MGOMBEA URAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO SI WA CHAMA CHA SIASA, NI WETU SOTE NA TUNAHAKI YA KUMJADILI
Bado niko katika bumbuwazi kwamba watu niliowafahamu kwa takribani miaka mitatu kama watetezi wenzangu wa maoni ya Wananchi yaliyojumuisha misingi ya maadili na uwajibikaji, leo ndio wanaoongoza kunitukana, kunibeza na kunisema kwamba mimi sipendi mabadiliko.
Nakumbuka mwaka 2013 nilianza safari ngumu sana, safari ambayo ilinitaka kuchagua upande, ama niendelee kupiga kelele za kudai kuheshimiwa maoni ya Wananchi au nikae kimya ili nisiharibu “future” yangu, inayojumuisha mafanikio katika maisha yangu siku zijazo. Niliamua kupuuza maelezo ya “future” au maisha mazuri yaliyo mbele yangu na kuamua kuchukua upande wa kutetea maoni ya Wananchi ambayo mimi na wenzangu wajumbe wa Tume ya Warioba tulishiriki kuwasikiliza watanzania kote nchini Tanzania.
Sikuwa nimetegemea ingekuwa safani ngumu, nilimwomba Mungu kwamba mapenzi yake yatimizwe, sikuwa na amani ya nafsi kukaa kimya dhidi ya upotoshwaji, uchakachuaji na kuona watanzania hawaelewi ni nini hasa kilichokuwa kinaendelea sio tu nyuma ya pazia lakini pia ndani ya Bunge Maalum la Katiba. Nilijiapiza kwamba, bora nipoteze mambo mema kwa ajili yangu binafsi lakini niishi kwa amani na kwamba sikuukana ukweli. Mimi ni muumini nina hofu ya Mungu, nilijua kama nimeandikiwa kukosa na kupoteza mambo ya kibinadamu, heshima ya kidunia inayoambatana na kufurahiwa na watu wote kwasababu ninasema wakitakacho na sio nikiaminicho, nikajieleza sana basi nitabaki na tumaini moja tu, kwamba nina Mbingu na huko ku bora zaidi kuliko niyakosayo sasa.
Kipindi chote kutoka mwezi juni 2013, kiliambatana na matusi, kebehi na kubezwa sana, baadhi ya watu wa CCM walisema nimenunuliwa, ni kiasi gani cha fedha nimelipwa kulisaliti Taifa langu. Wako walioniuliza hawa wahuni wa UKAWA wamekupa shilingi ngapi ambayo nimekubali ivunje heshima yangu? Hali ilizidi kuwa tete hata ikafika kipindi kwa maelezo haya ya mimi ama kupewa fedha na wafadhili hasa watu wa UKAWA, ikabidi hata Taasisi nyeti za Nchi yetu kunifungulia jarada, sikukata tama, wazazi wangu wakatishwa, sikukata tamaa.
Nakumbuka niliwaeleza baba na mama kwamba kazi yao kubwa waliifanya katika maisha yangu ilikuwa kunijenga katika misingi ya maadili ya dini na kunipa elimu ya namna ya kuishi na watu wengine na elimu ya shule. Nikawaambia kwa haya yanayoendelea ninayamudu kwa uwezo wa Mungu na wao waniombee tu kwasababu ninachosimamia ni kweli, namshukuru Mungu walinielewa hata kwa yanayoendelea leo.
Kwa msimamo ule nilipoteza marafiki kadhaa, marafiki wa rika langu lakini pia nilipoteza urafiki na watu wakubwa na watu wenye mamlaka makubwa kwenye nchi yetu. Baada yake nilibaki na wanaCCM kadhaa ambao waliniamini, marafiki zangu wapya wa iliyokuwa Tume na marafiki wachache walionifahamu kwa muda mrefu.
Katika Makala zangu kadhaa nimeeleza kwamba UKAWA hapaswi kubezwa, UKAWA ni mdau mkubwa katika ujenzi wa demokrasia ya Taifa letu. Nimeendelea kusema CCM imara ni ile inayoheshimu msingi huu kwamba wadau kama UKAWA wanakuwepo na kuwa sehemu ya ujenzi wa demokrasia. Nikaendelea kusema kwa anayedhani kwamba tatizo letu ni CCM pia hayuko sahihi, kama ambavyo baadhi ya wana CCM wanaidharau UKAWA nao niliwaambia hawajitambui.
Mimi kama mwana CCM, niliweka Taifa kwanza na kuamua kushirikiana na watanzania wote waliopenda Katiba Mpya inayotokana na maoni ya Wananchi na hasa hasa katika kusimamia misingi ya Maadili na Uwajibikaji. Nilishirikiana na viongozi kadhaa kutoka CCM wakiwamo wabunge, viongozi kadhaa wakiwemo wabunge kutoka CUF, Chadema na NCCR Mageuzi.
Niliamini kwamba tulikuwa na uelewa wa pamoja kwamba watu waliotaka madaraka kwa nguvu walivuruga mchakato wa Katiba. Watu waliotaka madaraka ya Rais makubwa walivuruga mchakato wa Katiba, watu hawa walitaka Urais wa kifalme, usiohojika na walifanikiwa kumshinda hata Mwenyekiti wa CCM. Mimi ni mwana CCM na nilijua yaliyokuwa yanaendelea ndani ya CCM na nguvu ya wale waliokuwa wanakwamisha maoni ya Wananchi hasa yale yahusuyo maadili, nilitaka kuvunjika moyo lakini dhamira ilisema utawakosea watanzania.
Katika kujaribu kuwaelewesha faida za rasimu ya Warioba, nilionana na wana CCM wengi kwa majadiliano ya kina, wazee kwa vijana na viongozi pia. Katika nilio onana nao alikuwapo Mhe. Lowassa, tulikuwa na kikao cha zaidi ya saa 2 na tukamfafanulia Rasimu na hasara ya kilichokuwa kinaendelea kwenye Bunge Maalum. Mhe. Lowassa alitueleza kwamba yeye anataka Muungano wa serikali 2 na zitakazowapa Zanzibar kila kitu na kubaki na Ulinzi na Usalama. Tukamweleza huko itakuwa ni kuvunja Muungano kwasababu huwezi kuwa na serikali 2 na Zanzibar ina kila kitu, tafsiri yake ni kwamba Rais wa Muungano atakuwa wa Tanganyika pekee na Rais wa Zanzibar kwa Zanzibar, hiyo ingekuwa Nchi Mbili na Serikali Mbili, hakuna Muungano hapo, hakuelewa na alishikilia msimamo huo.
Tunaweza kuwa na tofauti za kiitikadi, lakini tofauti hizi zinakuwa si kitu pale ambapo tunalitizama Taifa. Ninaposema kulitizama Taifa nazungumzia kuiishi misingi ambayo itahakikisha haki za watu wetu zinatolewa. Haki haiwezi kutolewa wala kupatikana iwapo misingi ya maadili na uadilifu inakandamizwa. Kiongozi ambaye marafiki zake wakubwa ni matajiri, hawezi kusimamia matajiri hawa walipe kodi. Kiongozi ambaye mtaji wake wa kisiasa ni fedha zake zisizo na majibu na michango ya marafiki zake matajiri, siku akipewa dhamana atajinasib zaidi na matajiri na sio masikini.
No comments:
Post a Comment