‘lGhuli ambapo msimulizi anaanza kwa kuomba dua na kumsifu Mungu kama
anavyoanza katika ubeti wa 1-8:
1.
Awali
bisumi ‘llahi
Jina la mola ‘llahi
Pweke
asiye shabihi
Ndiye
wahidi qahari. (unaweza angalia
pia katika ubeti 2-8)
Tukiziangalia beti hizo zinatuonesha
kuwa msimulizi anaanza kwa kuomba dua na kumsifu Mungu (Allah). Hii ni fomula
inayojitokeza katika tendi za Kiswahili. kwa mfano katika utendi mwingine wa
Kiswahili wa Utendi wa Fumo Liyongo
tunaona sifa hii ya fomula ya kuanza na dua na kumsifu Mungu au Mtume
ikijitokeza katika ubeti wa 1. Pia tukiangalia Utendi wa Al-Inkishafi tunaona fomula hii pia ikijitokeza, rejea
ubeti wa kwanza wa utenzi huo.
Aidha
utendi wa Kiswahili unakuwa katika mpangilio wa beti. Utendi wa Rasi ‘lGhuli nao ni utendi unaoundwa na beti, una beti
4,584 na kila ubeti umeundwa na vipande vinne vya mstari ambapo kila kipande
kina mizani nane (8). Aidha beti hizo huwa na vina vinavyofanana katika vipande
vya mwanzo na kina cha kipande cha mwisho ni kinabahari ambacho huishia na -ri kuanzia ubeti wa kwanza hadi wa
mwisho. Hili tunaweza kuliona tukitaza beti zote kuanzia ule ubeti wa kwanza
hadi wa mwisho. Beti hizo tatu tukiziangalia zinatuonesha kuwa kila ubeti una
vipande vinne vya mstari na kila kipande kina mizani 8. Kina bahari kikiwa ni -ri. Abedi (keshatajwa, 16) anasema kila
utenzi wa mizani nane huimbika vizuri.
Vilevile matumizi ya majigambo ni sifa
nyingine inayoitambulisha utendi wa Kiswahili. tendi za Kiswahili huwa na matumizi
ya majigambo. Wamitila (keshatajwa, 107) anaeleza majigambo kuwa ni aina ya
maghani (au sifo) yanayohusu kujisifu au sifa. Anaendelea kufafanua kuwa
majigambo hutongoa utungo wa kujisifu kuhusiana na kitendo fulani, ushujaa,
urijali au matendo muhimu. Katika Utendi
wa Rasi ‘lGhuli tunaona kabla mashujaa hawajaanza kupambana huanza
kujigamba kwanza na kuanza kuelezea sifa na uwezo wao mbele za adui zao. Mfano
mzuri ni Sayyidna Ali anajigamba mbele ya adui wake Zuheri na Zuheri kwa upande
wake anajigamba mbele ya adui yake huyo. Hebu tuangalie ukurasa wa 43 kuanzia
ubeti wa 845-847.
845. Jina langu takwambia 847. Ndimi samba maarufu
Ndi mimi Shekhe Alia Ndimi mvunda sufufu
Ibunu amu Nabia Wajapo
kuwa elfu
Muhamadi ‘lBashiri. Siwajali
sifikiri.
Kwa
upande wake Zuheri naye anamjibu Sayyidna Ali akijigamba kuanzia ubeti wa
865-868 (Rejea beti hizo).
Pia unaweza angalia ubeti 867 na 869. Beti
hizo zinatuonesha namna mashujaa hao walivyokuwa wakijagamba kila mmoja
akijisifu mbele ya mwenzake na mara baada ya kumaliza majigambo hayo huanza
kupambana kwa kupigana rejea ubeti 887-892 (uk. 45). Sifa hii ya majigambo
tunaona pia ikijitokeza katika Utenzi wa
Nyakiiru Kibi. Majigambo hayo
yanaoneshwa na Kanyamaishwa na
Nyakiiru Kibi. (rejea ubeti 383-389)
Sifa nyingine ya utendi wa Kiswahili
inayojitokeza katika Utendi wa Rasi
‘lGhuli ni sifa ya matumizi ya Kiswahili cha Lamu kwani ndiyo husemekana
kuwa ni Kiswahili cha kishairi. Taylor akinukuliwa na Mbaabu (2007:15) kuhusu
lahaja ya Lamu (Kiamu) kuhusishwa na ushairi anasema kuwa, ni ukweli unaotajwa
na Waswahili wenyewe kwamba Kiamu kinasifika kwa utajiri wa lugha ya kishairi. Hivyo
basi katika utendi huo sifa hii inajitokeza kwani kuna matumizi makubwa sana ya
Kiswahili au msamiati kutoka lahaja ya Kiamu.maneno kama ndia likiwa na maana ya njia
ubeti wa 447, nti likiwana maana
ya nchi katika ubeti wa 524, matolikiwa na maana ya macho katika ubeti wa 437 na 462, mtana likiwa na maana ya mchana katika ubeti wa 565 kwa kutaja
maneno machache.
Matumzi
ya Kiswahili cha kale ni sifa pambanuzi nyingine ya utendi wa Kiswahili. Wamitila
(2010:73) anasema utanzu wa ushairi unatumia msamitai wa kale ukilinganishwa na
utanzu wa riwaya au wa tamthiliya. Sifa pia
inajitokeza katika Utendi wa Rasi ‘lGhuli. Utendi umetumia
msamiati wa kale baadhi ya msamiati wa kale unaojitokeza katika utendi huo ni, akima likiwa na maana ya akisimama katika ubeti wa 785 na 818, akita likiwa na maana ya akaita katika ubeti wa 789 na 884.
Si
hivyo tu, utendi wa Kiswahili una sifa ya kuchanganya wahusika wanadamu na
wasio wanadamu. Msokile (1993:32 )
anaeleza kuwa wahusika ni watu , wanyama au vitu katika kazi ya kisanaa
ya kifasihi. Kwa mfano Utendi wa Rasi
‘lGhuli unachanganya wahusika binadamu ambao wanaongozwa na Mtume Muhamadi
na masahaba na wafuasi wa Kiislamu, pia kwa upande mwingine kuna binadamu
makafiri wanaongozwa na Rasi ‘lGhuli lakini pia msimulizi amechanganya na
wahusika wengine wasio binadamu kama vile malaika, Mungu n.k. Mathalani katika
ukurasa wa 13-19 ubeti wa 350-362
anasema;
354. Kiwasili
Jiburili 359. Kanituma nikujie
Akamwambia Rasuli Na maneno nikwambie
Akusalamu Jalali Tuma
mtu amwendee
Salamu nyingi kathiri. Sultani wa kufari.
Tukiziangalia beti hizo tunaona kuwa
kuna wahusika malaika wanajitokeza katika utendi huo. Ukirejea beti ya 354 na
359 tunamwona malaika Jibilii akimpa amri Mtume Muhamadi kwenda kwa Rasi ‘lGhuli.
Aidha kuhusu wahusika Malaika rejea pia ukurasa wa 189 ubeti wa 3761 – 3770 ambapo tunawaona Malaika
wakijitokeza kusaidia majeshi ya Muhamadi katika vita. Aidha kuna mhusika Ibirisi anajitokeza katika
utendi huu, tunamwona ibirisi akijibadilisha maumbo ya watu mbalimbali ili
kuwahadaa Waislamu, kwa mfano kuna wakati anajibadilisha na kuingia katika
sanamu ni kuwahadaa watu kuwa yeye ni Mungu kama msimulizi anavyotuambia katika
ubeti wa 473-476. Tuangalie beti chache:
473. Ibilisi maluuni 475.
Sikuzaa sikuzawa
Achondoka iyo hini Naua na
kufufua
Akangia sanamuni Naumba
nikiumbua
Sultani kumghuri. Ndimi wahidi
Qahari.
Vilevile, kuna wakati ibirisi
anajigeuza Kharid mmoja wa masahaba wa
Mtume Muhamadi na kwenda kuwaambia kuwapa taarifa za uongo kuwa Muhamadi
ameuwawa. Rejea ubeti wa 2397- 2399. Kwa ujumla wahusika kama Lata, Uza na
Manata, miungu ya uongo wa kike, Ibirisi na shetani ambao si binadamu
wanajitokeza katika kazi hii.
Kwa upande mwingine sifa ya matumizi ya
sintaksia au sarufi ya kisimulizi kama sifa ya utendi simulizi pia inajitokeza
katika Utenzi wa Rasi ‘lGhuli. Wamitila
(keshatajwa, 84) anaeleza muundo wa sintaksia unaweza kuwa msingi muhimu wa
kuakisi jinsi mawazo ya mhusika au wahusika wa kifasihi walivyo. Sintaksia
katika usimulizi ina maana upatanisho wa kisarufi unaoibua usimulizi fulani
katika ngano mara nyingi hujitokeza viambishi vya -ki-. Hebu tuangalie ubeti wa 99 (ukurasa 5) na ubeti wa 353
ukurasa wa 18: anaposema;
99.Wakikamata
wanangu 353. Akishuka mualimu
Wakiwafunga
kwa pingu
Ametukua alamu
Wakiwakusa
matungu
Akibalighi salamu
Na mwenyewe
hubusuri.
Akitikia Bashiri.
Hitimisho
Katika makala haya tumefanya uhakiki kwa
kuchambua Utenzi wa Rasi ‘lGhuli kama
unastahili kuitwa utendi wa Kiafrika na vilevile kama unafaa kuwekwa katika
kundi la tendi za Kiswahili. ili kujibu maswali hayo tulijikita zaidi kuangalia
vigezo vya utendi wa Kiafrika lakini pia tukaangalia utendi huo kama unakidhi
vigezo vya kuitwa utendi wa Kiswahili kwa kumakinikia zaidi katika sifa
pambanuzi za kifani na kimuundo za utendi wa Kiswahili. Ama kwa hakika baada ya
kupitia vigezo hivyo na utendi husika tunakubaliana kuwa Utenzi wa Rasi ‘lGhuli kama tulivyoona hapo juu ni utendi unaokidhi
sifa za kuitwa utendi wa Kiafrika kutokana na kukidhi vigezo vya utendi wa
Kiafrika kama vilivyotajwa na Mulokozi (keshatajwa, 11) lakini pia unakidhi
vigezo vya kuwa utendi wa Kiswahili na hii si kwasababu tu umeandikwa kwa lugha
ya Kiafrika au Kiswahili ni kwa sababu umekidhi vigezo vyote vya utendi wa
Kiafrika na Kiswahili.
[1]
Majina mengine ya Mtume Muhamadi kati utenzi huu ni kama vile, ‘lBashiri,
Mursali, Rasua, Rasuli
[2]
Majina yake mengine yanayojitokeza katika utenzi, Shekhe Ali, Aba ‘lHasani,
Haidari (samba), Imamu, Jabali Abu Qubesi
[3]
Ni wilaya inayopatikana Tanzania Bara katika Mkoa wa Pwani.
[4]
Shujaa ni mtu mwenye moyo thabiti anayeweza mambo hata kama ni ya hatari TUKI
(1981:258). Aidha Mlokozi (1999:11) anataja sifa za shujaa kuwa ni nguvu za kimwili
na nguvu za kiume, kuwa na nguvu za uganga na sihiri, kuwa na mshikamano na
kundi au jumuiaya fulani.
Simu: 0715 33 55 58
No comments:
Post a Comment